Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Dkt Angeline Mabula akizungumza na Wakurugenzi na Watendaji wa sekta ya rdhi
katika halmashauri za mkoa wa Simiyu juzi akiwa katika ziara yake ya kukagua
utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi Festo Kiswaga na wa tatu kulia ni Katibu Tawala Msaidizi mkoa wa Simiyu
Maganga Simon.
Watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za
mkoa wa Simiyu wakiwemo Wakurugenzi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) alipofanya ziara
kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa huo juzi.
Mkuu wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Festo Kiswaga akizungumza wakati wa
kikao baina ya Watendaji wa sekta ya ardhi wa halmashauri za mkoa wa Simiyu na
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
alipofanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya rdhi katika mkoa huo
juzi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akifuatilia wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi katika mfumo wa kielektroniki wa
kuhifadhi kumbukumbu za wamiliki wa ardhi
katika halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu juzi akiwa katika
ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Kulia ni Mkuu wa Kitengo
cha Kodi wizara ya Ardhi Denis Masami.
Na Munir Shemweta, WANMM SIMIYU
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wamiliki wa ardhi
wanaotaka kilipia kodi ya pango la ardhi kufanya hivyo kupitia mitandao ya simu
za viganjani ili kuepuka misongamano inayoweza kuchangia maambukizi ya virusi
vya Corona.
Dkt Mabula alitoa
tahadhari hiyo juzi wilayani Bariadi mkoani Simiyu alipozungumza na Wakurugenzi
na Watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Simiyu akiwa
katika ziara ya kuangalia utendaji kazi wa sekta hiyo sambamba na kufautilia
maagizo aliyoyatoa kuhusiaa na sekta ya ardhi.
Alisema, ni vizuri
katika kipindi hiki ambacho kuna maambulizi ya virusi vya Corona wamiliki wa
ardhi wakachukua tahadhari ya kutokwenda ofisi za ardhi kulipia kodi ya pango
la ardhi na badala yake wafanye malipo kwa kutumia mitandao ya simu.
Kwa mujibu wa Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, malipo ya kodi ya pango la ardhi
yanaweza kufanyika kwa kutumia mitandao yote ya simu za viganjani pamoja na kutembelea tovuti ya Wizara.
‘’Katika kipindi hiki
ambacho kuna maambukizi ya virusi vya Corona wadaiwa pamoja na wale wanaotaka
kilipia kodi ya pango la ardhi wakafanya hivyo kupitia mitandao ya simu pamoka
na kutembelea tovuti ya Wizara ili kuepuka misongamano inayoweza kuchangia
maambukizi’’ alisema Dkt Mabula
Akigeukia suala la
makusanyo ya kodi ya Pango la Ardhi katika halmashauri za mkoa wa Simiyu, Dkt
Mabula ameoneshwa kutoridhishwa na kasi ya ukusanyaji kodi ya ardhi katika
halmashauri za mkoa wa Simiyu pamoja na mkoa huo kusifika katika masuala ya
uwekezaji.
‘’ Mkoa wa Simiyu
mapato yatokanayo na kadi ya pango la ardhi yako chini sana, lengo la makusanyo
kwa mkoa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 ni kukusanya bilioni 10 lakini
kiasi mlichokusanya hadi sasa ni milioni 190 tu sawa na asilimia 9.1, inaonesha
hamjawa makini kufuatilia madeni’’ alisema Dkt Mabula
Aidha, Naibu Waziri
Mabula alisema hata malengo ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi yaliyowekwa
katika baadhi ya halmashauri hayaendani na hali halisi na kutolea mfano wa halmashauri
ya Busega kuwa na lengo la kukusanya milioni 30 wakati inadai
milioni 343 kutoka kwa wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi.
Kaimu Mkuu wa mkoa wa
Simiyu ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga alimuhakikishia Naibu
Waziri wa Ardhi, halmashauri za mkoa huo
zitaanza kuwafuatilia wadaiwa wote wa kodi ya pango la ardhi sambamba na kuhakikisha viwanja vinaingizwa katika
mfumo na kuwahamaisha wananchi kuchukua hati za ardhi ili kuongeza kasi ya
makusanyo ya kodi ya ardhi.
Kiswaga alipongeza
maboresho mbalimbali yanayofanywa na wizara ya ardhi katika masuala ya utoaji
huduma hizo na kutolea mfano uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa kuwa ni moja
ya mambo yatakayoleta ufanisi katika sekta ya ardhi.
No comments:
Post a Comment