Wanafunzi wakiandamana Siku ya Mtoto Afrika.
Mkurugenzi wa HakiElimu, Dk. John Kalage.
Na Happiness Mnale
KATIKA siku za hivi karibuni sekta ya elimu imepitia kipindi kigumu.
Maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19) yamesababisha sekta hiyo kuvurugika na kuathirika duniani.
Takwimu za Umoja wa Mataifa kupitia Shirika la Elimu (UNESCO) zinaeloleza kwamba takribani wanafunzi bilioni 1.54 wakiwemo watoto wa kike milioni 743 duniani wameathirika na virusi vya corona kwa kutokuwepo shuleni na hivyo kukosa haki ya kujifunza na kupata elimu rasmi.
Kwa Barani Afrika, hatari ni kubwa zaidi kwa kuwa hali ya upatikanaji wa elimu ina changamoto nyingi hata kabla ya maambukizi ya virusi vinavyosababisha COVID -19.
Katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, hata kabla ya shule kufungwa takribani 1 ya 5 ya watoto wa umri wa miaka sita mpaka 11 hawakuwa shuleni; 1 kati ya 3 ya watoto wa umri wa miaka 12 hadi 14 nao pia hawakuwa shuleni huku takribani asilimia 60 ya vijana wa umri wa miaka 15 hadi 17 wanaopaswa kuwa shule za sekondari hawakuwa shuleni.
Nchini Tanzania, Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto (UNICEF) linaeleza kwamba zaidi ya watoto milioni mbili wa umri wa shule ya msingi na zaidi ya watoto Milion 1.5 ya watoto wa umri wa kuwa shule za Sekondari, hawako shuleni.
Makala haya yanaangazia maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika na mustakabali wa elimu hasa katika kipindi hiki cha janga la Corona.
Mkurugenzi wa Shirika la HakiElimu, Dk. John Kalage, anasema ni vyema kuangalia na kurahisisha changamoto ili kuwahakikishia watoto upatikanaji wa haki yao ya elimu bora na yenye usawa.
Umuhimu wa watoto kuwa shuleni na kujifunza hauhitaji kupigiwa mbiu, bali ni zile athari na hasara za wao kuwa nje ya mifumo rasmi ya kujifunza.
Kalage anasema Tanzania, pamoja na kufunguliwa kwa vyuo na kuruhusiwa kwa wanafunzi wa kidato cha sita kuendelea na mitihani yao ya mwisho; wanafunzi milioni 12 wa ElimuMsingi wanaendelea kubaki nyumbani kwa hadi jumatatu ijayo shule zitakapofunguliwa.
Anasema kipindi ambacho shule imefungwa nje ya utaratibu rasmi wa likizo kimefanya kugundua namna mfumo wa utoaji elimu ulivyo na mapungufu mengi.
Kalage, anasema hofu iliyooneshwa na Serikali, wazazi na wadau wengine wa elimu kuhusu hatima ya ujifunzaji na ufundishaji inatoa picha halisi ya namna mfumo wa ujifunzaji na ufundishaji ulivyojifungia kwa sehemu kubwa katika kuta za madarasa peke yake.
“Mijadala iliyoibuka kuhusu njia mbadala za kuendelea kujifunza na kumlinda mtoto wakati wa kipindi hiki cha COVID-19, ni ushahidi tosha wa namna ambavyo mfumo wetu wa utoaji elimu ulivyo nyuma ya wakati,”anasema.
Kalage anasema mathalani, moja ya njia mbadala iliyotiliwa mkazo ni matumizi ya vipindi vya runinga na redio kumwezesha mwanafunzi kuendelea kujifunza akiwa nyumbani.
Kwa mujibu wa utafiti wa bajeti za kaya mwaka 2017-2018, asilimia 43 ya nyumba zina redio, runinga asilimia 24 na simu asilimia 78 pekee.
Pamoja na ukweli kwamba idadi ya Watanzania wenye uwezo wa kusikiliza vipindi vya redio na runinga kupitia simu janja na simu za kawaida, unaongezeka, lakini bado idadi inaonesha siyo kaya zote zinaweza kutumia njia hizi kwa watoto wao kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumiliki njia hizi za mawasiliano.
Kalage anasema kwamba ina maana kwamba njia hizo, pamoja na changamoto zake, bado ni njia ambazo haziwezi kuwafikia wanafunzi wote hasa wanaotoka kwenye familia masikini.
Anasema mapendekezo ya kutumia teknolojia hasa ya kimtandao nayo ina mapungufu yake pamoja na kuwa ni njia muafaka.
“Ukiachilia mbali ujuzi mdogo wa wazazi, walimu na wanafunzi kwenye namna ya kutumia teknolojia ya mtandao na vifaa vyake kama kompyuta/tarakilishi na simu, bado idadi kubwa ya wanajamii hawana uwezo wa kununua vifaa na kugharamia bando zinazowezesha mtandao kuwepo,”anasema.
Ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya Desemba, 2019 ilitaja Tanzania ilikuwa na jumla ya watumiaji wa mtandao 25,794,560 ambayo ni asilimia 46 tu ya soko.
Ukitazama wastani wa gharama za matumizi ya intaneti bado uko juu pia ambapo kwa wastani angalau MB 75 ni Sh. 1,000 kwa siku, sawa na Sh. 30,000 kwa mwezi.
Kwa hatua hiyo ni familia chache zinazoweza kugharamia kiasi hicho cha fedha kwa mwezi kwa ajili ya mtandao pekee.
Hivyo ni dhahiri kwamba njia hizo pia ni wazi zitazidi kuwaacha pembeni sehemu kubwa ya wanafunzi ambao wengi wanatoka familia masikini na wanaosoma shule za umma.
Dk. Kalage anasema kwa bahati mbaya, utamaduni wa utoaji elimu haumfanyi mzazi/mlezi kuwa sehemu kuu ya kujifunza kwa mtoto.
“Ni nadra sana shule zetu, hasa za umma, wameweza kujenga utamaduni wa kutoa kazi za kufanyia nyumbani kwa watoto (homework) ambazo anatakiwa kufanywa kwa pamoja na wazazi nyumbani,”anasema.
Anasema hatua hiyo inasababisha hatari zaidi kwa mwanafunzi kuwa nyumbani kwa kuwa anakosa uhakika wa kuendelea kujifunza kupitia wazazi/ walezi.
Kalage anasema kwamba ni muhimu serikali na wadau kuendeleza mijadala zaidi juu ya upatikanaji wa elimu ya watoto wetu katika kipindi cha maambukizi ya COVID-19 na baada ya maambukizi haya.
“Ni vizuri kuja na mipango itakayosaidia kufidia ombwe la ujifunzaji lililoletwa na kufungwa kwa taasisi za elimu,”anasema.
Kufuatia hatua hiyo Kalage anapendekeza kuzitumia changamoto zilizotokana na janga la corona kuwa fursa katika kujifunza namna bora ya kuimarisha mfumo wetu wa elimu ili uweze kuwa nyumbufu na unaokidhi matakwa ya utoaji wa elimu na unaeondana na mahitaji ya karne ya 21.
“Tunapendekeza pia kuwekeza kwa nguvu katika matumizi ya teknolojia katika utoaji elimu kwa watoto wetu. Ni lazima mabadiliko yafanyike ya namna shule zinaweza kutumia teknolojia zaidi kuambukiza maarifa yanayokusudiwa,”anasema.
HakiElimu wanapendekeza janga hili kuwa fursa ya kuleta mabadiliko katika namna ya uwekezaji katika uendeshaji wa shule na taasisi za elimu.
“Kuna mapungufu makubwa ya miundombinu na hasa ya Tehama ambayo ingeweza kurahisisha ujifunzaji, changamoto iliyoletwa na COVID-19 inapaswa iwe fursa ya kutafakari namna ambavyo tunaweza kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto awapo shuleni au nyumbani,”anasema.
Anaongeza kwamba changamoto na uzoefu katika kipindi cha COVID-19, vinapaswa kuwa fursa ya kufanya marekebisho ya sheria za kodi, tozo na uwezeshaji wa wananchi katika matumizi ya teknolojia.
No comments:
Post a Comment