HABARI MSETO (HEADER)


April 01, 2020

TATHMINI GHARAMA KABLA YA KULIPA KWA TEKNOLOJIA

Maendeleo yanakuja na mambo mengi mazuri, mfano hapo awali ili kuwasiliana na ndugu zako mkoa mwingine ilikuwa ni lazima usafiri, au uandike barua na uende kilomita kadhaa udumbukize kwenye sanduku la posta na posta waisafirishe pengine wiki mbili ndipo ifike kule inapokwenda, mpaka ujibiwe  miezi kadhaa inakuwa imepita.


Taarifa kama misiba kwa watu walio mbali walikuwa wanazipata muda mrefu baada ya mazishi, redio ilikuwa moja tu, Redio Tanzania huu ni mfano tu. Taasisi za fedha zilikuwa chache sana,  benki ilibidi ujaze karatasi nyingi, faili lako litafutwe uli kutambua sura na saini yako. 
Foleni zilikuwa ndefu sana, kwenda benki ilikuwa ni shughuli ambayo lazima uitengee muda tena wa kutosha. Kwa kifupi  teknolojia kwenye Nyanja nyingi hiyo ilikuwa duni sana. 
 
Mabadiliko ya teknologia na ukuwaji wa uchumi ukihuishwa na elimu pana umeleta mapinduzi makubwa sana katika jinsi ambazo tunaweka pesa zetu, leo sio lazima uende benki kuchukuwa au kuweka pesa zako, kwa njia ya simu au kadi unaweza kuchukuwa pesa zako bila kuongea na mtu, yaani mashine tu na kutumia alama mbali mbali kama vidole, nywila, mashine inakupa hela huhitaji kuongea na muhudumu au meneja wa benki, na miamala hii unaweza ifanya kijijini na hata mjini,  na popote pale duniani.
Katika Nyanja ya uwekezaji unaweza weka akiba kwa simu yako, ukaitumia kama daraja la kukuwezesha kuwekeza, mfano ukachukuwa pesa ukaweka kwa akaunti yako ya akiba benki au ukachukuwa pesa ukawekeza kwenye akaunti yako ya uwekezaji ya UTT AMIS, kwa simu unaweza ukakata bima yako ya afya, unaweza ukanunua piki piki  kwa simu hiyo hiyo na  makusanyo ya kila siku ukayawekeza kila siku kwa simu. Yaani kwa kifupi kukua kwa tekinolojia kuna rahisisha maisha.
Urahisi huu una faida na hasara zake. Wakati faida ni kama vile kuokoa muda, uharaka wa miamala, usalama wa miamala, na kuongeza mzunguko wa fedha kwenye uchumi jambo ambalo ni la kheri hasara zipo pia kama vile gharama zaidi, kupata ujumbe kutoka kwa matapeli, kupoza simu, na kama nywila yako ikaangukia kwenye mikono mibaya.
Baada ya kuunganisha simu yako na akaunti yako ya benki,tayari utakuwa unaweza kufanya miamala, kuna tofauti kubwa sana pale unapokuwa umeishika noti/hela mkononi na kuihesabu ili kufanya malipo fulani. Kwanza ukiishika unaiskia yaani kuna mgusano kati ya mwili wako na hela halisi, unapolipa inatoka mkononi mwako unaiona inapokelewa upande ule unapo lipia bidhaa au huduma fulani na unaona ikipokelewa.
 Wakati wa kulipa unahesabu na ukilipa ndoa yako na pesa hiyo imekwisha sababu unaona vile inakwenda roho inakuuma, na inaweza kukufanya ujiulize mara nyingi ni lazima nivunje hii ndoa, mbona nalipa sana na maswali mengine mengi. 
Lakini kama unatumia simu kulipa au kadi –tunasema kama una chanja hela huioni, uhusiano wako na hiyo hela unakuwa kama uko mbali sana.unakuwa kama vile si wa moja kwa moja. Wakati mwingine haikupi uchungu kwa sababu hakuna mgusano, huioni, ina katwa huko kwa huko, na pengine mpaka uchukuwe taarifa yako ya pesa kutoka benki  au kutoka kampuni ya simu ndipo una stuka kuwa ulifanya miamala ya gharama kubwa sana, na hapo ndipo ambapo kama hukua makini roho inakuuma, macho yanakutoka. Kukosekana kwa msuguano kati ya mkono wako na hela kumekufanya usijisikie kama huja tumia hela kumbe umetumia tena sana tu. 
Swali kubwa la kujiuliza ni wapi nilipe kwa pesa halisia na ni wapi nilipe kwa kutumia simu au kadi za benki na hii itanisaidia vipi kutunza pesa zangu kwa jili ya kuwekeza?
