Mkuu wa Mkoa wa Songwe
Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akipanda mti katika chanzo cha maji cha Ilolo
Wilayani Mbozi katika maadhimisho ya Siku ya kitaifa ya Upandaji miti ambapo
kimkoa yamefanyika Wilayani Mbozi kwa viongozi na Baadhi ya wananchi kupanda
miti.
Songwe, Tanzania
Mkuu wa Mkoa wa Songwe
Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela, ametoa rai kwa wananchi wote kujenga mazoea ya
kupanda miti bila kusubiri maagizo au maelekezo kutoka serikalini ya kuwataka
kufanya hivyo.
Brig. Jen. Mwangela ametoa
rai hiyo mapema leo katika chanzo cha maji cha Ilolo Wilayani Mbozi wakati wa
maadhimisho ya siku ya kitaifa ya Upandaji Miti ambapo kwa Mkoa wa Songwe
maadhimisho hayo yamefanyika kwa viongozi mbalimbali kupanda miti.
Amesema wananchi wajenge
tabia ya kupanda miti kwa wingi kwakuwa miti ina faida nyingi na pia Mkoa wa
Songwe una ardhi nzuri ambayo inawezesha aina nyingi za miti kustawi.
Brig. Jen. Mwangela
ameongeza kuwa licha ya Mkoa wa Songwe kuwa na hali ya hewa nzuri, kipaumbele
kiwe ni kupanda miti kwa wingi kwakuwa isipo fanyika hivyo itafikia kipindi
mvua zinazo patikana hivi sasa hazitakuwepo.
Aidha ameziagiza
halmashauri za Wilaya kuhakikisha zinatunza vizuri vyanzo vya maji na mikakati
inawekwa ya kuhakikisha miti inayopandwa yote inakua vizuri ikiwa ni pamoja na
kutorusu mifugo kusambaa na kuharibu vyanzo vya maji.
Afisa Maliasili Halmashauri
ya Wilaya ya Mbozi Charles Ndimbo amesema kwa sasa wanaendelea kuwahamasisha
wananchi kujengea wigo katika maeneno yote waliyopanda miti na kuzuia mifugo
yao isizurure na kufanya uharibifu.
Ndimbo amesema Halmashauri
ya Wilaya ya Mbozi inasimamia misitu 70 huku Lengo likiwa ni kupanda miti milioni
mbili kwa Mwaka Lakini kwa mwaka 2018/2019 zaidi ya miti milioni 1.6 ilipandwa huku
iliyofanikiwa kukua ikiwa ni miti milioni 1.1.
Amesema kuna sababu
mbalimbali zinazopelekea miti inayopandwa kushindwa kukua ikiwa ni pamoja na
miti hiyo kupandwa katika maeneo yasiyo faa, kuliwa na wadudu, kuharibiwa na
mifugo, ukame pamoja na kuchomwa moto.
Nao baadhi ya wananchi
walioshiriki maadhimisho ya siku ya upandaji miti wameiomba serikali kuendelea
kuwachukulia hatua kali za kisheria wote wanao haribu miti.
Kaulimbiu ya kitaifa ya
maadhimisho ya Siku ya Upandaji miti kwa mwaka 2020 ni, “Tutunze Mazingira,
tukabiliane na Mabadiliko ya tabia Nchi”.
No comments:
Post a Comment