WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema suala la ulinzi wa
nchi ni la Watanzania wote na siyo la kuwaachia vyombo kama Jeshi la Wananchi, Uhamiaji,
Polisi au Magereza.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumapili, Julai 19, 2020)
wakati akizungumza na wakazi wa Matogoro, wilayani Tandahimba, mkoani Mtwara.
“Suala la ulinzi ni letu sote na siyo la Serikali peke
yake kupitia wanajeshi au polisi. Kila Mtanzania anawajibika kuilinda nchi hii,
kuanzia nyumbani kwako hadi kwa jirani yako. Niwakumbushe kwamba tunapaswa
tuendelee kujenga utamaduni wa kutoa taarifa, kila unapoona kuna jambo ambalo
una shaka nalo,” amesema.
Amesema mikoa ya pembezoni ya Kigoma, Kagera, Mtwara,
Ruvuma, Katavi, Songwe, Mbeya, Lindi, Mara, Tanga, Kilimanjaro na Arusha ni
mikoa ambayo wananchi wake ni lazima wawe wepesi wa kutoa taarifa. “Ni lazima Watanzania
tuwe makini, hata kama tuna utaratibu wa kutembeleana, ni lazima tuwe macho.”
Amesema Serikali imeweka mwongozo kwa wageni
wanaoingia nchini ambao ni lazima apite kwenye mpaka ulio rasmi na kutoa
taarifa zake. “Mgeni huyo atapaswa aeleze amekuja nchini kufanya nini, amekuja na
nani na atakaa kwa siku ngapi.”
“Tunapomuona mgeni huko kijijini, ni lazima tujiridhishe
kuwa mgeni huyo amepitia kwenye sehemu zote husika. Kama mtu utaona shaka, toa
taarifa kwa mtendaji naye atapeleka taarifa hizo ngazi za juu hadi kwa Mkuu wa
Wilaya.”
Amesema kila mwananchi atakapojiridhisha kuwa nchini kuna
amani, kutakuwa na hali ya utulivu ambayo ni muhimu kwa usalama wa ndani na nje.
Amesema wilaya za Masasi, Nanyumbu na Mtwara Vijijini
ni maeneo yanayovutia watu kuingia nchini kwa sababu ya zao la korosho na biashara
zilizopo. “Hapa Tandahimba kuna mzunguko mkubwa wa fedha. Tandahimba ina idadi
kubwa ya wafanyabiashara, hivyo ni rahisi kwa mtu kuja kufanya ujambazi au
kuiba mazao yenu. Tunataka muwe macho, lengo letu ni kuhakikisha eneo hili
lisiwe moja ya maeneo hatarishi,” amesisitiza.
No comments:
Post a Comment