HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 28, 2020

Mpango: Mifumo ukusanyaji takwimu kuendelea kuboreshwa

Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Kituo cha Afya Munzeze, Bw. Linus Conrad, akimuongoza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (katikati), kukagua majengo matano ya Kituo cha Afya Munzeze,  kilichopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, likiwemo jengo la upasuaji, wodi ya wazazi, maabara, chumba cha kuhifadhia maiti na nyumba ya Mganga Mkuu. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina.



JOSEPHINE MAJURA NA PETER HAULE, WFM

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na mifumo ya ukusanyaji wa takwimu ili kuwa na takwimu bora kwa ajili ya kutunga sera na kupanga mipango endelevu ya maendeleo ya Wananchi ikiwa ni pamoja na kuifanyia tathmini na ufuatiliaji mipango hiyo.

Dk. Mpango aliyasema hayo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoa wa Kigoma ambalo hadi wakati linawekewa jiwe la msingi limegharimu shilingi milioni 173.
 
“Jengo hili litakapokamilika litaboresha zaidi utendaji kazi kwa watumishi pamoja  na upatikanaji na usambazaji wa takwimu  kwa wadau mbalimbali wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na hususan wakati  huu wa maandalizi ya zoezi la kitaifa la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika mwaka 2022” alisema.

Dk. Mpango aliipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa namna ambavyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa weledi na kuipatia nchi takwimu bora  ambazo ndizo zinatumika katika kusukuma gurudumu la maendeleo.

“Mafanikio ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano ambayo tunajivunia leo yamejengwa kwa msingi mzuri wa matumizi bora ya takwimu ambazo zinazalishwa na taasisi yetu hii’ aliongeza.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa alisema, kuwa ujenzi wa Jengo hilo ni miongoni mwa mikakati ya Ofisi yake ya kuboresha miundombinu itakayo wezesha  matumizi ya teknoljia ya kisasa katika shughuli za ukusanyaji na uchakataji wa takwimu mbalimbali hatua iliyolenga kupunguza matumizi ya Serikali.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya aliishukuru Serikali kwa kutenga fedha za kumalizia jengo hilo na kuomba fedha zilizotengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Ofisi hizo zitolewe mapema kwenye robo ya kwanza ya utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2020/21 ili liweze kukamilika mwezi Septemba kama ilivyopangwa.

Ujenzi wa jengo hili ulioanza mwaka 1994 wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili chini ya ufadhili wa Ofisi ya Takwimu ya Sweden (Statistics Sweden) iliyokuwa na ushirikiano na Idara Kuu ya Takwimu chini ya Wizara ya Mipango.

Statistics Sweden kwa mujibu wa kumbukumbu zilizoko waligharamia jengo hili kwa jumla ya Shillingi milioni tano mwaka 1994 na Serikali za Awamu ya Tatu, na Nne ziliendelea na juhudi za kugharamia ujenzi wake hadi lilipofikia kwa gharama ya shilingi 173,386,000.

No comments:

Post a Comment

Pages