HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 14, 2020

Haki Fursa Yafurahia Bajeti

Safu ya viongozi wa Taasisi ya Haki Fursa wakiwa kwenye mazungumzo na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, kutoka kushoto ni Ofisa Ustawi wa Jamii, Lwitiko Mwakikuti, Katibu Mtendaji Ntimi Charles, Ofisa Mipango Kwagilwa Reuben na Ofisa Habari Haran Sanga.



Na Janeth Jovin

TAASISI ya Haki Fursa imeipongeza Serikali kwa kuandaa bajeti bora yenye kuwajali wananchi wa kada zote.

Kadhalika taasisi hiyo pia imelishukuru Bunge la Tanzania kwa Azimio la kumpongeza Rais John Magufuli kwa namna alivyolishughulikia janga la Corona bila kufunga mipaka ya nchi.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Taasisi hiyo Ntimi Charles alisema ni busara kuipongeza Serikali na Bunge kwa hatua wanazoendelea kuchukua bila kuathiri uchumi wa nchi.

Hivi karibuni Bunge lilipitisha bajeti ya Serikali ya Sh. Trilioni 34.88 kwa mwaka 2020/21 iliyozingatia vipaumbele mbalimbali ikiwemo kuondoa umaskini.

"Tumewaiteni hapa leo kuwashukuru kwa namna mlivyotusaidia kupaza sauti kwa watanzania ili tumpongeze Rais Magufuli kwa namna alivyoliongoza taifa dhidi ya vita ya corona na kuishinda vita hiyo kwa weledi.

"Tulizungumza nanyi tukimuomba Spika Job Ndugai hoja yetu ilisikika na tulimuandikia barua Rasmi tunamshukuru amesikia.

"Lakini pia tunaipongeza Serikali kwa bajeti bora iliyolenga kufanya miradi mikakati itakayoinua uchumi wa nchi.

"Hii ni bajeti bora ukilinganisha nchi nyingine za Afrika Mashariki ambao ndio wenzetu hasa tunaotakiwa kujipima nao," alisema Charles.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Haki Fursa, Lwitiko Mwakikuti, alisema ubora wa bajeti hiyo imetokana na ujasiri wa Rais Magufuli wa kuruhusu wananchi kufanyakazi na kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

"Ni ujasiri wa aina yake ndio maana uchumi wa nchi haujadorora kama wenzetu walioamua kujifungia... tulifanya kazi na tunaendelea ndio maana tunasisitizwa kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na wataalam wa afya na viongozi wa Serikali," alisisitiza Mwakikuti.

No comments:

Post a Comment

Pages