![]() |
Mchungaji Getrude Rwakatare |
Na Mwandishi Wetu
MCHUNGAJI wa
Kanisa la Mlima wa Moto (Mikocheni B)
Askofu Getrude Rwakatare amefariki
dunia.
Mchungaji Rwakatare
ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alifariki
dunia jana alfajiri katika Hospitali ya Ribininsia jijini Dar es Salaam wakati akiendelea na matibabu.
Kifo cha askofu Rwakatare kimewagusa watu wa kada mbalimbali ambao mara baada ya tangazo la kifo
chake kila mmoja kwa wakati wake na kwa namna walivyomwelewa kiongozi huyo wa
kiroho, walilizwa na kifo chake cha ghafla.
Waliotikiswa zaidi na
msiba huo ni waumini wa kanisa lake, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano,
walimu, wanafunzi na wazazi ambao watoto wao wanasoma katika shule zake maarufu
za St. Marys.
Miongoni mwa walioguswa
na kifo cha Mchungaji Rwakatare ni Rais John Magufuli.
Katika salamu zake za
rambirambi, Rais Magufuli alielezea kusitushwa na msiba huo na kutuma salam za
rambirambi kwa familia, wabunge na waumini wa Kanisa la Mlima wa Moto kufuatia
kifo cha Mchungaji Rwakatare.
Katika salamu hizo,
Rais Magufuli ameelezea alisema Askofu Rwakatare alikuwa mcha Mungu, mwenye upendo, asiye na
majivuno, aliyepigania umoja na amani na aliyeipenda nchi yake kwa dhati.
Pamoja na kutoa pole
kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki, Rais Magufuli alimwomba Spika wa Bunge
Job Ndugai kufikisha salamu zake za pole kwa wabunge wote na pia amewapa pole
waumini wa Kanisa la Mlima wa Moto ambalo Askofu Rwakatare alikuwa kiongozi
wake.
“Katika kipindi hiki
cha majonzi, tumuombee Askofu Rwakatare apumzike mahali pema peponi, na
nawasihi waumini wa Kanisa la Mlima wa Moto muendelee kuwa wamoja na muendeleze
mazuri yote yaliyofanywa na Askofu Rwakatare wakati wa uhai wake,” alisema Rais Magufuli.
Naye Spika Ndugai,
alisema kuwa amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha
Mchungaji Dk. Rwakatare.
Kwa mujibu wa taarifa
kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa
Kimataifa Ofisi ya Bunge, Ndugai alisema anatoa pole kwa wafiwa wote wakiwamo
familia ya marehemu, ndugu, jamaa, wabunge na waumini wa Kanisa la Mlima wa
Moto (Mikocheni B Assemblies of God).
“Mwenyezi Mungu awape
moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” alisema Spika Ndugai
katika taarifa hiyo.
Aidha, Spika Ndugai
alisema ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia ya marehemu inaratibu
mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.
Akizungumzia kifo
hicho, Mchungaji wa kanisa hilo, Stanley Nnko alisema Askofu Rwakatare
amefariki dunia baada ya hali yake kubadilika ghafla na kupelekwa katika
Hospitali ya Rabininsia iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam.
Alisema mchungaji
Rwakatare alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na presha na ndio
magonjwa yaliyosababisha kifo chake.
“Baada
ya afya ya mama
kubadilika alipelekwa hospitalini ambapo
alibainika kuwa anasumbuliwa na presha na kisukari, juhudi kubwa
zilifanyika katika kuokoa maisha yake lakini hazikuzaa matunda,”
alisema Nnko.
Nnko alisema hadi sasa
bado hawajatoa taratibu za mazishi kwani bado wanaendelea na vikao hadi pale
watakapopata taarifa kamili kutoka kwa timu ya madaktari waliokuwa wakimtibu.
"Waumini wa kanisa
letu baadhi tumekusanyika kanisani na upande wa familia wapo nyumbani
wakiendelea na vikao vya kifamilia, huku tukisubiria mwongozo kutoka kwa
daktari ili tujue namna gani tutaweza kumpumzisha mpendwa wetu," alisema
Mchungaji Nnko.
Hata hivyo, aliwataka
waumini na wananchi wote kuendelea kuwa wavumilivu hadi pale taarifa kamili
zitakapopatikana na zaidi waendelee na maombi ya kumuombea Mchungaji Rwakatare,
ili apumzike kwa amani.
Mwanae Muta Rwakatare
alithibitisha kifo cha mama yake na kwamba alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa
moyo ambapo hali ilibadilika na kumkimbiza hospitali.
Mchungaji Rwakatare alizaliwa 31 December
1950, alisoma Shule ya Msingi Ifakara kuanzia
mwaka 1962 na kumaliza elimu ya sekondari 1971 na
baadae alisoma chuo kikuu.
1987 aliazisha shughuli
mbalimbali za kijamii kama Shule ya msingi na Sekondari za St.Mary katika Mkoa
Dar es Salaam, Morogoro, Mbeya, Dodoma na Mwanza Chuo cha Uwalimu cha St.Mary.
Mwaka 1995 aliazisha
Kanisa la Assemblies of God Mikocheni B,
ambapo kabla ya hapo alifanya kazi katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)
jijini Dar es Salaam na alipata PH.D Digrii ya Maendeleo ya Jamiii na Elimu Kristo
Mwaka 2006 aliazisha
Kituo cha kulelea watoto yatima ambacho kilikuwa kinafadhiliwa na kanisa lake.
Mwaka 2007 ateuliwa na
Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete kuwa Mbunge wa Viti Maalum 2007 ambapo
alihugumu 2010.
Pia marehemu Getrude
amekuwa kada wa muhimu CCM kwa miaka mingi hadi anakutwa na umauti.
No comments:
Post a Comment