Katibu Mkuu
Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo (kushoto) akizungumza na wananchi wa vijiji
vya Kyaka, Lubale na Katuntu Wilayani Missenyi (hawapo pichani) wakati wa
kukabidhi kwa Mkandarasi eneo la mradi wa Maji wa Kyaka Bunazi. Kulia ni Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi na Diwani wa Kata ya Kyaka, Projestus
Tegamaisho.
Katibu Mkuu
Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo (mbele katikati) alipowasili katika Kijiji
cha Kyaka kwenye eneo litalojengwa chanzo cha Maji cha Mradi wa Kyaka Bunazi
wakati wa hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo
Katibu Mkuu
Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo (katikati) akielekea kwenye eneo
litalojengwa chanzo cha mradi wa Maji Kyaka Bunazi wakati wa uzinduzi wa ujenzi
wa mradi huo
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele
ambaye ni msimamizi wa utekelezaji wa mradi wa Maji wa kyaka Bunazi kwa niaba
ya Wizara ya Maji akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wake kwa Katibu Mkuu
Wizara ya Maji, Prof. kitila Mkumbo (hayupo pichani)
Katibu Mkuu
Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo (katikati) akiwasili katika Kijiji cha
Kyaka wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa maji wa Kyaka Bunazi. Kutoka
kushoto Kaimu Mkurugenzi MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele na Meneja wa
RUWASA Mkoa wa Kagera, Mhandisi Warioba Sanya.
Mkurugenzi,
Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Nadhifa Kemikimba
(aliyesimama) akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kyaka, Lubale na Katuntu
Wilayani Missenyi (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa
maji wa Kyaka Bunazi.
Na Mohamed Saif-
Kagera
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo amezindua na
kukabidhi rasmi ujenzi wa mradi wa kwanza nchini utakaotumia maji kutoka Mto
Kagera maarufu kama Mradi wa Maji wa Kyaka Bunazi utakaogharimu kiasi cha
Shilingi Bilioni 15.1.
Uzinduzi kwa ajili ya kuanza kwa utekelezwaji wa ujenzi wa
mradi umefanyika Juni 1, 2020 Wilayani Missenyi Mkoani Kagera na kushuhudiwa na
wananchi kutoka vijiji mbalimbali wilayani humo ambapo Mkandarasi Kampuni ya
China Civil Engineering and Construction Corporation (CCECC) alikabidhiwa rasmi
eneo la mradi kwa ajili ya kuanza mara moja utekelezaji wake.
Profesa Mkumbo alipongeza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya kutumia Mto Kagera
kuwapatia wananchi maji safi na salama na huku akibainisha kwamba mradi wa Maji
wa Kyaka Bunazi ni wa kwanza nchini utakaotumia Mto Kagera kama chanzo
chake cha maji kwa wanachi wanaouzunguka.
“Mradi huu ni wa kwanza kutumia maji ya Mto Kagera
kupelekea huduma ya maji kwa wananchi, kwani hatukuwahi kuwa na mradi wa namna
hii ila kwa Awamu hii ya Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli hili
limewezekana,” alibainisha Profesa Mkumbo.
Akielezea namna ambavyo mradi huo ulivyopatikana, Profesa Mkumbo
alisema ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa
Julai 11, 2019 la kuhakikisha wananchi wa Mji wa Kyaka wanapata huduma ya
majisafi kutoka Mto Kagera baada ya kujionea kero ya maji waliyokuwa
nayo.
“Rais Dkt. Magufuli alimuelekeza Waziri wetu wa Maji, Profesa
Makame Mbarawa kuhakikisha anafika hapa ili kuhakikisha tatizo la Maji
linatatuliwa haraka na kesho yake Waziri alifika na alituelekeza sisi wasaidizi
wake tuanze utekelezaji wa mradi mara moja,” alisema Profesa Mkumbo.
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, utekelezaji wa mradi huo
umegawanyika katika sehemu mbili ambapo moja itatekelezwa na Kampuni ya CCECC
kwa gharama ya shilingi bilioni 9.4 na nyingine itatekelezwa na wataalam wa ndani
kwa gharama ya shilingi bilioni 5.7.
Alifafanua kuwa utaratibu wa kutekeleza baadhi ya miradi kwa
kutumia wataalam wa ndani ulianzishwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa
na umeonyesha mafanikio makubwa kwani umewezesha kupatikana kwa miradi mizuri
na kwa gharama nafuu ikilinganishwa na utumiaji wa wakandarasi.
“Mheshimiwa Waziri alianzisha mfumo huu unaitwa force account
kabla ya hapo ilikua hata shughuli ndogo anatafutwa mkandarasi lakini sasa
shughuli nyingi za kawaida zinatekelezwa na wataalam wetu wa ndani na
imetusaidia kuokoa fedha nyingi,” alisema Profesa Mkumbo.
Aidha, alibainisha kuwa mradi unatekelezwa kwa fedha za ndani na
kwamba tayari fedha zimetengwa ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati huku
akiweka wazi kwamba shilingi milioni 650 ilikwishatolewa kwa ajili ya
utekelezaji wake.
Profesa Mkumbo alielekeza mradi ukamilike kwa wakati kwani
hakuna kikwazo cha fedha kwenye utekelezaji wake na pia wahakikishe shughuli
zinazoweza kufanywa na wananchi wa maeneo ya mradi zifanywe na wananchi
hao.
“Sisi kama Wizara tumejipanga; fedha ipo Mkandarasi hata akileta
kesho maombi yake ya awali analipwa, hakuna kikwazo cha fedha kwenye kutekeleza
mradi huu,” alisisitiza.
Akizungumzia hali ya utekelezaji wa miradi ya maji kote nchini,
Profesa Mkumbo alibainisha kwamba Mradi wa Maji wa Kyaka Bunazi unakuwa ni
mradi wa 1,425 miongoni mwa miradi inayotekelezwa kwenye Serikali ya Awamu ya
Tano.
Aliongeza kuwa hadi hivi sasa miradi 792 imekamilika na kwamba
miradi 633 inaendelea kutekelezwa huku miradi 41 ikitekelezwa kwa fedha za nje
na mingine yote iliyobakia ikiwa inatekelezwa kwa fedha za ndani.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi
Leonard Msenyele ambaye ndiyo msimamizi wa utekelezaji wa mradi kwa niaba ya
Wizara ya Maji alisema sehemu itakayotekelezwa na Mkandarasi CCECC itahusisha
ujenzi wa chanzo cha maji, ujenzi wa kituo cha tiba ya maji, ulazaji wa bomba
kuu la kusafirisha maji kutoka kwenye chanzo hadi kwenye kituo cha tiba ya maji
lenye urefu wa kilomita 1.5 na ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji yaliyotibiwa
la lita milioni mbili.
Aliongeza kuwa sehemu ya pili ya mradi itahusisha ulazaji wa
bomba kuu la usambazaji kutoka kwenye tenki lenye urefu wa kilomita 14 na
ulazaji wa mtandao wa bomba za kusambaza maji kwa wananchi ambayo itatekelezwa
na wataalam wa ndani kutoka Wizara ya Maji, Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA),
Mamlaka ya Maji Bukoba (BUWASA) na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA).
Mhandisi Msenyele alisema mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni
mwa Mwezi Julai, 2021 na kwamba kukamilika kwake kutawezesha upatikanaji wa
maji kwa wakazi wa Kyaka, Bunazi pamoja na maeneo jirani kwa asilimia mia moja
na hivyo kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji inayowakabili
wananchi wa maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment