Serikali
ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki inatambua changamoto zinazojitokeza katika mipaka mbalimbali
ya Tanzania wakati wa usafirishaji wa bidhaa hususani katika kipindi
hiki cha janga la COVID-19 na kuwa changamoto hizo zinatafutiwa ufumbuzi
kwa njia ya majadiliano katika maeneo husika.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Balozi Kanali Wilbert Ibuge ameyasema hayo alipokutana na kufanya
mazungumzo na Balozi wa Tanzania Nchini Zambia Mhe. Benson Keith Chali
ili kuangalia namna ya kutatua changamoto mbalimbali za usafirishaji wa
bidhaa hususani zile zinazotoka katika bandari ya Dar es Salaam kuelekea
katika nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC.
Ameongeza
kuwa katika kipindi hiki cha janga la COVID – 19 unaosababishwa na
virusi vya Corona changamoto mbalimbali zimejitokeza katika utoaji wa
huduma za usafirishaji wa huduma na bidhaa mbalimbali na hivyo serikali
inafanya jitihada za majadiliano na baadhi ya nchi katika mipaka ili
kutatua changamoto zinazojitkeza na kuwezesha huduma ya usafirishaji
kuendelea bila ya vikwazo.
Nae
Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Mhe. Chali amemuahidi Balozi Kanali
Ibuge kuwa Serikali ya Zambia imeshaanza kuzifanyia kazi changamoto
zinazojitokeza. "Suala hili limesaanza kufanyiwa kazi na kila kitu
kitakuwa sawa," amesema Balozi, Chali.
Katika
tukio jingine Balozi Kanali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya
mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi ambapo katika mazungumzo hayo
wameongelea zaidi namna ya kushirikiana na kuwezesha kujenga uwezo wa
kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa wawekezaji wadogo na wakati wa Tanzania
na kuwa na ubia na wawekezaji wakubwa hususani katika kipindi hiki cha
COVID – 19 na baada ya COVID – 19 ili kuunusuru uchumi wa Taifa
kuanguka.
"Tumekubaliana
kuongea ushirikiano katika sekta za afya, maji, maendeleo na uwekezaji
…….kwa hili tunawashukuru sana UNDP kwa kazi wanayoifanya lakini pia
hata katika ushirikiano wa kisera tumekuwa tukishirikiana nao jambo
ambalo linazidi kuimarisha uhusiano wetu hasa katika wakati huu wa COVID
- 19 kwani jambo hili linasaidia kunusuru uchumi wa taifa kuanguka,"
amesema Balozi, Kanali Ibuge.
Katika
hatua nyingine, Balozi Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo kwa
nyakati tofauti na Balozi wa Uingereza nchini Bi. Sarah Cooke pamoja na
Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania Bw.
Zlatan Milišić ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano
hususani katika kipindi hiki cha janga la COVID – 19.
Tarehe
6 Aprili, 2020 ulifanyika Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo pamoja na mambo
mengine, mkutano huo ulijadili janga la COVID-19 unaosababishwa na
virusi vya Corona. Mkutano huo ulihusisha Mawaziri wenye dhamana ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha,Viwanda,Biashara,
Utalii, Mambo ya Ndani na Uchukuzi, kutoka nchi 16 wanachama wa SADC.
Katika
mkutano huo, Baraza la Mawaziri lilitoa mwongozo kuhusu Usafirishaji wa
Bidhaa Muhimu na Huduma katika Nchi za SADC katika kipindi hiki cha
janga la Virusi vya Corona. Mwongozo huu unatumika katika kipindi hiki
unalenga kupunguza safari zisizo za lazima na kuwezesa usafirishaji wa
bidhaa muhimu wakati huu wa janga la COVID - 19.
No comments:
Post a Comment