Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akizungumza na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi kwenye wilaya ya
Musoma mkoa wa Mara alipokuwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa
sekta ya ardhi. Wa pili kulia ni Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Mara Jeswald Majuva
na Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Mara Jerome Kiwia.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akishangaa utunzaji Nyaraka na Majalada ya Ardhi kwenye ofisi za Ardhi ya
Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoa wa Mara alipokuwa katika ziara ya kukagua
utendaji kazi wa sekta ya ardhi. (Picha na Wizara ya Ardhi).
Na Munir Shemweta, WANMM TARIME
Naibu Waziri wa Ardhi
nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameziagiza halmashauri nchini
kufanya operesheni maalum ya kupima na kumilikisha ardhi ili kuwawezesha
wananchi kuwa na hati miliki kwenye maeneo wanayoyamiliki.
Dkt Mabula alitoa
maagizo hayo jana kwa nyakati tofauti katika wilaya za Tarime na Musoma mkoani
Mara alipokutana na uongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi wa wilaya
hizo wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na miradi
inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoani humo.
Alisema, ni lazima
halmashauri zifanye opresheni maalum ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi ili
kuwawezesha wananchi kuwa na hati miliki zitakazowawezesha kuzitumia kwenye
sughuli za kimaendeleo na wakati huo kuiwezesha serikali kukusanya mapato
kupitia kodi ya pango la ardhi.
Kwa mujibu wa Naibu
Waziri Mabula, pamoja na wizara ya Ardhi katika Bajeti yake ijayo ya 2020/2021 kuwa na
mpango wa kupima kila kipande cha ardhi kupitia miradi ya Benki ya Dunia na Benki
ya Exim-Korea lakini halmashauri zina wajibu kuhakikisha ardhi inapimwa na
kumilikishwa.
Alizitaka halmashauri za
wilaya na zile za miji kutenga bajeti kwa ajili ya kazi ya kupanga na kupima
maeneo na kusisitiza kuwa, zoezi hilo lisiishie katika upimaji pekee bali
lifikie hatua ya umilikishaji ardhi kwa kuwapatia wananchi hati.
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, vifaa kwa ajili ya kazi za upimaji vipo kwenye
baadhi ya Ofisi za Ardhi za Mikoa na kuongeza kuwa kinachotakiwa ni halmashauri
kuwasiliana na ofisi hizo ili kuvitumia kwenye kazi ya upimaji.
Alisema, kwa halmashauri
zenye wataalam wachache wa sekta ya ardhi zinaweza kuazima wataalam kutoka maeneo mengine ikiwemo Ofisi za Ardhi
za Mikoa na kubainisha kuwa kinachotakiwa ni wakurugenzi kutenga pesa ya
kujikimu kwa wataalam watakaofanya kazi ya upimaji.
‘’Mnaweza kuazima
wataalam kutoka maeneo mengine kama ile vofisi za ardhi za mikoa na cha msingi hapa
ni kwa Mkurugenzi kutenga fedha za kuwalipa wataalam watakaoenda kufanya kazi’’
alisema Dkt Mabula.
Akigeukia suala la
migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali, Dkt Mabula amezitaka halmashauri
kushirikiana na ofisi za ardhi za mikoa zilizoanzishwa hivi karibuni ili kuatua
migogoro ya ardhi kwenye maenro yao na kubainisha kuwa ofisi za ardhi za mikoa
zisipotumika ipasavyo basi itakuwa haina maana kuanzisha ofisi za ardhi za
mikoa.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Tarime Mhandisi Mtemi Msafiri aliipongeza Wizara ya Ardhi kwa hatua
inazochukua katika kushughulikia migogoro ya ardhi nchini ambapo aliiomba ofisi ya
Kamishna wa Ardhi mkoa wa Mara kuyachukua matatizo ya ardhi ya wilaya yake na
kuyafanyia kazi ili kuleta suluhu miongoni mwa wananchi wenye migogoro.
No comments:
Post a Comment