Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha Zimamoto kilichopo eneo la Fire, Ilala jijini Dar es salaam, Kenedy Komba (kulia) kuhusu vifaa mbalimbali vya zimamoto katika Maoneosho ya Pili ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Mei 18, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Na Jasmine Shamwepu, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuweka sera nzuri zinazotoa fursa kwa Vyuo vya ufundi na sekta binafsi ili kuhakikisha mafanikio yanapatikana.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Mei 28, 2021 wakati akifungua maonyesho ya pili ya elimu ya ufundi yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuweka sera nzuri zinazotoa fursa kwa Vyuo vya ufundi na sekta binafsi ili kuhakikisha mafanikio yanapatikana huku akiitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi ili kukuza ujuzi huo.
Vilevile, ameitaka sekta binafsi nchini inapokutana na changamoto yoyote kufika Serikali ili waweze kufanya kazi kama timu na kukabiliana changamoto hiyo ya ajira.
Waziri Mkuu ,ametoa wito kwa wadau wote kuendelea kushikamana, kuzungumza lugha moja kwa kuhakikisha mwelekeo huo unaeleweka kwa Watanzania.
Aidha, Majaliwa amesema Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya kuwekeza katika sekta ya elimu nchini na kwamba hadi kufikia mwaka 2021 idadi ya vyuo vilivyosajiliwa nchini na Nacte 430.
Amesema pia idadi ya wanafunzi waliojiunga na vyuo hivyo imeongezeka kutoka 117,478 mwaka 2015 hadi 172,312 mwaka 2020.
Amesema wanafunzi hao ni wa ngazi za astashahada na stashahada na kwamba ongezeko hilo limepanua wigo kwa wahitimu wa kidato cha nne kujiunga na masomo katika ngazi hizo.
“Ongezeko hili limetoa nafasi kwa vijana waliomaliza darasa la saba kujiunga na vyuo vya Veta na wale ambao hawakupata elimu kabisa kujiunga katika taasisi ambazo zinatoa elimu ya ufundi na ujuzi ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine,”amesema.
Katika hatua nyingine,Majiliwa ametaja mbinu zinazofanywa na Serikali katika kukabaliana na tatizo la ajira ni pamoja na kuweka msisitizo katika ujenzi wa viwanda nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa ametaja mbinu nyingine ni kutoa fursa kwa wajasiriamali kubuni vifaa mbalimbali na kuimarisha eneo la elimu hasa ya ufundi.
Amesema bado kuna changamoto kubwa na kwamba ukubwa huo ni wakufikia soko la ajira la kufikia idadi ya raslimali watu wenye ujuzi zaidi ya milioni 15.
Waziri Mkuu amesema suala la changamoto ya ajira si kwa Tanzania tu bali ni duniani kote lakini kila nchi inatafuta mbinu za kukabiliana na changamoto hiyo ambapo amedai moja kati ya mbinu muhimu ni kutoa fursa kwa wajasiriamali wabunifu kubuni vifaa mbalimbali na kwenda kuvionyesha kwa lengo la kutafutia masoko.
“Pia, kuweka msisitizio katika ujenzi wa uchumi wa nchi kupitia viwanda kwa kukaribisha wawekezaji nchini wa kujenga viwanda vyenye ukubwa tofauti.Serikali inaendelea kukaribisha wawekezaji wa viwanda nchini na kwamba Tanzania inafursa nzuri ya kuendesha viwanda pamoja na malighafi nyingi,”amesema.
Majaliwa amesema licha fursa ya viwanda, Tanzania ina uwepo wa ardhi nzuri unatoa fursa ya kupeleka vijana na watanzania kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kuajiriwa na pia kupata mbinu mpya za kujiajiri.
Amesema wanaimarisha katika eneo la elimu hasa kwenye vyuo vya ufundi ambapo nako pia kutatoa waajiriwa wengi sana
Kwa upande wake,Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema kupitia maonyesho hayo wadau wataweza kubadilishana mawazo ya nini kifanyike katika kuboresha utoaji wa elimu ya ufundi hapa nchini.
“Tutaweza kukuza mashirikiano katika kuhakikisha vijana wanapata sehemu za kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo.Serikali inatambua umuhimu wa elimu inayozingatia ujuzi na umahiri kwa vijana wetu katika kufanikisha mageuzi ya uchumi hapa nchini,”amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Uongozi wa Nacte, Profesa John Kandoro amesema Nacte itaendelea kwa juhudi kubwa kusimamia utoaji wa mafunzo na kuhakikisha elimu ya ufundi inatolewa kwa ubora unaotakiwa ili iweze kukidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani.
Amesema mitaala ya umahiri inayotolewa na vyuo vya elimu ya mafunzo ya ufundi inawawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo zaidi na sio nadharia.
“Tatizo kubwa linalovikabili vyuo vyetu ni ukosefu wa nafasi za mafunzo kwa vitendo.Ukosefu huo unasababishwa na ushiriki mdogo wa wadau katika utoaji wa mafunzo na kwamba inatoka na wadau kutotilia maanani ushiriki wao katika utoaji wa mafunzo,”amesema.
Amesema changamoto hiyo inatokana na baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu gharama za mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment