HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 19, 2020

BILIONI 4 ZATUMIKA KATIKA MIRADI YA MAENDELEO MANISPAA YA IRINGA

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Hamid Njovu wakiwa kwenye ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.

 

Na Denis Mlowe, Iringa


MKUU wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, akiambatana na mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Iringa Ahmid Njovu wamekagua miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya sh.bilioni  4 iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa ajili ya Manispaa.

Miradi hiyo imekaguliwa katika Siku ya kwanza ya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika  Halmashauri ya Manispaa  ambapo imejumuisha maeneo mbalimbali ikiwemo katika sekta ya elimu,afya na miundo mbinu kwa kukamilika na mengine ikibakiza asilimia chache kumalizika.

Miradi iliyo kaguliwa ni pamoja na Ujenzi wa nyumba ya Walimu kwa ajili ya shule ya Msingi  Kigonzile iliyoko kata ya Nduli, Ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Mtwivila , Ujenzi wa vyumba vya madarasa  na bweni shule ya ya Sekondari ya wasichana Iringa, ukarabati wa mabweni na miundo mbinu Lugalo Sekondari.

Aidha miradi mingine iliyokaguliwa ni  Ujenzi wa Jengo la uchunguzi Hospitali ya  Frelimo, Ujenzi wa maktaba ya bwalo  Sekondari ya Mawelewele, Ujenzi wa machinjio Ngelewala na Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Isikalilo ambayo madarasa sita yamejengwa na ofisi za walimu.

Wakielezea miradi baadhi ya walimu wakuu na watendaji juu ya ujenzi kutokana na fedha za serikali,Mwalimu Mkuu wa Msingi Kigonzile, Ambrose  Mpunga alisema kuwa gharama za mradi wa ujenzi wa nyumba za walimu ni sh milioni 46 ambapo fedha za EP4R ni sh milioni 25,nguvu za wananchi ni milioni 3.9 na ofisi ya mkurugenzi imechangia sh milioni 17.1

Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo utasaidia kuboresha mazingira ya ufundishaji na kuimarisha ulinzi na usalama wa shule pamoja na mazingira yake na kuishukuru serikali ya awamu ya tano kuweza kujenga nyumba hizo.

Kwa upande wa vyumba vya madarasa ya shule ya msingi Mtwivila na ofisi moja ya walimu mtendaji kata wa Mtwiviula, Ibrahim Mpogole alisema kuwa gharama za mradi ni sh milioni 68 ambapo lengo la mradi ni kuboresha mazingira ya kufundishia sambamba na kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani kwenye shule hiyo.

Aidha alisema kuwa katika kuboresha miundo mbinu ya shule hiyo halmashauri imetenga jumla ya sh milioni 50 na kuendelea kuhamasisha jamii kuchangia nguvu kazi kushirikiana katika uboreshaji huo.

Aidha mwalimu mkuu wa shule ya wasichana Iringa,Blandina Nkondola alisema kuwa kwa upande wao ujenzi wa bweni la wasichana utagharimu zaidi ya sh milioni 234 ambapo fedha za wizara ni sh milioni 75, ofisi ya mkuu wa mkoa milioni 1.5 ambapo sh. Milioni 46 ilibadilishwa kutoka kwenye fedha za chakula iliyozidi mwaka wa fedha wa 2016/2017 huku wadau wakichangia milioni 22.8, milioni 90.7 fedha za ndani na halmashauri ya manispaa walichangia milioni 44.2 ikiwa ni fedha za ujenzi wa bweni la kwanza.

Alisema kuwa bweni la pili utagharimu zaidi sh milioni 118.3 ikiwana vyanzo vya mapato ya ndani ya shule sh. Milioni 72, ofisi ya mkuu wa mkoa milioni 1.5 na halmashauri ya manispaa sh milioni 44.8.

Nkondola aliserma kuwa serikali imejenga uzio wa kudumu wa shule hiyo utakaogharimu zaidi sh milioni.141 huku mradi wanne ukiwa ni ujenzi wa majengo yapatayo 21 ambayo fedha sh zaidi ya milioni 754 zimetolewa na serikali ya awamu ya tano.

Aidha miradi mingine iliyotolewa fedha na ni ukarabati wa shule ya sekondari Lugalo ambapo zaidi ya sh. Milioni 966 kutoka serikali kuu zimetolewa  kwa ajili ya shule hiyo kongwe nchini.

Akizungumza kuhusu miradi hiyo, Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alimshukuru rais John Magufuli kwa kuweza kutoa fedha hizo ambazo zimesaidia kwa kiasi kikubwa miradi mbalimbali kukamilika na kuwataka wale ambao miradi haijakamilika kufanya hivyo haraka ili wananchi waweze kunufaika na serikali yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa manispaa ya Iringa, Hamid Njovu alisema kuwa miradi hiyo itawasaidia wananchi kwa kiasi kikubwa na kusema kuwa kama msimamizi mkuu wa miradi hiyo atahakikisha inakwisha kwa wakati ili kuleta tija kwa wananchi.

Aidha alimshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa fedha ambazo zimeleta maendeleo kwa wananchi wa manispaa ya Iringa kwani miradi mbalimbali imekwisha kamilika hali inayoifanya iringa kuwa moja ya mikoa wanayojivunia mkuu wa nchi kutekeleza ahadi zake kwa haraka zaidi.


No comments:

Post a Comment

Pages