NA ABDALLAH HIJA
UONGOZI wa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ yenye maskani yake jijini
Tanga, umefunguka kuwa utafaidika na usajili wao Beki wao wa zamani
Bakari Mwamnyeto aliyejiunga na Yanga SC hivi karibuni, kwa kupata dau
la asilimia 30 endapo Wanajangwani watamuuza timu nyingine.
Mwamnyeto aliyejiunga na Yanga kwa ajili ya kususka upya kikosi chao kwenye dirisha hili la usajili linaloendelea hivi sasa, kwa mkataba wa miaka miwili akitokea kwa Wagosi hao wa Kaya.
Inaelezwa kuwa Wagosi wa Kaya watafaidika na dili la Mwamnyeto endapo
atauzwa kwenye timu nyingine huku wakikubaliana na wanajangwani kuwa
thamani ya beki huyo isiwe chini ya Dola laki 1, huku Coastal Union
watalamba asilimia 30 ya fedha hizo.
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mguto alisema
wanatengeneza wachezaji ili wapate maendeleo na wakati huohuo klabu
ifanikiwe kibiashsara kwa hiyo suala la Mwamnyeto ni la mwanzo na
wengine watafuata.
“Kwa kiasi fulani hatujafaidika makubaliano yetu na Yanga mchezaji
atacheza kwao, ikiwa wataweza kumuuza kwa klabu nyingine basi kiasi
hicho kisiwe chini ya Dola laki 1, tulikubaliana kwamba sisi tutachukua
asilimia 30 na wao watachukua 70,” alisema Mwenyekiti huyo wa Wagosi wa
Kaya.
Katika hatua nyingine Mguto aliweka wazi suala la wao kuingia
makubaliano ya kudhaminiwa na Kampuni ya GSM kuelekea kwenye msimu wa
Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) utakaoanza hivi karibuni.
Mguto alisema jitihada walizofanya wamekubaliana na GSM waweze
kuwadhamini ikiwa si dhambi kufanya hivyo kwao japokuwa wapo na Yanga.
“Jitihada tulizozifanya tukakubaliana na wadhamini GSM, waweze
kutudhamini, si dhambi kuwadhamini yanga na sisi na hata ikiwezekana na
timu nyingine hao wanalenga biashara yao.
Kusema kweli sijaweka bayana kwamba makubaliano yetu ya udhamini yakoje ni siri kati yetu na wanaotudhamini”alisema Mguto.
No comments:
Post a Comment