Na Denis Mlowe, Iringa
KATIKA kuunga mkono mapambano
dhidi ya ugonjwa Corona nchini Umoja wa Waendesha Bajaji Manispaa ya Iringa
(UMBI) wamefanikiwa kutoa msaada kwa vituo viwili vya watoto wanaoishi katika
mazingira magumu msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh milioni 3
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo,
Mwenyekiti wa Umoja huo, Norber Sumka alisema kuwa lengo la msaada huo ni
kuungana watoto katika kipindi hiki kigumu cha mapambano dhidi ya virusi vya
Covid 19 kwani watu wengi wamejisahau kama kuna watoto hawa wanahitaji msaada
wa vitu mbalimbali.
Alisema kuwa baada ya
kuwatembelea na kubaini changamoto ambazo wanakabaliana walikaa kama uongozi na
kuchangishana na wadau mbalimbali wakiwemo madereva wote wa bajaji na kuweza
kupata vitu mbalimbali ambavyo wamekabidhi kwa vituo vya watoto wanaoishi
katika mazingira magumu vya Tosamaganga na Faraja Care Center vilivyoko
manispaa ya Iringa.
Alisema kuwa vitu ambavyo
wamefanikiwa kutoa ni magodoro, unga wa ugali, mchele, nguo, sukari, sabuni,
nepi kwa ajili ya watoto, matunda mbalimbali ambapo vitu hivyo vimegaiwa kwa
vituo hivyo viwili vikiwa na thamani ya zaidi ya sh milioni 3.
Alisema kuwa kupitia utaratibu huo
wa kurudisha faida katika jamii ametoa wito kwa wadau wengine kujitoa katika
kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwani kwa kipindi hiki cha
ugonjwa wa corona hali ya vituo hivyo ni ngumu na kuwafanya wazidi kuishi kwa
shida.
Kwa upande wake, Katibu wa UMBI,
Salum Gerald alisema kuwa Corona wanakabiliana na njia nyingi licha ya elimu
kubwa inayotolewa na serikali kwa upande wao wamebaini kwamba watoto hao
wanahitaji mahitaji mbalimbali kutokana na mazingira wanayoishi
Alisema kuwa kitendo cha serikali
kufunga shule na watoto hao kurudi katika vituo ina maanisha kwamba wako tayari
karantini hivyo jukumu letu kama jamii kuwasaidia chakula na vitu mbalimbali
kuweza kupunguza changamoto wanazokabiliana nazo wakiwa ndani ya vituo
wanavyolelewa.
Alisema kuwa jamii inapaswa
kutambua na kujitoa katika kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu
na kuwajali kwa kila namna ili waweze kuishi kwa upendo kama ambapo wangekuwa
katika familia zao hivyo msaada huo utawasaidia kwa kiasi kidogo.
“Japo msaada sio mkubwa sana
kukidhi mahitaji ya watoto yatima,bali itasaidia kidogo kufanya watoto wajisike wapo kama
watoto wengine wenye wazazi kwani kutoa ni moyo hivyo ni wakati huu wa mapambano
dhidi ya corona kuna umuhimu mkubwa sana kwa watu kujitolea vitu mbalimbali kwa
watoto hawa” alisema
Alisema kuwa watoto yatima ni
wahanga wa matatizo yetu katika jamii ndio maana wapo hivyo sio jukumu la
serikali pekee kuwahudumia watoto hawa kutokana na umuhimu wao katika jamii
kwani ndani yao kuna watoto watakaokuja kuwa kuwa Profesa, madaktari bingwa na
wanasheria hivyo kuwatembelea ni njia mojawapo ya kuwafanya wapate moyo wa
kusoma zaidi na kujitoa.
Kwa upande wao viongozi wa vituo
hivyo, Father, Franco Sordella wa kituo
cha Faraja na Sister Winfrida Mhongela
wa kituo cha Tosamaganga walishukuru umoja wa bajaji kwa kuwakumbuka kwa
misaada hiyo na imekuja kwa wakati mwafaka kutokana na changamoto nyingi ambazo
wanakabiliana nazo katika vituo.
Walisema kuwa kitendo cha UMBI
kuwakumbuka kwa misaada hiyo wakati dunia nzima inapambana na Corona na misaada
ya wadau mbalimbali inakwenda huko hakika ni faraja tosha kabisa kwa watoto
ambao wamekuwa wakisaulika na jamii kwa kudhani vituoni wanapata kila kitu.
Father Franco alisema kuwa licha
ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ndani ya kituo kuhusu watoto alisema
kuwa changamoto kubwa kituoni hapo ni suala la umeme na maji ambapo umeme
alipofatilia kwa kipindi cha miaka mitatu ni gharama kubwa kuliko matarajio yao
ambapo milioni zaidi ya 52 alizotajiwa na shirika zilimshinda.
Kwa upande wake Sister Winfrida
Mhongole alisema kuwa changamoto kubwa katika kituo hicho ni baadhi ya walezi
hawaji kuwasalimia wala kuwachukua watoto sasa tunapata shida wakati
wanapotakiwa kurudi nyumbani, maana umri wa mwisho wa kukaa kituoni hapa ni
miaka 6.
Alisema kituo kinapokea watoto
wasio na mama au wenye mama ambaye ni anatatizo la akili, na kuwa baadhi ya
ndugu ndiyo wamekuwa wakiwatelekeza watoto mara tu wanapowafikisha kituoni
hapo.
Changamoto nyingine
zinazowakabili watoto ni baadhi ya wazazi kushindwa kuwaendeleza kielimu
watoto, kwani baadhi ya walezi huwa hawana mwamko wa kuwaendeleza watoto hao,
na hivyo kusababisha watoto hao kutoendelea na masomo.
Vituo hivyo ambavyo jumla vina watoto zaidi ya 240 kwa kuwa kituo cha Tosamaganga
pekee kina watoto 180 ambapo wanaishi kwenye vituo hivyo huku kituo cha faraja
kina watoto zaidi 60 ambao wanaishi katika vituo hivyo na kuhitaji msaada wa
vitu mbalimbali.
Mwenyekiti
wa Umoja wa waendesha bajaji, Norbet Sumka, akikabidhi moja ya misaada
mbalimbali kwa Padre Franco Sordella ' Mwakilasi' kwa ajili ya kituo cha
watoto wanaoishi mazingira magumu cha Faraja Care Center (Picha na
Denis Mlowe).
No comments:
Post a Comment