Ukweli ni kuwa ukitembea na hela unaweza kuzipoteza, pochi inaweza ibwa, potea,, kadi na simu  pia zinaweza kupotea  lakini mtu aki okota mathalani ni lazima awe na nywila (password), kwa maana nyingine utakuwa umepoteza simu au kadi ila si pesa. 
Kama unataka kuwa mwekezaji ni lazima ujipema kama kwa kutumia simu au kadi za malipo huikupelekei kuwa na ki-here here cha kutumia pesa hovyo. Unalo jukumu la kuhakikisha kuwa matumizi yako yanakwenda sambamba na bajeti yako.
Katika tafiti za matumizi kwa njia ya simu au kadi inasemekana kuwa watu hutumia asilimia 23% zaidi ikilinganishwa na kama ingekuwa wanalipa kwa pesa moja kwa moja. Hii tukiweka kwa tarakimu ni kuwa kwa kila shilingi 100,000 kuna shilingi 23,000 ambazo ungeziokoa. Ina maana kwa kila milioni ungeokoa shilingi 230,000 na hii kama ni kwa mwezi ina maana kwa mwaka inakuwa shilingi 2,760,000 kwa miaka 10 matumizi haya ambayo si ya muhimu yanaweza kuwa zaidi ya shilingi 27,600,000.
Kwa mtu makini na mwenye kujuwa kuwekeza angewekeza hizo shilingi 230,000 kwa mwezi ambazo amekuwa akizitumia vibaya  kwa riba ya asilimia 12 kwa miaka hiyo kumi angeweza kupata shilingi 52,908,898.98
Uwekezaji wa namna hii unawezekana kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja ya UTT AMIS, kwa mfano huu ina maana miaka 10 umepoteza shilingi 27,600,000 ambayo ungeiwekeza kupitia mifuko ya UTT AMIS ingekupa shilingi 52,908,898.98. Tafiti zinaonyesha kua kuna watu hutumia mpaka aslimia 30 kwa kutokuwa makini na tekinoljia hizi za kisasa. Na pia ukumbuke kadri kipatao chako kinavyokukuwa ndivyo kiasi unachopoteza kinazidi kuwa kikubwa.
Kuumbuka kulipa kwa njia za simu au kadi si vibaya, hizi namna hazina ubaya wowote ule, mbaya ni wewe mtumiaji wa hizo namna. Unachotakiwa kukumbuka ni kila unapotumia kadi au simu ni kma vile umelipa pesa kwa mkono wako kutoka mfukoni kwako yaani ni lazima hiyo njia ya malipo uiweke kwenye maana halisi ya malipo. Ni lazima utafsiri uchungu au furaha ambayo ungepata kwa kulipa ‘cash’.
Uwekezaji wa pamojakpitia UTT AMIS ni daraja zuri sana la kuwekeza, kwani ni rahisi na unapata nafasi ya kuwekeza pesa ndogo ndogo ambazo pengine ungezitumia vibaya, watu wengi wanachanga pesa zao katika mfuko mmoja na kumpa meneja (UTT AMIS) ambaye anaziwekeza pesa hizo kwa kuzingatia waraka wa makubaliono, anaziwekeza kwa ufanisi, huku akizingatia usalama, uwazi na taratibu zote kwa malengo ya kuzipa pesa hizo thamani zaidi. 
Jambo zuri kuhusu uwekeza wa pamoja ni huhitaji kuwa na pesa nyingi ili uwe mwekezaji anzia shilingi 10,000 tu unaweza kuwa mwekezaji hii shilingi 10,000 inaweza kua ile ambayo ungeiteketeza kwa kutumia vibaya au ile uliyo jilipa kwanza yaani ile ambayo ulitenga baada ya kupata kipato fulani ukaitenga kwa ajili ya maisha ya baadae na kuiwekeza na ukafanya hivyo mara kwa mara. 
Na uzuri unaweza kuwekeza kwa simu au kwa kwenda benki ya CRDB na kuweka pesa zako kwenye akaunti yako ya UTT AMIS.
Ili kuwa mwekezaji ni lazima ujisome ujuwe mambo yanayo kuchochea kutumia pesa. Mara nyingi matumizi yanendana na tabia, watu na jamaa iliyo kuzunguka, mtazamo, na pengeni vile mwili unajisikia-tamaa. Kikubwa hapa ni kuangalia pesa unayoweza kutenga kutoka kwenye kipato chako, pesa unayoweza kupata bila kutegemea na kuepuka yale mambo yanayo kufanya utumie pesa vibaya, ili pesa hizo uweze kuzipa thamani zaidi kwa kuwekeza sehemu zenye tija kama vile UTT AMIS.

Kama kuna mazingira ambapo kuwepo kwako pale kunakufanya utumie zaidi ya epuke. Kwa mfano ukiwa baa kama baada ya bia moja au mbili unaanza kunua hovyo hovyo, na malengo yako ni bia mbili basi kunywa nyumbani. Au kama starehe yako ni kuwa baa basi chukuwa pesa ya bia mbili tu. Hii itakusaidia kuokoa hela kwa ajili ya mambo muhimu kama vile kuwekeza kwa ajili  muda wa kustaafu.
Wengine wakiwa na hasira wana kwenda kulewa, badala ya kwenda kulewa vaa raba tembea kilomita mbili mpaka tatu, msongo wa hasira utapungua. Na bado utakuwa umeokoa pesa.
Je ukiwa na bibi au bwana yako unatumia zaidi? Pia ukiwa na marafiki fulani matumizi yako yanongezeka? Marafiki wazuri wanaweza kuwa wabaya pia hususani kama ni vinara wa matumizi. Badala ya kukutana nao sehemu za gharama, kutana nao kwenye baa au migahawa ya bei ndogo. Kumbuka soda coca cola ni hiyo hiyo lakini bei yake hutofautiana kati ya hoteli na hoteli, dukani ni shilingi 600 lakini kwenye hoteli kubwa ni shilingi 2500.  
Je una staili gani ya maisha? Tumia kulingana na mfuko wako, ukiona matumizi yako yanazidi kile kilichopo mfukoni mwako tambua hutaweza kuwa mwekezaji, kuna watu wanapenda maisha ya juu sana. Unachukuwa mkopo wa milioni 20 unaenda nunua gari la pesa yote hiyo ili uonekane?? Mwekezaji atanunua piki piki au gari isiyozidi hata milioni 10, kiasi kilicho baki atawekeza, Badilika acha sifa.

Ili usitoke nje bajeti, hakikisha unafuatilia matumizi yako ikibidi andika matumizi. Hii itakusaidia kufahamu kila shilingi umeitumia vipi. Na kuweza kufanya tathimini ya ni wapi ungetumia vizui zaidi na ni wapi umekosea. Pia itakusaidia kujuwa pesa zako nyingi zinakwenda kwenye matumizi gani zaidi. Ukiweza kuepusha shilingi 3,000 kwa siku inakuwa shilingi 90,000 kwa mwezi, hizi ni pesa nyingi sana kwa mwaka na ni pesa nyingi kwenye uwekezaji wa pamoja katika miaka ya baadae.
Pendelea kulipa kwa keshi badala ya kadi kama Makala hii ilivyo ainisha hapo mwazo. Mambo mengine ya kufanya ni kama vile kupanga malengo ya muda mfupi na yanyo fikika unarekebisha malengo kabla unavyo yamudu. Usiweke malengo ambayo yako nje ya uwezo wako. Jifunze jinsi ya kubajeti sababu bajeti ndiyo njia ya kukupeleka kwenye Uhuru wa Pesa.
KUmbuka kwenye kutumia kuna vitu muhimu, kuna dharura na kuna vitu unavipenda. Mapenzi yasizidi vitu au maswala muhimu, jambo muhimu ni kuwekeza kwa ajili ya kesho yako, kurahisisha maisha zaidi.
Kumbuka si rahisi kutokuwa na madeni, weka mpango wa kulipa madeni yako. Kumbuka madeni yenye riba ni hatari sana kwani muda unavyokuwa mrefu ndivyo mzigo unakuwa zaidi. Mikopo inatakiwa iwe ni kwa ajili ya kufanya maisha yawe bora na si kuyanya yawe magumu au mzigo usio bebeka. 
Ki ujumla kuna faida nyingi sana kiuchumi kwa kutumia simu kama chombo cha kufanya miamala, utalipia mahitaji yako sokoni, dukani n ahata hosipitali,  Utalipia bili za maji, umeme, kodo za nyumba, viwanja, bima na mabo kadha wa kadha.   Kulipa kwa simu ni rahisi na haraka, na pia salama kwa kiwango kikubwa sana. Ukiwa na simu si lazima uwe na akaunti ya benki hiyo hiyi simu yaweza kuwa sehemu ya kuhifadhi pesa zako. Makala hii ilijaribu kukupa jicho la ziada pia tujaribu kuwangalia faida hizo na hasara zake ukilenga dhana nzima ya  uwekezaji kwa pamoja.

No comments:

Post a Comment

Pages