HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 13, 2020

Ubovu wa miundombinu, umeme vyakimbiza wawekezaji Nanjilinji A

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nanjilinji A, wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Mohamedi Mkalimaga, akizungumza na Wajumbe wa Serikali ya Kijiji na Kamati ya Maliasili ya kijiji hicho hivi karibuni. (Picha na Suleiman Msuya).
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa mkaoni Lindi, Christopher Ngubiagai, akizungumza na waandishi wa habari pichani hawapo kuhusu mipango mbalimbali ya wilaya kuhusu kutatua kero ya barabara yenye utefu wa kilomita 64 kutoka Kilanjelanje hadi Nanjilinji.



Na Suleiman Msuya, Kilwa

UBOVU wa miundombinu na ukosefu wa umeme katika kijiji cha Nanjilinji A wilayani Kilwa mkoani Lindi zimetajwa kuwa ni sababu ya kijiji hicho ambacho kina rasilimali misitu na ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo kukosa wawekezaji.

Hayo yameanishwa na viongozi na wananchi wa kijiji hicho wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wakati wa ziara ya kuangalia shughuli za maendeleo kijijini hapo hivi karibuni.

Akizungumza kadhia hiyo Mwenyekiti wa kijiji cha Nanjilinji A, Mohamedi Mkalimaga alisema wamekuwa kuwa na changamoto ya barabara na umeme kwa miaka yote tangu kupata uhuru hali ambayo inawakwamisha kuwa na maendeleo.

Mkalimaga alisema barabara yao ina urefu wa kilomita 64 kutoka Kilanjelanje hadi Nanjilinji A, hivyo wanaomba Serikali iipe kipaumbele cha matengenezo kwa kuwa ina mchango mkubwa kiuchumi, jamii na maendeleo.

"Naomba nitumie nafasi hii kuiomba Serikali hasa Rais John Magufuli ambaye anatumia msemo wa kuwasaidia wanyonge atujengee hii barabara kwa kuwa ina mchango mkubwa kwenye uchumi wa kijiji, wilaya, mkoa na taifa kupitia mazao yanayopatikana ikiwemo zao la ufuta," alisema.

Mtendaji wa kijiji hicho Muhidin Mkunguru alisema wanaomba Serikali kutengeneza barabara hiyo kwa haraka ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo.

"Barabara hii inatumika sana hasa kipindi cha mavuno ya ufuta lakini pia rasilimali misitu ambazo zinavunwa kwa kufuata taratibu za uvunaji endelevu," alisema.

Mansour Mwalimu Mjumbe wa Serikali ya kijiji aliomba Serikali kuhakikisha kijiji hicho kinapata umeme wa uhakika mapema ili shughuli za kiuchumi na biashara ziweze kuimarika.

Katibu wa Kamati ya Maliasili ya kijiji, Said Bakari alisema ubovu wa barabara umesababisha kukosa mamilioni ya fedha ambazo zingeingia kupitia wawekezaji wa uvunaji wa rasilimali za msitu wa kijiji chao.

Akizugumzia changamoto hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, alisema wanaijua na wanaifanyia kazi kwa kushiriana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ambapo kwa sasa wanachofanya kuikwangua.

Ngubiagai alisema mkakati uliopo kwa sasa ni barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 64 kujengwa kwa kiwango cha lami ambapo itafika hadi wilayani Ruangwa.

"Tunajua hii changamoto na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliahidi kuwa itajengwa kwa kiwango cha lami kwa sasa kinachofanyika ni upembuzi yakinifu na baadae ujenzi utaanza tunatambua mchango wa Nanjilinji A kwa uchumi wa Kilwa, Lindi na nchi kwa ujumla ni mkubwa hasa kupitia zao la ufuta," alisema.

Aidha, mkuu huyo wa wilaya alisema changamoto ya umeme itatatuliwa ifikapo Julai Mosi mwaka huu hivyo kuwataka wananchi wa Nanjilinji kuwa na amani.

No comments:

Post a Comment

Pages