HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 27, 2020

NAIBU WAZIRI ATAKA DARAJA LA KOGA KUKAMILIKA MWEZI

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza jambo na Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kassanda, wakati akikagua ujenzi wa sehemu ya barabara ya Komanga - Kasinde (km 112.18), inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Katavi.
 Kazi za kusambaza lami katika sehemu ya barabara ya Komanga - Kasinde ikiendelea. Kazi hiyo inafanywa na mtambo maalum wa kisasa unaogusa upana wote wa barabara na wenye uwezo wa kusambaza lami kilometa 1.2 kwa siku.




Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amemuagiza mkandarasi wa kampuni ya China Wu Yi kukamilisha ujenzi wa Daraja la Mto Koga lenye urefu wa mita 120 ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu na kuruhusu magari kupita juu yake
badala ya kutumia daraja la zamani.
 
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kukamilika mapema kwa ujenzi wa barabara ya Tabora - Koga - Mpanda (km 342.7), kwa kiwango cha lami kwani itaongeza uchumi wa wananchi na kuongezeka kwa shughuli za kibiashara kwa kuwa ni
mikoa yenye uzalishaji mwingi wa bidhaa mbalimbali za kilimo, ufugaji wa nyuki, madini na utalii.

Ametoa agizo hilo akiwa mkoani Katavi, wakati akikagua hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya Tabora - Koga - Mpanda ambao unahusisha na ujenzi wa daraja hilo ambalo kipindi cha mvua mawasiliano kati ya wilaya ya Mlele mkoani
Katavi na wilaya ya Sikonge mkoa wa Tabora hujifunga na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.

"Nahitaji kazi iendelee haraka, sisi kama Serikali na Wizara tumejipanga kuona kwamba barabara hii inakamilika mapema na kuondoa ile adha waliyokuwa wanaipata wananchi wa Katavi na Tabora", amesititiza Naibu Waziri huyo.

Kwandikwa, amesema ujenzi wa daraja hilo ambalo limekuwa likisababisha kufungwa kwa barabara ya Mpanda – Tabora kutokana na kujaa maji wakati wa mvua za masika itakuwa historia kwa kuwa urefu wa barabara umeongezeka kwa mita 1.5 kutoka pale ilipokuwa.
 
"Wizara imeona kwamba maeneo yote yenye changamoto kama hapa yawekewe mkazo yakamilike mapema wakati ujenzi ukiendelea wa barabara", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Kuhusu ujenzi wa barabara hiyo kwa upande wa mkoa wa Katavi, Naibu Waziri Kwandikwa, amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya mradi huo ambapo sehemu ya barabara ya Kasinde - Mpanda tayari mkandarasi amekwishaweka lami kilometa 38 na sehemu ya Komanga - Kasinde kilometa 40 nazo zimekwishawekwa lami.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kassanda, ameishukuru Serikali kwa kutizama daraja hilo kwa karibu zaidi kwani takribani miezi miwili iliyopita barabara hiyo ilikuwa imejifunga kabisa lakini kwa juhudi zinazoendelea naimani wananchi hawatakwama tena hasa vipindi vya masika.

"Barabara hii imekuwa ni desturi ya kila mwaka kujifunga kwa sababu ya maji kupita juu ya daraja lililopo lakini kwa mwaka huu ni matumaini yetu tutaendelea na shughuli zetu za uzalishaji kwani mabasi na malori hayatakwama katika eneo hili", amesema Mkuu wa Wilaya hiyo.
 
Naye, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Katavi, Mhandisi Martin Mwakabende, amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa sehemu ya ujenzi wa barabara ya Kasinde - Mpanda umefikia asilimia 48 na sehemu ya barabara ya Komanga - Kasinde umefikia asilimia 58 na miradi yote hiyo inatarajiwa kumalizika kwa wakati mmoja.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua sehemu ya barabara ya Usesula - Komanga ambayo ipo mkoani Tabora na kumtaka mkandarasi Jiangxi Geo - Engineering kuongeza bidii ili kukamilisha barabara hiyo kwa muda uliopangwa.
 
Mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Tabora-Koga-Mpanda unajengwa kwa sehemu tatu ambazo ni sehemu ya Usesula - Komanga, sehemu ya Komanga - Kasinde na sehemu ya Kasinde - Mpanda ambapo utagharimu jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 481 na unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa
mwaka 2021.

No comments:

Post a Comment

Pages