HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 19, 2020

Masoko ya madini Singida yaingiza shilingi bilioni 3.2

Na Mwandishi Wetu

MASOKO ya madini mkoani Singida yameleta mapinduzi makubwa katika sekta hiyo kwa kuwezesha Serikali kukusanya zaidi ya Sh.Bilioni 3.2 sawa na asilimia 216 kwa kipindi cha mwaka 2019/2020.

Hayo yamebanishwa na Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mjiolojia Chone Malembo wakati akizungumza na  Kitengo cha Habari cha Tume ya Madini  ambao walitembelea mkoani hapo juzi.

Alisema kuanzishwa kwa masoko ya madini katika mkoa wa Singida kumeleta mapinduzi makubwa kwenye uchumi ikiwa ni pamoja na makusanyo ya shilingi bilioni 3.243 ambayo ni sawa na asilimia 216.2 kwa mwaka wa fedha 2019-2020 ambao haujamalizika.

Malembo alifafanua kuwa, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019-2020 ofisi yake ilipangiwa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.5 na kuongeza kuwa hadi kufikia katika kipindi cha mwezi Machi mwaka huu wamekusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.243 sawa na asilimia 216.2 na kufanikiwa kupewa cheti cha pongezi kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Tume  ya Madini .

Alisema siri ya makusanyo ni pamoja na usimamizi mzuri kwenye masoko mawili ya madini yaliyoanzishwa katika maeneo ya Shelui Wilayani Iramba na Manispaa ya Singida mkoani Singida.

"Ukusanyaji wa maduhuli kabla ya kuanzishwa masoko haya kati ya mwaka wa fedha 2018-2019, ofisi yangu ilipanga kukusanya shilingi bilioni moja na kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 804.5 ila sasa wamevuka lengo," alisema.

Malembo alisema ufanisi huo unatokana na ushirikiano aliokuwa akiupata kutoka katika vyombo vya ulinzi na usalama na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Aliongeza kuwa mafanikio hayo ni mazao ya uwepo wa uwazi, uwajibikaji na ushirikiano  thabiti wa Serikali kwa ujumla wake na kwa msaada mkubwa wa viongozi wa Wilaya na Halmashauri zote.

Aidha, alisema  uanzishaji Kikosi Kazi Madini (KKM) ambacho kina wajumbe kutoka taasisi muhimu ikiwemo baadhi ya taasisi zinazounda kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa ni sababu nyingine iliyochangia udhibiti utoroshaji madini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iramba Emmanuel  Luhahula alisema uanzishwaji masoko ya madini umechangia mapato katika halmashauri ya Iramba yaongezeka hadi shilingi milioni 99 tofauti na awali ambapo walikuwa wakipata shilingi 500,000 kwa mwaka.

Aliongeza kuwa, uanzishwaji wa masoko ya madini umepunguza kwa kiasi kikubwa cha utoroshaji wa madini kwa kuwa wachimbaji wa madini wamekuwa na mwamko mkubwa wa kuyatumia masoko ya madini yaliyoanzishwa  na kupata faida huku Serikali ikipata kodi mbalimbali.

Luhahula alitaja mafanikio mengine ya masoko ya madini yaliyoanzishwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mzunguko wa fedha katika wilaya ya Iramba  na kuwataka wachimbaji kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na kanuni za madini huku wakijikinga na ugonjwa wa korona.

"Mikakati ya wilaya yetu ni kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinaboreka lakini poa udhibiti wa maambukizi ya virusi vya corona hususan kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini yanadhibitiwa," alisema.

Lahahula alisema, ofisi yake kwa kushirikiana na ofisi ya Ofisa Madini Mkazi wa mkoa wa Singida wameanza kutoa elimu kwa wachimbaji wa madini na kuhakikisha wachimbaji wanaendesha shughuli zao kwa tahadhari ikiwa ni pamoja na kuwa na maji tiririka na vitakasa mikono.

Wachimbaji wa madini katika machimbo ya dhahabu ya Sekenke mbali na kuipongeza Serikali kwa kuwapatia maeneo ya uchimbaji wa madini na uanzishwaji wa masoko ya madini walisema kuwa masoko ya madini yameleta mapinduzi makubwa.

Akizungumza kwa niamba ya wachimbaji wa madini, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wachimbaji Wadogo wa Madini Kisonga na Shelui (UWAWAKISHE), Masumbuko Jumanne alisema kuwa kuanzishwa kwa masoko ya madini kumeleta manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kuuza madini yao kwa kufuata bei elekezi zinazotolewa na Serikali kila mwezi na kupata faida na  usalama kwenye biashara ya madini.

No comments:

Post a Comment

Pages