Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Arusha Ladslaus Bamanyisa
akimuonesha sehemu ya eneo la mradi wa Safari City-Arusha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Dk. Angeline Mabula wakati wa ziara ya kukagua miradi inayoendeshwa na
NHC kwenye mkoa wa Arusha. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Arusha Gabriel
Daqqaro. (Picha na Munir Shemweta, WANMM).
Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC) limebadilisha viwango vya bei za kuuzia viwanja vyake kwenye mradi
wa Safari City mkoani Arusha kwa kutoa punguzo la asilimia 40% kwa viwanja
vyote.
Hayo yamebainishwa jana
na Meneja wa NHC mkoa wa Arusha Ladislaus Bamanyisa wakati akitoa taarifa ya
utekelezaji wa mradi wa Safari City kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipotembelea mradi huo akiwa katika
ziara ya kukagua miradi ya NHC pamoja na uendaji kazi wa sekta ya ardhi katika
mkoa wa Arusha.
Bamanyisa alisema,
uamuzi wa kubadilisha viwango vya bei za mauzo katika mradi huo kumesababishwa
na kusuasua kwa mauzo ya viwanja katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019 ambapo
Shirika limeuza viwanja 6 tu kwa kile alichokieleza hali ngumu ya kiuchumi .
Kwa mujibu wa Meneja
huyo wa NHC mkoa wa Arusha, viwango vipya vilivyopitishwa ni vile vya makazi ambapo sasa itakuwa Tsh 21,000 kwa kila mita ya mraba badala ya
Tshs 35,000 na Tsh 27,000 badala ya Tshs 45,000/- kwa viwanja vya biashara.
Aliongeza kuwa, tangu
kuzinduliwa mradi wa Safari City Juni 2016 shirika limeuza jumla ya viwanja 589
vyenye thamani ya shilingi 13,097,198,200/= na kukusanya
shilingi 7,981,887,540/= sawa na asilimia 61% ya makusanyo kwa viwanja
vilivyouzwa.
Hata hivyo, alisema
katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 NHC imeuza viwanja 122 vyenye
thamani ya Tsh 2,058,113,600 na kukusanya Tshs 453,952,600/- na kubainisha kuwa
viwanja vilivyobaki na kuendelea kuuzwa
ni 1,252.
Kwa upande wake Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelitaka
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuongeza kasi katika kukamilisha mradi wa safari city kwa kuweka miundombinu
ili kupata mafanikio kama ilivyo
dhamaira ya Shirika.
Alisema, Shirika la
Nyumba la Taifa linatakiwa kukahikisha eneo la mradi linakuwa na miundombiunu imara
kama vile barabara, maji pamoja na umeme ili kuwavutia wateja wanaotaka kununua
viwanja vya mradi.
‘’NHC inatakiwa kushughulikia miundombinu hapa, adha anayoipata mteja anayenunua kiwanja na kufika eneo lake ni
ngumu na hasa mvua ikinyesha atafikaje? Inabidi ajifikirie mara mbili kununua
eneo hilo‘’ alisema Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ukosefu wa miundombinu
inachangia eneo la mradi wa Safari City kutopata wateja na kubainisha kuwa mawasiliano
na watoa huduma yawe karibu ili mji uweze kupendeza.
Aidha, Dkt Mabula
amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa NHC kuhakikisha pia inautangaza mradi wa
Safari City kupitia vipindi vya televisheni na radio ili kuwawezesha wananchi
kuutambua na kununua viwanja vya mradi huo na hivyo kuliingizia Shirika mapato.
Pia Naibu Waziri Mabula
aliitaka NHC kufikiria utaratibu wa kuwakopesha watumishi wa umma viwanja vya mradi
huo kwa njia ya kulipa kwa awamu tofauti na ilivyo sasa ambapo shirika limekuwa
likiwafikiria zaidi wafanyabiashara.
Mradi wa Safari City
wenye eneo la ukubwa wa ekari 587.03 lenye viwanja zaidi ya 2,141 ulianzishwa na
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili kusaidia uendelezaji na usimamizi
madhubuti wa mpango kabambe wa jiji la Arusha kama ulivyoandaliwa, kusaidia
kupunguza uhamiaji holela pamoja na kuwawezesha watu binafsi, kampuni na
taasisi mbalimbali kupata maeneo yenye huduma muhimu za kijamii.
No comments:
Post a Comment