Mfanyabiashara Tariq Machibya akiwa Mahakamani.
Na Janeth Jovin
Mfanyabiashara Tariq Machibya (29) maarufu Mr Kuku, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka saba ikiwemo kufanya biashara ya upatu na utakatishaji fedha wa Shilingi bilioni 17.
Machibya ambaye ni Mkazi wa Oysterbay Dar es Salaam, alifikishwa mahakamani hapo leo, Agosti 10,2020 na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi, Godfrey Isaya.
Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai katika shtaka la kwanza, katika tarehe tofauti kati ya Januari 2018 na Mei 2020, maeneo ya jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa alifanya na kusimamia biashara ya upatu kwa kukusanya fedha toka kwa umma kwa ahadi kwamba zimewekewa kwa biashara ya kuku na watu wangepata asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 kwa mtaji wa awali uliowekezwa kwa miezi sita kiasi ambacho ni kikubwa kuliko mtaji uliokusanywa.
Wakili Simon amedai kati ya Januari 2018 na Mei 2020, maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Machibya alikubali kupokea fedha kutoka kwa umma ambazo ni Sh bilioni 17 bila kuwa na leseni.
Imedaiwa kati ya Aprili 26,2019 na Januari 26,2020 maeneo ya jiji hilo, mshtakiwa alijihusisha na miamala ya Sh 6,477,297,614.83 kwa kutoa kutoka kwenye akaunti ya CRDB ya Mr Kuku Farmers Ltd huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kusimamia biashara ya upatu.
Mshtakiwa Tariq Machibya (29) maarufu Mr Kuku (aliyevaa shati jekundu) akitoka Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mara baada ya kumaliziwa kusomewa mashtaka yanayomkabili.
Pia imedaiwa kati ya Januari 17,2020 na Machi 30,2020 maeneo hayo, Machibya alijihusisha na miamala ya Sh 629,249,576.36 kwa kutoa fedha hizo katika akaunti ya CRDB wakati akijua fedha hizo ni zao la biashara ya upatu.
Wakili Simon aliendelea kudai kuwa kati ya Machi 5,2020 na Aprili 17,2020 maeneo ya Dar es Salaam, mshitakiwa alijihusisha na miamala ya 1,366,718,048.46.
Katika shtaka la sita, Simon amedai kati ya Januari 17,2020 na Januari 30,2020 maeneo ya CRDB Viva tower iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam Machibya alijihusisha na miamala ya Dola za Marekani 107,893.73 na kuingiza fedha hizo kwenye akaunti ya CRDB.
Imedaiwa kati ya Machi 3 na 30, mwaka huu maeneo ya CRDB Waterfront mshitakiwa alijihusisha na kuingiza Dola za Marekani 146,300 kwenye akaunti ya Mr Kuku Farmers Ltd.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Isaya aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 24, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshitakiwa amerudishwa rumande kwa sababu mashtaka yanayomkabili hayana dhamana.
No comments:
Post a Comment