Mkuu wa Mkoa wa
Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akizungumza wakati wa kukagua mabomba ya
maji katika Mradi wa Iyula ambapo amemzuia Mkandarasi wa Mradi huo kutotoka
Mkoa wa Songwe Mpaka atakapo kamilisha vifaa na wataalamu wote muhimu kwa ajili
ya ukamilishaji wa Mradi huo.
Wajumbe wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama wakikagua mabomba ya maji katika Mradi wa Iyula ambapo Mkuu
wa Mkoa amemzuia Mkandarasi wa Mradi huo kutotoka Mkoa wa Songwe Mpaka atakapo
kamilisha vifaa na wataalamu wote muhimu kwa ajili ya ukamilishaji wa Mradi huo.
Na Mwandishi Wetu
Mkandarasi wa Mradi
wa maji wa Iyula uliopo Wilaya ya Mbozi amezuiwa kutoka Nje ya Mkoa wa Songwe
huku akiwekwa chini ya uangalizi wa jeshi la Polisi mpaka atakapo kamilisha
vifaa na wataalamu watakaomalizia Mradi huo.
Mkuu wa Mkoa wa
Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ametoa zuio hilo leo mara baada ya
kutembelea Mradi wa maji wa Iyula ambao ulitarajiwa kukamilika tangu mwaka 2017
huku ukiwa na thamani ya shilingi bilioni tano.
Brig. Jen. Mwangela
amesema mkandarasi huyo anatakiwa aweke vifaa vyote na wataalamu wote watakao
muwezesha kukamilisha ujenzi wa mradi huo ndipo ataruhusiwa kutoka nje ya Mkoa
wa Songwe.
Ameongeza kuwa mkandarasi
huyo aliweka masharti ya kupewa fedha nyingi ambapo tayari ameshapewa sehemu ya
fedha hizo lakini bado utendaji wake wa kazi umekuwa wa kusuasua huku wananchi
wakiendelea kupata adha ya kukosa maji.
Meneja wa Wakala wa
Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Songwe Mhandisi
Charles Pambe amesema mradi wa Maji wa Iyula una gharimu shilingi bilioni tano
na tayari Mkandarasi ameshapewa bilioni 2.2
Mhandisi Pambe
amesema kutokana na kusuasua kwa mkandarasi huyo RUWASA wana angalia uwezekano
wa kuujenga mradi huo wenyewe kwa kutumia Force
Account.
Naye Mkandarasi wa
Mradi wa maji wa Iyula kutoka STC Construction ya Dar es Salaam Alan Makame
amesema kusuasua kwa mradi huo ni kutokana na kucheleweshewa malipo pamoja na
RUWASA kutotembelea mradi huo.
Amesema ndani ya siku
tatu atakuwa ameanza kazi ya kuweka baadhi ya mabomba katika mradi huo na kuwa
baada ya wiki mbili atakuwa amekamilisha mradi huo.
No comments:
Post a Comment