HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 01, 2020

MAHAKAMA YATOA HUKUMU KESI YA MKE NA MUME KUHUSU DNA ZA WATOTO WAO

Na Nwandishi Wetu

HUKUMU ya kesi ya matunzo ya watoto na kuomba mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi minne  na wa miaka tisa, kupimwa Kipimo cha Vinasaba (DNA), iliyofunguliwa na Dativa Mallya dhidi ya mume wake Festo Kavishe, imeonesha kuwa vipimo vya DNA vimeonesha watoto ni wa Kavishe.

Kwa mujibu wa Kesi hiyo namba 103 ya mwaka huu iliyofunguliwa katika Mahakama ya Watoto Kisutu, Dativa aliomba mtoto wao  mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi mitatu apimwe  Kipimo cha DNA ili kuthibitisha Festo ndiyo baba halisi wa mtoto huyo na Festo kuomba mtoto wao wa miaka tisa naye kupimwa Kipimo hicho.

Akizungumza mara baada ya kutolewa hukumu hiyo mwishoni mwa wiki, Wakili wa Kavishe, Abdul Aziz alisema hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo Devotha ambapo alitoa hati ya matunzo ya Watoto kama ilivyoelekezwa kwenye sheria yafuatwe.

Hata hivyo mahakama hiyo haikuweza kuendelea zaidi kwa sababu kuna kesi nyingine ya talaka baina ya  Mallya na mume wake Kavishe katika Mahakama ya Mkulanga hivyo kuamuru suala la matunzo kuzungumziwa huko.

Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Dativa akizungumza na waandishi kwa njia ya simu alisema yeye kama Mama mwenye uchungu na mwenye kuwaheshimu watoto wake na mwanaume aliyempatia watoto hao aliifungua kesi hiyo ya kuomba watoto kupimwa DNA ili haki ya watoto wake ipatikane na wamtambue Baba yao ni nani kwa sababu baba huyo aliwakataa na hakuwa na sababu za kueleweka.

Dativa alisema kuwa pia alitaka kuweka kando udhalilishaji juu yake kwa kuwa kitendo cha baba kusema hawa watoto siyo wake na wamefunga ndoa na wameishi miaka 10 anamaanisha hakuwa mwaminifu ndani ya ndoa hiyo.

Hata hivyo Mallya aliwaasa wababa kuwaheshimu wanawake kwa sababu wanajua siri nyingi za familia.

Kwa upande wake Kavishe alipozungumza na waandishi alidai kuwa yeye hajawahi kuwakataa watoto hao ndio sababu alikuwa akiwaelea mpaka Mallya mwenyewe alipoondoka kwenye ndoa yao.

Kavishe alidai kuwa Mallya aliondoka mwenyewe na watoto katika ndoa yao mwaka mmoja na nusu sasa hajui wanaishi wapi wala hajawahi kupata nafasi ya kuwaona watoto wake.

Alidai katika maisha yao ya ndoa mkewe Mallya alikuwa akimtamkia kuwa hao watoto siyo wake kwa sababu hana nguvu za kiume.

"lakini mimi sijawahi kuwa na mashaka kuwa watoto hawa siyo wa kwangu wala kufikiria kupima DNA ila kufuatia maneno aliyokuwa akitamka mama yao mara Kwa mara alikuwa akinitia mashaka"alieleza Kavishe.

Hata hivyo Kavishe alidai kuwa baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo waliambiwa wakae na mawakili wao wapange jinsi ya kuwaona watoto lakini mpaka sasa hilo halijafanyika na anatamani kupata nafasi ya kukaa na watoto wake.

Mallya na Kavishe walifunga ndoa ya Bomani Novemba 12,2010 na Katika ndoa  hiyo walifanikiwa kupata watoto wawili wa kwanza wa kiume mwenye umri wa miaka tisa na wa pili wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi mnne.

Katika ndoa hiyo mgogoro wa kutoelewana baina ya mume na mke unatokana na kauli za mke  ambazo zinadaiwa kuwa zimekuwa zikijirudia mara kwa mara akimtamkia Mume wake kuwa Mtoto huyo wa kike siyo wake.

No comments:

Post a Comment

Pages