HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 28, 2020

PAROKO WA PAROKIA YA LUHANGA AMEWATAKA VIJANA KUTUMIA UJANA WAO KUMTUMIKIA MUNGU

Na Mwandishi Wetu

PAROKO wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji Luhanga Father Raymond Manyanga amewataka vijana kutumia ujana wao kumtumikia Mungu pasi na kuchoka.

 Akizungumza na vijana wakati akitoa homilia yake katika adhimisho la misa takatifu ya vijana iliyofanyika katika Kigango cha Mt. Peter Feba Mabibo Dar es Salaan, Fr. Manyanga amewahimiza vijana kutumia vipaji walivyopewa na Mungu kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu.

 Aidha ameongeza kuwa ujana ni kipindi cha mpito tu ambapo ni fursa ya kutengeneza maisha ya baadae kwani kuna umri utafika ambao kila mtu atakuwa mtatuzi mkuu wa matatizo ya familia yake bila kumtegemea yeyote.

"Wanangu, yaandaeni maisha yenu vyema ili baadae mkiwa na familia zenu iwe rahisi kupambana na changamoto za kifamilia na maisha kwa ujumla. Tumieni vipaji vyenu kumtukuza Mungu kikamilifu, kamwe msitumie vipaji vyenu kwa ajili yenu.

 Mtangulizeni Mungu mbele katika kutatua changamoto zenu ili muweze kupita vyema katika ujana wenu. Iweni na moyo wa ukarimu kama yule mama aliyemkaribisha nabii nyumbani kwake ili mpate neema na baraka kama tulivyosoma katika injili ya leo" alisema.

Baada ya misa hiyo, Fr. Raymond Manyanga amepata fursa ya kukutana na vijana wote na kuwapa maelekezo ya namna nzuri ya kuwajibika katika kanisa kwa majitoleo makuu ya moyo na nafsi bila kusukumwa. Vijana wa Parokia hiyo wameyapokea maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi.

No comments:

Post a Comment

Pages