SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wananchi na wafanyabiashara wote nchini kutoa taarifa
zitakazosaidia kuwabaini wazalishaji wa bidhaa za umeme hususani nyaya, zisizo
na viwango ili waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa upimaji na ugezi wa Bidhaa kutoka TBS, Johanes Maganga, alipokuwa akizungumza
jijini Dar es Salaam kufuatia malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara juu ya uwepo wa baadhi ya viwanda hapa nchini vinavyozalisha nyaya
hizo zisizo na ubora na hivyo kutishia usalama wa wananchi pamoja na mali zao.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Maganga alisema milango ya
TBS ipo wazi wakati wote hivyo ni muda muafaka kwa wananchi, wafanyabiashara
kwenda na kutoa taarifa juu ya uwepo wa viwanda vinavyozalisha nyaya hizo ili
hatua ziweze kuchukuliwa dhidi yao
“Tunawakaribisha muda wote na kutoka mahali popote waje
hapa ofisini kwetu kutupa taarifa ya
watu hao ili tuweze kujiridhisha na
kisha tuchukue hatua kali dhidi yao kwa kuwa sheria ipo wazi kwa yeyote anayeikuka
taratibu zilizowekwa kisheria na mamlaka
husika” alisema Maganga.
Kwa mujibu Mkurugenzi wa upimaji na ugezi wa Bidhaa, TBS imekuwa na utaratibu wa kutoa
leseni za uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo za umeme kwa kuweka
utaratibu wa viwango vinavyotakiwa hivyo kama kuna kiwanda chochote kinazalisha
chini ya ubora hilo litakuwa ni kosa ambalo mhusika anapaswa kuwajibishwa jambo
alilotaka litolewe taarifa pale linapojitokeza.
Aidha Maganga alisema pamoja na malalamiko hayo kutolewa,
TBS haitakaa kimya na badala yake itaendelea na utaratibu wake wa kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara viwandani na kwenye maduka ili kuona kama viwango
stahiki vinafuatwa ikiwa ni utaratibu wa usimamizi wa sheria zilizopo.
Hivi karibuni kulijitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara
wa vifaa mbalimbali vya umeme jijini Dar
es Salaam wakidai juu ya uwepo wa biashara ya nyaya zisizo
na ubora zinazozalishwa na baadhi ya viwanda hapa nchini na kuiomba Serikali
kupitia Shirika la viwango Tanzania (TBS) kufanya msako viwandani na madukani
ili kuwabaini wahusika
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Kariakoo,
baadhi ya wafanyabiashara hao pamoja na wanunuzi wa bidhaa hizo wamedai
kumekuwepo na wimbi la uzalishaji wa bidhaa hizo hususani nyaya za umeme za
majumbani ‘wiring’ zisizo na viwango
unaohitajika.
Wafanyabiashara hayo waliojitambulisha kwa majina ya Rashid
Salum pamoja na Frank Mtonga waliopo eneo hilo, walisema kumekuwepo na bidhaa
hizo katika baadhi ya maduka ya kariakoo na hivyo kusababisha maduka yanayouza
bidhaa zenye viwango bora kukosa wateja kutokana na wananchi wengi kukimbia kwa
kigezo cha bei na kuzifuata nyaya zisizo na ubora kutokana na unafuu wa bei
bila kujua athari zake.
“Kuna maduka mengi hasa maeneo ya mitaa ya Narungombe na
maeneo mengine yanye maduka yanayouza bidhaa hiyo, wanauza nyaya ambazo hata
ukizitamaza kwa macho utabaini kuwa hazina ubora, kigezo kikubwa kinachofanya wananchi
wazikimbile ni unafuu wa bei” alisema Salum
Kwa upande wake Mtonga alisema yeye kama mfanyabiashara
aliwahi kupokea lawama kutoka kwa baadhi ya wateja wake, waliomtuhumu kuwauzia
nyaya zisizo na ubora, suala alilodai kuwa hakulifahamu kwa kuwa hakuwa na
uelewa wa kutosha juu ya nyaya hizo na viwango vyake.
Akitolea mfano katika suala hilo, Mtonga alisema kwa nyaya
zenye ubora wa viwango ambazo zinauzwa kwa wastani wa Sh 100,000, huuzwa kwa
wastani wa hadi 70,000 kwa nyaya zisizokuwa na ubora wa viwango na hivyo
kuathiri ushindani wa bei katika sokoo huku pia zikileta madhara kwa wananchi
yakiwemo ya nyumba kuungua.
No comments:
Post a Comment