*Ampongeza
Waziri Mkuu kwa uhodari wake wa kuchapa kazi
RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza mkandarasi wa Kampuni ya
China Railway 15 Bureau Group Corporation kutoka China aliyesaini mkataba wa
ujenzi wa barabara ya kutoka Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa km 53.2 kwa
gharama ya sh. 59,286,553,159 aanze kazi mara moja.
Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Juni 27, 2020) alipozungumza na
wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwa njia ya simu alipompigia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
wakati wa tukio la utiaji saini mkataba wa makubaliano ya ujenzi wa barabara ya
Ruangwa-Nanganga km 53.2 kwa kiwango cha lami.
“Nashukuru ahadi niliyoitoa leo imeanza kuzaa matunda na ilimradi
mkandarasi amekubali kusaini aanze mara moja kupeleka mitambo kwenye eneo la mradi
na nitakuja kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo.”
Pia, Rais Dkt. Magufuli ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi kwa
uhodari wake katika kufanya kazi. “ Endeleeni kumuani Mheshimiwa Majaliwa,
amekuwa akinisaidia. Aendelee kuchapa kazi kwa ajili ya Ruangwa na Tanzania.”
Kwa upande wake, Waziri
Mkuu amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kuthamini na kujali maendeleo ya
Watanzania wakiwemo na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwa sababu ujenzi wa
barabara ya Ruangwa hadi Nanganga kwa kiwango cha lami ni utekelezaji wa ahadi
yake.
“Leo hii ni siku ya kihistoria kwa sababu kile ambacho tulikuwa
tunatamani, kikaahidiwa hapa na kiongozi wa nchi Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli
alipofanya ziara Ruangwa aliweza kuvunja kiu yetu Wana-Ruangwa toka alivyokuwa
anaingia Nanganga wananchi walimuomba asimame na yeye alisimama akijua kuwa
hawa wana hamu ya maendeleo.”
Waziri Mkuu aliongeza kuwa baada ya Rais Dkt. Magufuli kusimama aliwaambia kuwa “najua hamu yenu ni ya maendeleo,
lakini mimi ninaanza kuwaondolea kiu ya muda mrefu ya barabara yenu kutoka hapa
Nanganga mpaka Ruangwa kwa kuijenga kwa kiwango cha lami. Sifa moja ya Rais Dkt.
Magufuli ni kusema na kutenda na ametekeleza.”
Vilevile, Waziri Mkuu amewataka Watanzania wote waendelee kushirikiana
bila ya kujali itikadi zao za kisiasa kwa sababu maendeleo hayana chama na miradi
ya maendeleo anayoitekeleza katika maeneo mbalimbali nchini imekuwa
ikiwanufaisha wananchi wote.
Akizungumzia kuhusu Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group
Corporation kutoka China iliyosaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya kutoka
Ruangwa hadi Nanganaga kwa kiwango cha lami, Waziri Mkuu amesema ni miongoni
mwa kampuni kubwa zinazojenga kwa viwango.
Waziri Mkuu
ameendelea kuwashukuru wananchi wa wilaya hiyo kwa
umoja na mshikamano mkubwa waliompatia katika kipindi chote cha miaka mitano na
amewaahidi kuendelea kuwatumikia bila ya ubaguzi wa aina yoyote na kwamba
waendelee kuiunga mkono Serikali ambayo imefanikiwa kutekeleza ilani ya
uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 kwa vitendo.
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
anayeshughulikia Ujenzi, Dkt. Elias Kuandikwa amesema barabara hiyo itakuwa na
madaraja makubwa matatu na makaravati 31 na kwamba itajengwa kwa wakati na kwa kuzingatia
viwango vya ubora vinavyohitajika.
Dkt. Kuandikwa aliongeza kuwa barabara zingine za mkoa wa Lindi
zikiwezo za kutoka Nachingwea hadi Liwale yenye urefu wa km 159 ipo katika
hatua ya usanifu na barabara ya kutoka Liwale hadi Nangurukuru km 230 na Nanganga-Nachingwea-Masasi
zipo katika utaratibu wa ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mapema, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)
Mhandisi Patrick Mfugale alisema barabara ya Nachingwea - Ruangwa -
Nanganga ni barabara muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Lindi kwani inaunganisha pia mkoa wa Lindi na mikoa
jirani kwa barabara kuu ya Mtwara – Dar es Salaam na Mtwara – Masasi – Songea.
“Ili
kurahisisha utekelezaji, mradi huu umegawanywa katika sehemu mbili: Sehemu ya
Nachingwea hadi Ruangwa yenye urefu wa kilometa 52.8 na sehemu ya pili ni kutoka
Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 53.2. Serikali imeamua kuanza
ujenzi wa sehemu ya Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 53. 2 na
upana wa meta 10.0, kwa kutumia fedha za ndani na itajengwa kwa muda wa miezi
27.”
Mhandisi
Mfugale aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakapokamilika utasaidia kukuza
kilimo na utalii katika wilaya ya Ruangwa na mkoa wa Lindi kwa ujumla. Aidha
mradi utakapokamilika utachochea ukuaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na
kijamii kwa wananchi waishio maeneo ya Ruangwa, Nanganga na Nachingwea.
Wakizungumza
kuhusu ujenzi wa barabara hiyo wananchi wa wilaya ya Ruangwa walimshukuru Rais
Dkt. Magufuli pamoja na Waziri Mkuu ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa kwa uamuzi
wao wa kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani itasaidia katika
ukuaji wa uchumi.
Miongoni mwa
wananchi hao ni pamoja na dereva wa basi litokalo Ruangwa kwenda Masasi, Omar
Njinji ambaye amesema kutengenezwa kwa barabara hiyo kutarahisisha shughuli za
usafirishaji wa abiria na mizigo, pia nauli zitapungua na maendeleo ya wilaya
nayo yataimarika.
Dereva
mwingine Issa Lingonda wanaishukuru sana Serikali kwa uamuzi wake wa kujenga
barabara hiyo kwa sababu ubovu wake unasababisha magari kuharibika mara kwa
mara. “Tunamshukuru sana Rais pamoja na Mbunge wetu kwani tutapumzika kwenda
gereji maana siku mbili tunafanyakazi siku mbili gereji. Ikiwekwa lami vyombo
vyetu vya usafiri vitadumu na nauli zitapungua.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Dkt. Elias Kuandikwa wakishuhudia wakati Mkurugenzi Mkuu
wa Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale na
Mwakilishi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation, Su
Jinlan wakitia saini mkataba wa makubaliano kati ya serikali na Kampuni
hiyo ya ujenzi wa barabara ya Nanganga -Ruangwa kwa kiwango cha lami
yenye urefu wa Kilomita 53.2 kwa gaharama ya Sh. Bilioni 59.28. Utiaji
saini wa Mkataba huo ulifanyika kwenye uwanja wa Likangala , Ruangwa,
Juni 27, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TAROADS), Mhandisi
Patrick Mfugale na Mwakilishi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau
Group Corporation, Su Jinlan wakibadilishana nakala za mkataba wa
makubaliano kati ya serikali na Kampuni hiyo wa ujenzi wa barabara ya
Nanganga -Ruangwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Kilomita 53.2 kwa
gaharama ya Sh. Bilioni 59.28. Mkataba huo ulitiwa saini na kushuhudiwa
na Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa kwenye uwanja wa
Likangala, Ruangwa Juni 27, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale (kulia) na Mwakilishi wa Kampuni ya
China Railway 15 Bureau Group Corporation, Su Jinlan wakionyesha
nakala za mkataba wa makubaliano kati ya serikali na Kampuni hiyo ya
ujenzi wa barabara ya Nanganga -Ruangwa yenye urefu wa Kilomita 53.2
kwa gaharama ya Sh. Bilioni 59.28. Mkataba huo ulitiwa saini huku
ukishuhudiwa na Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa kwenye
uwanja wa Likangala, Ruangwa Juni 27, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
No comments:
Post a Comment