Na Mbaraka Kambona
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
(THBUB) amesema uamuzi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe
Magufuli wa kuwasamehe wafungwa 3973 ni hatua muhimu katika kudhibiti kusambaa
kwa maambukizi ya maradhi yanayosababishwa na Virusi vya Korona.
Jaji Mwaimu aliyasema hayo leo Mei 7, 2020 Ofisini
kwake jijini Dodoma alipokuwa akitoa mtazamo wake juu ya jitihada za Serikali
za kudhibiti kuenea kwa maradhi hatari ya Korona.
Alieleza kuwa msamaha huo ni muhimu hasa katika
nyakati hizi ambapo Tanzania na nchi nyingine Dunia zipo katika kupambana na
vita kubwa ya mlipuko wa maradhi yanayosababishwa na virusi vya Korona.
Jaji Mwaimu aliendelea kusema kuwa msamaha huo
utasaidia sana kupunguza msongamano kwa wafungwa na mahabusu unaoweza
kuhatarisha afya zao. “Kimsingi msamaha huu wa Rais utasaidia kulinda haki ya
afya kwa wananchi. Sisi Tume tunaona uamuzi huu wa Rais Magufuli umebebwa na
nia njema ya kutaka kuwalinda wananchi anaowaongoza”, alisema Jaji Mwaimu
Aliendelea kusema kuwa Serikali inaweza kuendelea
kupunguza misongamano kwa kutumia mifumo mbalimbali ya Sheria iliyopo kwa kutoa
adhabu mbadala ikiwemo matumizi ya Sheria ya Parole ambayo inaruhusu vifungo
vya nje kwa wale wafungwa wenye tabia njema.
Katika hatua nyingine, Jaji Mwaimu aliwashauri baadhi
ya askari Polisi ambao wamekuwa wanalalamikiwa kuwa na tabia ya kubambikiza
kesi wananchi kuacha kufanya hivyo kwani ni moja ya chanzo cha
misongamano isiyo ya lazima magerezani.
Aidha, Jaji Mwaimu alimpongeza Mkurugenzi wa Mashtaka
kwa ziara zake za hivi karibuni magerezani ambapo lengo lake ni kupunguza
misongamano magerezani kwa kufuta kesi za Mahabusu baada ya kuona baadhi yao
kesi zao hazina msingi wala ushahidi wa kutosha.
Hata hivyo alimuomba DPP aendelee na jitihada hizo ili
kupunguza
misongamano magerezani.
Pia Mwenyekiti anaona kuwa Mahakama ina mchango katika
kupunguza misongamano magerezani kwa kutoa dhamana kwa makosa yanayodhaminika kwa
masharti nafuu.
Vile vile alisema kuwa ameliomba Jeshi la Polisi kwa
mamlaka iliyonayo kutoa dhamana kwa watuhumiwa waliopo katika vituo vyao ambao
wana makosa madogomadogo ambayo yanaweza kudhaminika ili kupunguza misongamano katika
mahabusu zao.
Aprili 26, 2020 kwenye Maadhimisho ya miaka 56 ya
Muungano, Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa 3,973
ambapo kati ya hao 256 walikuwa wanakabiliwa na adhabu ya kunyongwa na
wamebadilishiwa adhabu hiyo.
No comments:
Post a Comment