Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa (katikati), akipata ufafanuzi kuhusu matumizi ya mashine
ya Cherehani katika utengenezaji wa Barakoa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Kiwanda cha Uchapishaji cha Five stars, Ashik Abbas Karim (kushoto), leo
Aprili 20, 2020 alipokua katika ziara ya Jijini Dar es Salaam ya kutembelea
Viwanda vinavyozalisha Barakoa na Vitakasa Mikono.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa (katikati), akisikiliza kwa makini maelezo ya eneo la
uzalishaji kutoka kwa Msimamizi wa Mradi wa Uzalishaji Vitakasa mikono kutoka
Kampuni ya Total, Umesh Ankoleker (kulia) leo Aprili 20, 2020 alipokua
katika ziara ya Jijini Dar es Salaam ya kutembelea Viwanda vinavyozalisha
Barakoa na Vitakasa Mikono.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa (kulia), akipata ufafanuzi kuhusu mtambo wa kutengeneza
Barakoa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Uchapishaji cha Five
stars, Ashik Abbas Karim (kushoto), leo Aprili 20, 2020 alipokua katika
ziara ya Jijini Dar es Salaam ya kutembelea Viwanda vinavyozalisha Barakoa na
Vitakasa Mikono.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, amebainisha kwamba Serikali imejipanga kuzalisha zaidi ya
Barakoa Milioni tatu na nusu kwa mwezi ili kukidhi mahitaji ya Watanzania wote.
Hayo ameyasema leo Aprili 20, 2020
alipokua katika ziara ya Jijini Dar es Salaam ya kutembelea Viwanda
vinavyozalisha Barakoa (face mask) na Vitakasa mikono (Hand sanitizer) ambapo
kwa siku ya leo ziara hiyo imefanyika katika Kiwanda cha Uzalishaji cha Prestine,
Kiwanda cha Uchapishaji cha Five stars na Kiwanda cha Uzalishaji Mafuta na
Vilainishi cha Total.
Waziri Bashungwa ameeleza kwamba
Uzalishaji wa Barakoa za kutosha kwa sasa ni muhimu sana na Serikali
inahakikisha kwamba Viwanda hivi vinapata malighafi ya kutosha ili viendelee
kuzalisha vizuri.
“Kiwanda cha Prestine sasa hivi
kinatengeneza Barakoa elfu thelathini kwa siku (30,000) lakini baada ya vifaa
kuingia kitazalisha elfu hamsini kwa siku (50,000) na Kiwanda cha Five Star
kitazalisha barakoa laki moja kwa siku (100,000) hivyo kwa ujumla Viwanda hivi
vitazalisha barakoa zisizopungua milioni tatu na nusu kwa mwezi mmoja
(3,500,000) hii ni hatua muhimu sana.”alisema Waziri Bashungwa.
Akizungumza kuhusiana na ziara yake
katika Kiwanda cha Total Waziri Bashungwa ameeleza kwamba Uongozi umekubali
kushirikiana na Serikali katika kuzalisha vitakasa mikono na tayari maandalizi
ya awali yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuangalia sehemu ambayo itatumika kwa
ajili ya uzalishaji.
“Baada ya kuangalia Kiwanda na eneo
maalumu ambalo wamelitenga kwa ajili ya uzalishaji wa vitakasa mikono, na kwa
uwezo wa kiwanda hiki kwa siku kitakua na uwezo wa kutengeneza lita elfu sita
(6000) ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kudhibiti ugonjwa huu.”
Aliongeza Waziri Bashungwa.
Katika hatua ya mwisho Waziri
Bashungwa ametoa wito kwa watanzania “Natoa wito kwa wazalishaji wengine
kujitokeza na Serikali tutawapa ushirikiano wa kipekee, Pia Tuendelea
kuzingatia melekezo na kanuni za kujikinga na Maambukizi ya virusi vya Corona
(COVID -19).”
No comments:
Post a Comment