Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hati ya Shule ya Sekondri ya
Wasichana ya Bunge kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai (wa pili
kushoto) wakati alipoweka jiwe la msingi na kukabidhiwa shule hiyo
iliyopo Kikombo Dodoma, Juni 14, 2020. Shule hiyo imejengwa na wabunge
na kutolewa kwa Serikali. Wa pili kulia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais
TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga, na wa watatu kulia ni Mbunge wa
Urambo na Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania , Margaret
Sitta na kushoto ni Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua majengo ya Shule ya Sekondari ya
Wasichana Bunge iliyopo Kikombo Dodoma Juni 14, 2020. Kushoto ni Naibu
Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai (wa tatu
kulia) wakiweka jiwe la Msingi la Shule ya Sekondari ya Wachana ya
Bunge iliyojengwa na wabunge na kukabidhiwa kwa Serikali Juni 14, 2020.
Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo na wa
pili kulia ni Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson Mwansasu. Kushoto
ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako na
wapili kushoto ni Mbunge wa Urambo na Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge
Wanawake, Margaret Sitta. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipanda mti wakati alipoweka jiwe la
msingi la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge katika eneo la
Kikombo Dodoma, Juni 14, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiagana na Spika wa Bunge Job Ndugai
(kushoto) na Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (katikati)
baada ya kuweka jiwe la msingi la Shule ya Sekondari ya Wasicha ya
Bunge na kukabidhiwa shule hiyo iliyojengwa na Wabunge katika eneo la
Kikombo Dodoma, Juni 14, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Dodoma, Tanzania
Dodoma, Tanzania
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa watu wote watakaothibitika
kufanya vitendo vya kuwakatisha watoto wa kike ndoto za masomo ikiwemo
kuwafunga jela miaka 30.
Pia amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote
nchini wahakikishe wanaendelea kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama hadi
ngazi za kata kusimamia Sheria ya Elimu ya kuwalinda watoto wote wa kike walio chini
ya umri wa miaka 18.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumapili, Juni 14, 2020) wakati alipoweka
jiwe la msingi na kukabidhiwa shule ya sekondari ya wasichana ya Bunge High School
iliyojengwa na wabunge katika Kata ya Kikombo jijini Dodoma kwa thamani ya
zaidi ya sh. bilioni moja.
“Sekta ya elimu ni wakala wa mabadiliko katika
jamii kiuchumi, kiteknolojia na kiutamaduni katika kuleta maendeleo ya nchi.
Ninawapongeza sana waheshimiwa wabunge kwa kuamua kuwa sehemu ya wadau muhimu
katika sekta ya elimu .”
Amesema
utoaji wa elimu bora kwa Watanzania ni moja ya vipaumbele vya nchi katika
kuleta maendeleo na kufikia malengo ya Milenia 2025, Elimu kwa wote (EFA) na
Mkakati wa Kupambana na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA).
Waziri
Mkuu amesema ili kuweza kufanikisha hayo wanahitaji sekta hiyo iwe bora, imara,
inayokidhi mahitaji ya jamii kwa kuwapa vijana maarifa na ujuzi wa kukabiliana
na matatizo ya kijamii, kitaifa na kimataifa.
Amesema
Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali imepata mafanikio
makubwa sana kwa upatikanaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya na maji,
ambapo kwa sasa kuna shule za msingi 17,659 na shule za sekondari 4,883 nchi
nzima zikiwemo shule za sekondari za Serikali za wasichana 156.
”Idadi hii ya shule imesaidia kutoa
fursa kwa wanafunzi wengi kupata elimu nchini katika ngazi mbalimbali. Hivi sasa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya
Chama cha Mapinduzi tunatekeleza mpango wa elimu bila ada kwa kutoa shilingi bilioni
22.8 kila mwezi kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule
anapata fursa bila vikwazo.”
Amesema
Serikali, itaendelea kusimamia utekelezaji wa sera ya Elimumsingi Bila Ada kwa lengo
la kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu ya sekondari na stadi za kazi,
kuondoa vikwazo kwa watoto wa kike kupata elimu ya sekondari, kuimarisha
matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji pamoja na uratibu,
usimamizi na tathmini ya ubora wa elimu ya sekondari.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali
imeweka mikakati maalum ya kuwasaidia watoto wa kwa kuhakikisha wanapata elimu bora na kutokana na mikakati
hiyo idadi ya wanafunzi wa kike wanaosoma Elimu ya Juu imekuwa ikiongezeka
mwaka hadi mwaka katika ngazi mbalimbali.
Mfano idadi ya wanafunzi wa kike katika
Elimu ya Juu wameongezeka kutoka wanafunzi 49,959 kati ya wanafunzi 139,638
waliodahiliwa mwaka 2010/2011 hadi kufikia wanafunzi 90,159 kati ya wanafunzi
230,339 waliodahiliwa mwaka 2017/2018. “Niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea
kuwekeza kwa elimu ya mtoto wa kike.”
Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu isimamie kufungua madawati ya malalamiko
katika vyuo vikuu kuhusu unyanyasaji wa kijinsia. “Serikali itaendelea kuchukua
hatua kali kwa wahadhiri watakaobanika kujihusisha na unyanyasaji wa kijinsia katika vyuo chini ya
sheria ya Mahusiano ya kulazimisha.”
Wakati huo huo, Waziri
Mkuu ametoa wito kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) watumie shule hiyo kuwatambua wasichana
wenye vipaji hususan kwa tahasusi za
sayansi na kuwasaidia kuvikuza na kuviendeleza.
Amesema
kwa kufanya hivyo, watakuwa wakitoa motisha kwa wanafunzi hasa wa kike na
kuwatia moyo ili wayapende masomo ya sayansi na teknolojia na hatimaye kuongeza
idadi ya wataalamu wa kike. Shule hiyo ni ya mchepuo wa sayansi.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge Job Ndugai amesema
ujenzi wa shule hiyo ni alama kubwa iliyowekwa na wabunge wa bunge la 11 kwani
wamefanya jitihada kubwa katika kujitolea kuchangia fedha zilizowezesha ujenzi
wa shule hiyo.
“…Namshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha wabunge wa bunge la 11 kuweza kufanikisha ujenzi
wa shule ya Wasichana ya Bunge ambayo itakuwa ya kidato cha tano na sita kwa
mchepuo wa sayansi.”
Awali, Mwenyekiti wa Umoja wa Wapunge
Wanawake Tanzania (TWPG), Margaret Sitta alitumia fursa hiyo kumshukuru Spika
Ndugai kwa kuunga mkono juhudi za wabunge wanawake na hatimaye kufanikisha
ujenzi wa shule hiyo.
Pia,
alimshukuru na kumpongeza Spika Ndugai kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia
unaendelea kuwepo bungeni. Hata hivyo ameiomba Serikali iangalie namna ya
kuwawezesha wanawake wengi kuingia bungeni kwa kupitia majimbo kwani waliopo ni
asilimia tisa tu ya wabunge wote wa majimbo.
No comments:
Post a Comment