Mwenyekiti wa Baraza
la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mh. Kalolo Ntila
amemtahadharisha Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo juu ya kusuasua kwake
kuwachukulia hatua watumishi ikiwemo watendaji wa vijiji wanaokwamisha
utekelezaji wa maazimio na mipango mbalimbali ya halmashauri hali inayopelekea kukwamisha
maendeleo ya wananchi.
Mwenyekiti huyo
amesema kuwa baraza hilo limekuwa likimuagiza Mkurugenzi ambaye ndiye katinbu
wa vikao vya baraza kutekeleza maazimio kadhaa ikiwemo kuwawajibisha watumishi
wasio waadilifu hasa katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri lakini mrejesho
wa maazimio hayo umekuwa sio wa kuridhisha, jambo ambalo madiwani hao
hawaridhiki nalo.
“Na sisi tunampenda
sana ndugu yetu Mkurugenzi, lakini kama anaweza kawaacha wadogo zake
wakamfikisha pahali pa hovyo, pia anahatarisha kibarua chake, kumbe wakati
mwingine ukimuona mdogo anafanya vya hovyo ni vizuri kuchukua hatua ili ugali
wako pia uendelee kuwepo, kwasababu mwisho wa siku sisi hatuji kumtafuta
mtumishi mmoja mmoja, Tunaempa maelekezo haya ni Mkurugenzi Mtendaji, na yeye
anajua akina nani wanafanya hivyo,lakini kama anaweza akatuletea kwamba hawa
sisi wanatukwamisha, sisi tuna meno, hawa ni maji maramoja tu ” Alisisitiza.
Awali wakati akichangia
hoja hiyo Diwani wa kata ya Kaengesa Mh. Godfrey Kauzeni alisema kuwa kwa muda
mrefu baraza hilo limekuwa likitoa maazimio lakini hakuna utekelezaji hali
inayopelekea kila siku kutoa maazimio hayo kwa hayo ilihali madiwani wenyewe
ndio wasimamizi na kuongeza kuwa huenda wao kama wasimamizi wanachelewa
kuchukua hatua.
“Mheshimiwa
Mwenyekiti kwa umakini wako wewe mwenyewe, kama tukisimama vizuri katika
kusimamia hizi hoja, zikajibiwa kwa wakati na pale ambapo kunaonekana kuna
kuchelewa, wapo wanaochelewesha, kwanini tunawaacha tusichukue hatua, pengine
na sisi chombo hiki tumekuwa wapole sana, pengine Mkurugenzi alishajua namna
tulivyo, kwahiyo naacha tu bora liende tu, kwasababu anajua hakuna ‘action’
zozote zitakazochukuliwa,” Alisema.
Hayo yamesemwa katika
kikao maalum cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kilichohusu
utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali nchini.
Akizungumza kabla ya
kufungwa kwa baraza hilo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amelisisitiza
baraza hilo kuwa na uwezo wa “kung’ata” pale inapobidi baada ya kuona
utekelezaji wa maazimio hayajatekelezwa kama mlivyokubaliana na kuongeza kuwa
kuazimia ni jambo moja lakini ufuatiliajia wa maazimio hayo ni jambo jingine
ambalo linapaswa kufanyika.
“Kwahiyo nikazie tu
kwamba, lazima baraza ling’ate, baraza lisimamie maazimio yake kuhakikisha
kwamba yametekelezwa tena kikamilifu, kwasababu mlipokaa na kutoa maazimio
mlikuwa mko ‘serious’ sasa hiyo ‘seriousness’ lazima iwepo pia kwenye
kutekeleza yale maazimio ambayo sasa ni kazi ya Mkurugenzi, sasa ni lazima
muudhibiti upande huu wa Menejimenti, ni jukumu la kwenu hilo la kiusimamizi,”
Alieleza.
Kwa mujibu wa taarifa
za mfumo wa ukusanyaji wa mapato, hadi tarehe 23 Aprili, 2020 makusanyo
yatokanayo na mashine za Point Of Sales (POS) ambayo hayajapelekwa benki ni
shilingi 509,033,302/= huku waheshuimiwa madiwani wakiidai halmashauri hiyo
shilingi 175,000,000/= ambayo wanatakiwa kulipwa kabla ya tarehe 30.5.2020.
No comments:
Post a Comment