Mkurugenzi wa Kiwanda
cha kualisha Unga wa Sembe wenye virutubishi wa AMP Sembe, Alfred Mpanga
akizungumza na na wanahabari kuhusu changamoto wanazokumbana nazo
kutokana na kushuka kwa uzalishaji. (Picha na Denis Mlowe).
Na Denis Mlowe, Iringa
WAMILIKI wa viwanda vya kuzalisha unga wa sembena
wafanyabiashara wa chakula ‘mama lishe’ mkoani Iringa wamelalamika kuporomoka
kwa uzalishaji na wateja kutokana na
janga la Corona linaloendelea duniani kote.
Wakizungumza na mwanahabari wamiliki hao wamesema kwamba
hali ya sasa ya uzalishaji imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na biashara
hiyo kuathiriwa na kuenea kwa virus vya corona nchini.
Mmoja wa wa wamiliki hao, Alfred Mpanga Mkurugenzi wa
kiwanda cha kuzalisha unga wa Sembe wa AMP Sembe alisema kuwa kwa sasa uzalishaji umepungua
kwa kiasi kikubwa kuytokana na janga la virusi vya Corona hali ambayo
imewaathiri kwa kiasi kikubwa katika biashara.
Alisema kuwa awali walikuwa wanazalisha zaidi ya tani 6
hadi 8 kwa siku tofauti na sasa ambapo wanazalisha tani mbili kwa siku hii yote
kutokana na kupungua kwa wateja ambao walikuwa wanawategemea nje ya mkoa wa
Iringa.
Mpanga alisema kuwa hali hiyo imewafanya kukabiliana na
hali ngumu ya maisha kwani uchumi wao kwa ujumla umepungua na kuwa katika
hatari ya kupoteza hata mtaji kwani biashata hakuna na taasisi za kifedha
zinawadai.
Alisema kuwa kutokana na kupungua kwa uzalishaji
amelazimika kuponguza idadi ya wafanyakazi katika kiwanda hicho ili kuendana na
hali ya soko kwani wakati mwingine wamekuwa wakifunga kabisa ofisi kutokana na
gharama kubwa za uendeshaji kuliko kipato wanachopata.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kiwanda kinachozalisha
unga wa sembe cha Ihemi, Dickens Lulandala alisema kwa kuwa kufungwa kwa shule
za sekondari na msingi ambazo zilikuwa zinanunua unga kwenye kiwanda hicho
kimewaathiri kwa kiasi kikubwa na hii kutokana na kuenea kwa virusi vya corona.
Lundala alitoa wito kwa serikali na taasisi za Fedha
kurekebisha mifumo ya Ulipaji wa Madeni yao kutokana na kuporomoka kwa Biashara
ya chakula na kushindwa kumudu gharama za maisha.
Kwa upande wao mamalishe ambao wanafanya shughuli zao
katika eneo la Igumbilo, Devotha Salim, Getruda Mwipoki walisema kuwa kwa sasa
biashara ya chakula imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana wateja wao wengi
kujifungia nyumbani hali ambayo wanapika kilo mbili za chakula lakini bado
zinabaki.
Walisema kuwa hali hii ikiendelea basi maisha yatakuwa
magumu zaidi kwani wanategemea biashara kuendesha maisha yao na kulipa mikopo
wanayodaiwa kwenye taasisi za kifedha hivyo kuporomoka kwa Biashara za Chakula
na Nafaka kunatajwa kuwa na athari zinazowafanya washindwe kuendesha maisha yao
ikiwa ni pamoja na Ulipaji wa Kodi ya serikali.
No comments:
Post a Comment