HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 28, 2020

COSTECH yatangaza ruzuku utafiti corona

NA SULEIMAN MSUYA
 

WATAFITI, washauri na waandishi wa habari nchini wametakiwa kuandika mandiko ya kuomba ruzuku ili waweze kufanya utafiti na kuandika taarifa kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19) unaosababishwa na
virusi vya corona.
 
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), Dk. Amos Nungu (pichani), wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kwa njia ya video.
 
Mkurugenzi huyo alisema ruzuku hiyo ambayo inahusu makundi matatu ni zaidi shilingi bilioni 10 za Kitanzania inayotolewa na wadau mbalimbali kupitia Taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Afrika Kusini (NRF).
 
Dk. Nungu alisema janga la COVID-19 limeathiri maeneo mengi nchini na duniani hivyo ni wakati muafaka kwa watafiti, washauri na waandishi wa habari nchini kujitokeza na kuomba fedha hizo ili kuja na majibu sahihi kuhusu ugonjwa huo.

“COSTECH inaratibu hapa nchini ruzuku hii ilitolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo kupitia NRF, rai yangu kwa wadau wote waliolengwa kuanza maandalizi ya kuleta maandiko yatakayostahimili ushindani. Maelekezo ya kina na fomu za maombi zinapatikana kupitia
https://www.nrf.ac.za/division/funding/covid-19-africa-rapid-grant-fund,
alisema.

Alisema uratibu huu ni sehemu ya majukumu ya tume ya kutafuta rasilimali fedha ili kuendeleza utafiti ambapo wadau hao wametoa dola za Marekani Milioni 4.75 ambazo ni zaidi ya Shilingi Bilioni 10 kwa nchi 15 za Afrika.

“Ruzuku hii inahusu nchi 15 zilizo ndani ya “Science Granting Councils Initiative” ambazo ni Botswana, Burkina Faso, Côte d’Ivoire, Ethiopia, Ghana, Kenya, Malawi, Namibia, Mozambique, Rwanda, Senegal, Tanzania, Uganda, Zambia, and Zimbabwe. Lengo la ruzuku ni kufanikisha
upatikanaji wa maarifa kuhusiana na huu ugonjwa ili kufanikisha uchunguzi, kinga na tiba,” alisema.

Mkurugenzi huyo aliwataja wadau ambao wamechangia ruzuku hiyo ni pamoja na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Kimataifa la Sweden (SIDA); Kituo cha Utafiti cha Maendeleo cha Kimataifa cha Canada (IDRC) na Idara ya Uingereza ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID).
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti COSTECH, Profesa Mohammed Sheikh alisema watafiti, washauri na waandishi wa habari wanapaswa kutumia fursa hiyo kuionesha dunia uwezo wao katika utafiti na taarifa. 

Prof. Sheikh alisema dhana ya ushirikiano ambayo walikubaliana katika mkutano wa wanasayansi na watafiti mwaka jana ndio wakati wake wa kuonekana kivitendo.
“Tunaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi fedha zipo kinachohitajika ni andiko ambalo limekidhi vigezo ili mtu au taasisi ipewe,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages