Lagos, Nigeria
Benki ya UBA imekuwa mwezeshaji mkuu (lead arranger) wa upatikanaji wa mkopo wa jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.5 ili kufanikisha mradi wa uzalishaji wa mafuta unaoendeshwa na Shirika la Taifa la Petroli la Nigeria (National Petroleum Corporation - NNPC).
NNPC, kwa kupitia Kampuni ya Maendeleo ya Petroli ya Nigeria (Nigerian Petroleum Development Company - NPDC), inahitaji jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.5 ili kuongeza uwezo wake wa uzalishaji mafuta.
Benki ya UBA itatoa Dola za Marekani milioni 200 ili kuwezesha kuongezeka kwa kiwango cha uwekezaji cha kampuni hiyo pamoja na kuboresha ukwasi wake katika uendeshaji.
Nchi ya Nigeria hutegemea zaidi sekta ya mafuta ili kujipatia mapato yake
ya fedha zakigeni.
Deni la Dola za Marekani bilioni 1.5 litalipwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itahusisha malipo ya Dola za Marekani bilioni 1 (moja) yatakayolipwa ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Awamu ya pili inahusisha malipo ya fedha za Naira ya Nigeria ambazo zitakuwa sawa na Dola za Marekani milioni 500.
Mikopo yote italipwa kupitia makato ya mapipa 30,000 kwa siku ya uzalishaji wa mafuta ghafi wa NPDC.
Benki ya UBA inayo historia ndefu ya uwezeshaji katika rasilimali za Africa ambapo mwaka 2013 iliwezesha muamala wa Dola za Kimarekani milioni 100 kati ya NPDC na kampuni ya PXF Funding.
Mwaka 2015, UBA iliwezesha muamala wa Dola Zakimarekani milioni 60 kati ya NPDC na Phoenix Export Funding Limited. UBA pia imewezesha miamala ya sekta ya mafuta katika nchi za Senegal na Congo Brazzaville.
Washiriki wengine wa mkopo wa Dola za Marekani bilioni 1.5 wa NNPC ni pamoja na Benki ya Standard Chartered, Benki ya Afrexim, Benki ya Umoja (Union Bank) pamoja na kampuni za uuzaji mafuta za Vitol na Matrix.
Mwenyekiti Makampuni ya UBA, Tony O. Elumelu alisema benki yake inawajibika kusaidia nchi ya Nigeria ili kuchochea ukuaji wa uchumi ambao kwa muda hivi sasa umekumbwa na changamoto ya kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
“Kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta pamoja na janga kubwa la Covid-19, sekta binafsi ni lazima iungane na kuchangia pakubwa ili kuchochea kuboresha uchumi,” alisema.
Benki ya UBA ni miongoni mwa waajiri wakubwa katika sekta ya fedha barani Africa, ikiwa na wafanyakazi zaidi ya 20,000 huku ikihudumia wateja zaidi ya milioni 20.
Benki ya UBA hupatikana katika nchi 20 za Africa pamoja na nchi za Uingeleza, Marekani na Ufaransa. (Na Mashirika ya Habari)
No comments:
Post a Comment