HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 22, 2020

WAHITIMU WA VYUO VYA ELIMU YA JUU 3,200 WANUFAIKA NA MAFUNZO YA VITENDO SEHEMU ZA KAZI

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Richard Kasesela akitoa taarifa kuhusu Mafunzo ya Vitendo sehemu za Kazi “Internship Training” kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (kulia) alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua mafunzo wanayopatiwa vijana hao na waajiri katika mkoa huo. 
Sehemu ya Vijana wanufaika wa Mafunzo ya Vitendo sehemu za Kazi “Internship Training” wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani).  
 


 Na Mwandishi Wetu, Iringa


Vijana wahitimu wa Vyuo vya elimu ya juu zaidi ya 3,200 nchini wamenufaika na Mafunzo ya vitendo mahala pa kazi “Internship Training” yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira ambapo zamani ilikuwa ni Wakala wa Huduma za Ajira (TAESA).

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa katika ziara Mkoani Iringa kutembelea waajiri wenye vijana wanaowapatia mafunzo katika sehemu zao za kazi yaani “Interns”.

Waziri Mhagama alieleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa yakihusisha vijana waliohitimu ngazi mbalimbali za elimu ambapo wanapatiwa fursa ya kujifunza kwa vitendo katika maeneo ya kazi kwa lengo la kuwapatia uzoefu wa kazi utakaowasaidia kuajiriwa au kujiajiri.

“Kuanzishwa kwa mafunzo hayo ilikuwa ni moja kati ya maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba vijana hususani kwenye masuala ya ajira nchini, hivyo vijana waliomaliza kozi mbalimbali kupatiwa ujuzi katika maeneo ya kazi ili waweze kuwa na uzoefu pale wanapojiajiri ama kuajiriwa,” alisema Mhagama

Aliongeza kuwa Mpango huu wa mafunzo ya vitendo mahala pa kazi umekuwa na mchango mkubwa na ni chachu katika kuwezesha nguvukazi ya taifa hususan vijana waliohitimu kwa kuwajengea uzoefu, weledi na maadili ya kazi yanayohitajika pindi wanapoajiriwa.

“Tunataka kuona vijana wanapomaliza mafunzo haya wanakuwa na dhana ya kuchangamkia fursa mbalimbali ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu hii ya tano kwa kuwa tayari mnauzoefu,” alisema Mhagama

“Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kufanya tathmini ya mafunzo haya na mafunzo mengine yanayotolewa chini ya Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ili kuona namna ujuzi wanaopatiwa vijana nchini unakuwa wa manufaa katika kuwezesha vijana wanakuwa sehemu ya kufikisha taifa lao katika uchumi wa kati,” alieleza Mhagama

Aidha Waziri Mhagama alitoa wito kwa vijana ambao wamenufaika na mafunzo hayo kufanya kazi kwa bidi, weledi na maarifa kwa kuonyesha umahiri wa kujenga uchumi wa taifa.

Sambamba na hayo, alitoa pongezi kwa waajiri wote nchi katika sekta ya Umma na Binafsi kwa namna walivyoshirikiana na Serikali katika kuwapatia vijana mafunzo hayo kwa muda wa miezi sita hadi mwaka mmoja na wamekuwa sehemu ya mafanikio katika kuziwezesha taasisi kufikia malengo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Richard Kasesela alieleza kuwa Programu hiyo ya mafunzo kwa Vitendo sehemu za Kazi imekuwa na manufaa makubwa kwa vijana na ameiomba Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha ujao kutenga bajeti zaidi kwa ajili ya kuwezesha vijana wanaohitimu kwenye vyuo mbalimbali nchini ili waweze kunufaika na mafunzo hayo.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa GIBRL Business Solutions Ltd, Bi. Hadija Jabir alisema kuwa uwepo wa vijana wanaopatiwa mafunzo hayo katika kampuni yake umekuwa na tija.

“Kama mwajiri nimeona ufanisi wa vijana hao, naiomba serikali iwapatie nafasi zaidi ya vijana hao wanaohitimu kufanya mafunzo katika sehemu za kazi ili yale waliyojifunza kwa nadharia waweze kuyatekeleza kwa Vitendo,” alisema Jabir

Naye, Mmoja wa Wanufaika wa Mafunzo hayo, Bi. Felister Gerald ameishukuru serikali kwa kutambua mchango wa vijana na kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewasaidia kuwajengea uzoefu na ujasiri wa kufanya kazi.

No comments:

Post a Comment

Pages