Baadhi ya wanakikundi wa Kundi la
Simba Jamii Tanzania Enterprises (SJTE), mkoa wa Mbeya wakimkabidhi kiti
cha matairi, Mwanafunzi Mlemavu wa Shule ya Msingi Nzovwe, Lucy
Furaha. (Na Mpiga Picha Wetu).
Na Mwandishi Wetu
WANACHAMA na wapenzi ya
Klabu ya Simba nchini na nje ya nchi wameomba kusaidia makundi mbalimbali ya
kijamii ambayo yanakabiliwa na changamoto za kimaisha.
Ombi hilo limetolewa na
Kiongozi wa Msafara wa Wajumbe wa Kundi la WhatsApp la Simba Jamii Tanzania Enterprises
(SJTE), mkoa wa Mbeya Jacob Madeje wakati akikabidhi msaada wa kiti cha matairi
‘wheelchairs’ na mahitaji mengine muhimu kwa Mwanafunzi Mlemavu wa Shule ya
Msingi Nzovwe Lucy Furaha.
Alisema wamemkabidhi
Lucy kiti hicho ambacho kinathamani ya shilingi 500,000 na vitu vingine ili viweze
kumsaidia kwa ajili ya mahitaji yake ya kila siku.
Madeje alisema wana
Simba popote walipo wanajukumu la kusaidia makundi maalum wakiwemo walemavu ili
nao waweze kushiriki shughuli za uzalishaji kama raia wengine.
“Tunawahimiza wana
Simba wenzetu na jamii kwa ujumla kukumbuka kujitolea kwa jamii isiyojiweza ili
kupata baraka na kuondokana na mikosi,” alisema.
Alisema makundi ya
WhatsApp na matawi ya wana Simba yanapaswa kutumika kusaidia na hiyo itakuwa
wametekeleza maelekezo ya Mungu ambaye anasisitiza kusaidia wasiojiweza.
Kiongozi huyo wa msafara alisema SJTE ni kundi
la mashabiki na wanachama wa Simba ambalo limekuwa na muendelezo wa kutoa
misaada kwa Watanzania ambao wanachangamoto mbalimbali.
“Sisi SJTE, ni kundi la
wanachama na washabiki zaidi ya 200 ambao tumeamua kushirikiana kwa pamoja
kusaidiana wenyewe kwa wenyewe na kusaidia makundi mbalimbali yenye mahitaji,”
alisema.
“Kundi hilo hivi karibuni
lilikabidhi tanki moja ya lita 2,000 pamoja na Solar kwa Kituo cha Yatima cha
Ukhty Raya kilichopo Mindu Morogoro.
Pia limekabidhi mabati
kwa misikiti kadhaa na linaendelea kutoa misaada mingine mbalimbali kwa kila
jamii ikiwamo ugawaji wa ‘wheelchairs’ kwa watoto walemavu pahala popote hapa
nchini,” alisema.
Akizungumza baada ya
kupokea msaada huyo Lucy alisema anashukuru kundi hilo kwa kuwa limeweza
kumuondolea changamoto iliyokuwa inamkabili kwa muda mrefu.
“SJTE imefungua upya
maisha yangu, naamini nitaweza kushiriki masomo kwa nguvu zote naomba Mungu
awasaidie na kuwaongezea kipato zaidi waendelee kusaidia wengine,” alisema.
Mwalimu Mkuu wa Shule
ya Msingi Nzovwe, Emilia Ndimbo, Mwenyekiti Kamati ya Shule Happy Bakamba na Afisa Elimu Kata Angomwile
Mwanansyobe wamesema msaada uliotolewa kwa Lucy utaweza kubadilisha maisha
yake.
No comments:
Post a Comment