WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa (KUU) wa Mwanza imchukulie hatua za
kisheria mfanyabiashara aliyekamatwa kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya
zana haramu za uvuvi.
“Yuko mfanyabiashara anaitwa
Jeremiah Asam Omolo ambaye amekamatwa mara kadhaa kwa kukutwa na nyavu haramu.
Wizara ilitoa specifications (aina ya
nyavu) zinazoruhusiwa kutumika na KUU ya Mkoa ikasimamia lakini kuna maafisa wa
Wizara waliingilia zoezi hilo mara tatu na akatozwa faini mara zote,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
leo (Jumatano, Aprili 15, 2020) wakati akizungumza na Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Mkoa wa Mwanza kwenye kikao alichokifanya
kwa njia ya video (video conference) kutokea ofisini kwake Mlimwa,
jijini Dodoma.
Amesema kwa kuwa si mara
yake ya kwanza kukamatwa, KUU ya Mkoa haina budi kuchukua hatua kali zaidi kwa
sababu nia ya kutoa adhabu ni kumfanya mkosaji asirudie kosa lakini mfanyabiashara
huyo amekuwa akilipa faini na kurudia makosa yaleyale.
Kwa
upande wake,
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella alisema katika kosa la kwanza, mfanyabiashara
huyo alipatikana na marobota 66 ya nyavu haramu aina ya makila sawa na vipande
13,200 ambapo alitozwa faini ya sh. milioni 50.
Amesema katika tukio la
pili, Aprili 3, mwaka huu, Bw. Omolo alikutwa na zana haramu za uvuvi aina ya makila
vipande 6,964 na Timba vipande 179 na kutozwa faini ya sh. milioni 129.8.
“Katika tukio la tatu, Aprili
4, 2020 alipatikana na kosa la kumiliki zana haramu za uvuvi ambazo ni marobota
10 ya nyavu haramu aina ya makila sawa na vipande 300 na marobota 437 ya nyavu
haramu aina ya Timba sawa na vipande 12,875 na kutozwa faini ya sh. milioni 300,”
alisema.
Alisema uongozi wa mkoa uliamua
kuunda timu ya wataalamu inayojumuisha vyombo vya usalama ambayo itafuatilia na
kuchunguza kwa undani mienendo ya mtuhumiwa huyo ikiwemo masuala la kikodi na
ufanyaji wa biashara.
Mkuu huyo wa Mkoa alimweleza
Waziri Mkuu kwamba timu hiyo iliyoundwa Aprili 9, mwaka huu, itapaswa kukamilisha
kazi yake na kukabidhi taarifa yake, Jumatatu ijayo (Aprili 20, 2020).
Wakati
huohuo, Waziri
Mkuu amekemea mikusanyiko inayofanyika kwenye nyumba za ibada kwa kigezo cha
kutaka watoto wasikae majumbani kwa vile hawaendi shuleni.
“Ninazo taarifa kwamba
wameanzisha mfumo wa kupeleka watoto kwenye madarasa ya dini. Tumeruhusu ibada tu, na hizo ibada
lazima ziangaliwe ziwe za muda mfupi kadri inavyowezekana. Tumesisitiza kwenye
makanisa au misikiti ambako ibada zinafanyika, waumini wakae kwa kuachiana
nafasi.”
Amesema changamoto
inajitokeza kwenye makanisa makubwa ambayo yana waumini karibu 3,000. “Hayo
sasa yatakuwa ni makongamano. Tunaaamini Maaskofu na Mufti wataliweka vizuri
suala hili,” amesema.
Amesema Serikali haitazuia
biashara kwenye masoko, maduka au supermarkets
isipokuwa amewataka wenye biashara hizo wahakikishe wanaweka ndoo za maji na
sabuni ili wateja wanawe mikono kabla ya kuingia kupata huduma na wakati
wanapotoka kupatiwa huduma hizo. Vilevile, amehimiza wananchi wazingatie kukaa
umbali wa zaidi ya mita moja kutoka kwa mtu mwingine.
Kuhusu mikusanyiko mingine,
Waziri Mkuu amesema watu wanapaswa wajizuie kwenda kuzagaa kwenye vituo vya
mabasi na kama hawana shughuli za lazima za kufanya huko, basi wabakie majumbani
kwao.
Majaliwa akizungumza
kwa njia ya video na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa
Mwanza akiwa ofisini kwake, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 15, 2020.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment