Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akifafanua jambo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo (kushoto) akiwa
katika ofisi ya ardhi mkoa wa Rukwa baada ya kuizindua rasmi jana. Wa pili
kulia ni Kamishna Msaidizi wa ardhi mkoa wa Rukwa Swagile Msananga na wa tatu
kulia ni Katibu Tawala mkoa wa Rukwa Benard Makali. (Picha na Munir Shemweta-WIZARA YA
ARDHI).
Na Munir Shemweta, WANMM SUMBAWANGA
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewaagiza Makamishna
Wasaidizi wa ardhi katika ofisi za mikoa kukaa na taasisi za serikali
zinazodaiwa kodi ya pango la ardhi kuangalia namna bora ya kulipa madeni
wanayodaiwa.
Dkt Mabula alitoa agizo
hilo jana mkoani Rukwa wakati akizundua rasmi ofisi ya ardhi ya mkoa ikiwa ni
mfululilizo wa uzinduzi wa ofisi za ardhi katika mikoa mbalimbali nchini.
Tayari ofisi saba za ardhi katika mikoa ya Tanga, Arusha, Manyara, Singida,
Iringa, Njombe na Songwe zimezinduliwa.
Alisema, mkoa wa Rukwa
una taasisi za serikali pamoja na watu binafsi ambao kwa ujumla wao wanadaiwa
zaidi ya shilingi bilioni moja kiasi alichokieleza kuwa ni kikubwa na fedha
yake ingeweza kutumika katika shughuli za maendekeo kama vile ujenzi wa
hospitali au barabara.
Alizitaja baadhi ya
taasisi za serikali zinazodaiwa kodi ya pango la ardhi katika mkoa wa Rukwa kuwa
ni pamoja na Shirika la umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi Stadi (VETA) na Chuo Kikuu Huria na kubainisha kuwa katika
kumuwezesha rais kufanya kazi ya shughuli za maendeleo kuna wajibu wa kulipa
kodi ya pango la ardhi.
‘’Bilioni moja ni fedha
nyingi sana nawaagiza Makamishna Wasaidizi wa mikoa kukutana na taasisi pamoja
na watu wengine wanaodaiwa kodi ya pango la ardhi kukubaliana namna bora ya
kulipa fedha wanazodaiwa vinginevyo taratibu za kisheria zitafuata’’ alisema
Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Taasisi za serikali zinatenga
fedha kwenye bajeti zake kwa ajili ya kulipia gharama mbalimbali ikiwemo kodi
ya pango la ardhi na kutolipa kodi hiyo ni kutotimiza wajibu wa kulipa kodi ya
ardhi.
Alisema, Wizara yake
ilikutana na makampuni na taasisi za serikali zenye malimbikizo makubwa ya kodi
ya pango la ardhi mkoani Dodoma na baada ya kukutana ndani ya mwezi mmoja zilikusanywa
takriban bilioni ishirini na moja jambo linaloonesha kuwa taasisi hizo zinazo
fedha kwa ajili ya kodi hiyo.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya makazi Dkt Angeline Mabula alisema, wizara yake imeridhia kuanzishwa
Baraza la Ardhi la Nyumba la wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Hatua hiyo inafuatia
Dkt Mabula kuridhishwa na juhudi za wilaya ya Nkasi katika kuanzisha baraza
hilo ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi yake katika eneo la Namanyele
wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa na kusema kuwa kwa sasa takriban mabaraza mia moja
ya ardhi ya nyumba ya wilaya yameidhinishwa lakini ni mabaraza 55 ndiyo
yanayofanya kazi.
Hata hivyo, aliongeza
kwa kusema kuwa, wakati mchakato wa ofisi za baraza hilo ukiendelea mwenyekiti
wa baraza la ardhi la wilaya ya Sumbawanga anaweza kupanga ratiba na kwenda
kuendesha mashauri ya migogoro ya ardhi kwenye wilaya ya Nkasi kwa lengo la
kupunguza mashauri hao.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa
Joachim Wangabo alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa,
mkoa wake una baraza moja tu la ardhi la nyumba na wilaya huku mkoa mzima ukiwa
umesajili jumla ya mashauri 308 ya migogoro ya ardhi kuanzia mwezi januari hadi
juni mwaka huu.
Alisema, kufuatia hali
hiyo iko haja ya kuanzishwa baraza la ardhi la wilaya ya Nkasi kwa kuwa
wananchi wa wilaya hiyo wamkuwa wakipata taabu kutembea umbali mrefu na wakati
mwingine hulazimika kusafiri kilomita 160 kufuata huduma ya baraza wilayani Sumbawanga.
No comments:
Post a Comment