*Ni utekelezaji wa uamuzi wa Rais Dkt. John Magufuli
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameikabidhi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
nyumba 103 zenye gharama ya zaidi ya sh. bilioni tano kwa ajili ya
makazi ya Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nchini zilizojengwa na
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Iyumbu jijini Dodoma
ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi ulitolewa na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli.
Baada
ya kukabidhi nyumba hizo, Waziri Mkuu amesema kwamba makazi hayo yawe
chachu kwa Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nchini katika
kutambua wajibu wao wa kutoa huduma iliyobora na inayokidhi matarajio ya wateja ambao ndiyo waajiri wao.
Akikabidhi
nyumba hizo leo (Jumanne, Juni 2, 2020), Waziri Mkuu amesema “Uamuzi
huu wa Mheshimiwa Rais ambao leo hii tunashuhudia utekelezaji wake
kupitia makabidhiano haya, utasaidia kuwafanya Maafisa na Askari wa
Uhamiaji kukaa katika makazi yao tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo
waliishi uraiani.”
Ameongeza
kuwa “Ni ukweli usiofichika kuwa makabidhiano ya nyumba hizi baina ya
Shirika la Nyumba la Taifa na Idara ya Uhamiaji ni moja kati ya
vielelezo vya utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe
Magufuli ya kuwapatia Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nyumba
103.”
Pia,
Waziri Mkuu amesema “Nyote mtakubaliana nami kwamba leo ni siku muhimu
kwa sekta ya nyumba kwani ujenzi wa nyumba za namna hii ni muhimu katika
kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwenye Taasisi za Serikali
sambamba na kuboresha ufanisi wa wafanyakazi wetu.”
“Vilevile, utekelezaji wa mradi huu umetoa
ajira zipatazo 1,000 ikiwa ni sawa na ajira 800 za mafundi na ajira 200
kwa watoa huduma za chakula yaani mama lishe. Upatikanaji wa ajira hizo
umechangia kuongeza kipato kwa walengwa na kusaidia kujikwamua dhidi ya
umaskini.”
Amesema
ujenzi wa majengo hayo ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 inayosisitiza ujenzi wa majengo ya
ofisi na makazi kwa watumishi wa umma kwa lengo la kuipunguzia Serikali
gharama kubwa ya kodi ya pango pamoja na kuimarisha utendaji na
uwajibikaji wa watumishi wa umma katika kuwahudumia Watanzania.
Kadhalika,
Waziri Mkuu ametoa wito kwa Shirika la Nyumba la Taifa, kuendelea na
kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba za makazi pamoja na biashara kwani lengo
la Ilani ya CCM ya mwaka 2015 ni kuliwezesha Shirika la Nyumba la Taifa kuwa Mwendelezaji Miliki Mkuu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema watendaji wa shirika hilo wanapaswa kuongeza kasi
ya ukusanyaji kodi ili kuongeza mapato ya shirika. “Serikali kwa upande
wake, itaendelea kutoa Ushirikiano wa karibu kwa Shirika katika kutatua
changamoto zinazokabili utekelezaji wa malengo ya shirika hili.”
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Idara ya Uhamiaji kwa
kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka pamoja na kufanikisha maboresho
mbalimbali kama vile Uhamiaji Mtandao ambapo sasa huduma za pasipoti,
vibali vya ukaazi, viza, usimamizi na udhibiti wa mipaka vinafanyika kwa
njia ya kielektroniki. “Utekelezaji mzuri wa mageuzi ya Uhamiaji
Mtandao umewezesha idara hii kupata tuzo ya ushindi wa pasipoti yenye
ubora duniani kwa mwaka 2019.”
Waziri
Mkuu amesema ushindi huo, umelipatia sifa na heshima kubwa Taifa
Kimataifa. “Halikadhalika, nimefurahishwa na taarifa kuwa ujenzi wa
Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji, Dodoma nao unaendelea vizuri.
Ninawahimiza endeleeni hivyo kwa mustakabali wa ustawi wa Taifa letu.”
Awali, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala aliishukuru Serikali
ya Awamu ya Tano kwa kuwezesha Idara ya Uhamiaji, kupata nyumba 103 za
makazi kwa ajili ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji kwani hatua hiyo ni
kielelezo cha vipaumbele vya Serikali katika kuboresha makazi ya askari
wa vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi kwa ujumla.
“Aidha,
tunalipongeza pia Shirika la Nyumba la Taifa, kwa kubuni mradi mkubwa
kwa ajili ya kuboresha mazingira ya makazi ya Wananchi kwa kujenga na
kuuza nyumba kwa bei nafuu, ambapo nasi tumekuwa wanufaika wa mradi huu.
Gharama za nyumba 103 za makaazi ya watumishi wa Idara ya Uhamiaji, ni
kiasi cha sh. 5,306,000,000.”
Alisema
upatikanaji wa nyumba hizo utasaidia Maafisa na Askari wa Idara ya
Uhamiaji kuishi katika maeneo yao maalum, badala ya ilivyokuwa hapo
awali ambapo walilazimika kutafuta nyumba za makazi uraiani. Sambamba na
hilo, itasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu, kwani
itakuwa ni rahisi kuwapata askari walio katika eneo moja mara
wanapohitajika.
Makabidhiano
hayo yameshuhudiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Mhe. William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George
Simbachawene, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo,
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Dkt. Maulid Banyani, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo na Maafisa wengine wa Serikali.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi funguo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, George Simbachawene, kama ishara ya kukabidhi nyumba 103, kwa
akijili ya Makazi ya Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nichini,
zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Juni, 2, 2020. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Kamishina Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala,
akionesha ishara ya funguo, baada ya kukabidhiwa nyumba 103, kwa
akijili ya Makazi ya Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nichini,
zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Juni, 2, 2020. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment