HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 15, 2020

Tamko la THBUB wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kukuza Uelewa wa Dhuluma dhidi ya Wazee Duniani

JUNI 15 kila mwaka Tanzania na jumuiya ya kimataifa huadhimisha Siku ya “Kukuza Uelewa wa Dhuluma dhidi ya Wazee Duniani (World Elder Abuse Awareness Day).” Lengo la siku hii iliyopitishwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa
Mataifa kwa Azimio Na. A/RES/66/127 la Desemba 19, 2011 ni kutoa fursa kwa jamii kukuza uelewa wa dhuluma na unyanyasaji wanaokumbana nao wazee duniani kote na kupambana na tatizo hilo.

Aidha, hii ni siku ya wadau kutafakari njia bora ya kupunguza vitendo vya dhuluma kwa wazee kwa kukemea dhuluma hizo, kuandaa na kukuza sera, mikakati, miongozo, mifumo na sheria rafiki kwa ustawi wa wazee.
 
Ukosefu wa hatua zinazofaa au kitendo chochote kinachopelekea maumivu, usumbufu, changomoto za kisaikolojia, kiafya, kiuchumi kwa wazee na zinazoathiri
haki zao ni dhuluma na unyanyasaji dhidi yao. Vitendo hivi vinapaswa kukemewa na kupigwa vita na wote wanaojali haki na ustawi wa wazee.
 
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2002 na 2012, hapa nchini kuna ongezeko la idadi ya wazee la takriban asilimia mbili (2) kwa mwaka; kutoka wazee 1,952,041 mwaka 2002 hadi wazee 2,507,568 mwaka 2012. Hapa nchini, kama ilivyo duniani kote, hivi sasa idadi ya wazee inaongezeka kwa kasi.

 Hivyo, kwa kadiri idadi ya wazee inavyoongezeka ndivyo changamoto zinazowakabili zinavyoongezeka pia. Kwa msingi huo jitihada mahsusi lazima zifanyike kukabiliana nazo.
 
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha siku hii kwa lengo la kuikumbusha Serikali na jamii juu ya umuhimu wa kuheshimu na kulinda haki za binadamu wakiwemo wazee.

Tume inatambua na kuthamini jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali na wadau katika kushughulikia masuala ya wazee chini. Pamoja na jitihada hizo bado kuna changamoto zinazowakabili wazee ambazo zinapaswa kutambuliwa na kupatiwa ufumbuzi mapema.

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na Wazee kutofaidika na mafao mbalimbali ya mifuko ya hifadhi ya jamii, huduma duni za afya, kutokuwepo kwa sheria maalumya wazee, mauaji ya wazee, umaskini, kutelekezwa, manyanyaso, unyanyapaa na
usalama mdogo.
 
Kwa kuzingatia kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu, inayosema: “Paza sauti dhidi ya unyanyasaji kwa wazee” (Lifting up voices for elder abuses), THBUB inapenda kutoa mapendekezo yafuatayo kwa Serikali, wadau na jamii kwa ujumla:
 
1. Serikali iharakishe utungwaji wa Sheria ya wazee ili haki za wazee zilindwe kisheria;
 
2. Vyombo vya sheria viendelee kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mikakati ya kukomesha mauaji ya wazee nchini;

3. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbali mbali iendelee kuelimisha jamiii kuhusu haki za wazee;

4. Wizara ya Afya iendelee kuboresha huduma za afya kwa wazee ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa watoa huduma maalum wa afya na vyumba maalum kwa ajili ya wazee;

5. Halmashauri zitambue na kutenga bajeti kwa ajili ya familia yatimazinazolelewa na wazee.
 
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaamini kwamba tukidhamiria kama  Taifa, tunaweza kupunguza na hatimaye kukomesha kabisa dhuluma dhidi ya wazee
hapa nchini.

Imetolewa na:

(SIGNED)
Mohamed Khamis Hamad
Makamu Mwenyekiti

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

No comments:

Post a Comment

Pages