HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 29, 2020

Mabadiliko ya TabiaNchi yalivyoathiri Kisala, Mvomero

Athari mabadiliko tabianchi.

Mafuriko.


 NA BETTY KANGONGA

“Nimepoteza ardhi zaidi ya nusu heka, sina makazi ya kudumu na hivi sasa nipo na familia yangu ya watu watano tunajihifadhi katika chumba kimoja kilichopo katika eneo jirani karibu na ilipobomoka nyumba yangu,”


Hii ni kauli ya Juma Mpasu Mkazi wa kijiji cha Kisala, Turiani, Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.

Mpasu anasema kuwa ilikuwa Januari mosi, mwaka 2020 wakati wakiwa wamepumzika na familia yake majira ya usiku ndipo walipokutana na zahama ya kupoteza makazi yao baada ya mafuriko kuwavamia wakiwa wamelala.

Anasema kuwa mafuriko hayo yalisababishwa na kuvunjika kwa kingo za mto wa Diwale ambao ulisababisha maji kuingia katika makazi ya wanakijiji  ambapo kaya zaidi ya 70 zilipoteza makazi.

“Hadi sasa tunaishi kwa mashaka kwa kuwa serikali ilituahidi kutusaidia lakini hakuna msaada tuliopata zaidi ya maisha kuwa magumu kwa kuwa tulipoteza vyakula, ardhi pamoja na mali nyingi,” anasema.

Naye muathirika mwingine wa mafuriko hayo George Jaccob anasema, kuwa hadi sasa hajajua hatima ya maisha yake na familia aliyonayo kwa kuwa amerudi katika umaskini na hana uwezo wa kujenga upya nyumba aliyokuwa anaishi na familia yake.

“Hili janga lilitukuta mwaka huu Januari moja wakati tukiwa tumelala hivyo tulilazimika kutafuta maeneo ya kujihifadhi na familia yangu,” anasema.

Anasema kuwa hana uwezo wa kurudi katika eneo hilo kujenga upya kwa kuwa ardhi imeharibika na hivyo inahitajika kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha kujenga katika eneo hilo.

Mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa changamoto katika zama hizi. Kupungua kwa misitu, mabadiliko ya utaratibu wa mvua na kuongezeka kwa kiwango cha maji ya bahari kunaweza kuongeza shinikizo la kiuchumi, kisiasa na kijamii na kuathiri maendeleo ya jamii.

Kutokana na mafuriko yaliyotokea katika Kijiji hicho cha Kisala miezi sita iliyopita ilileta athari kubwa ikiwa ni pamoja na jamii iliyoishi maeneo hayo kupoteza mali zao ikiwemo mifugo, vyakula pamoja na mazao.

Jaccob anasema, mazao yaliyokuwa mashambani ukiwemo mpunga, mahindi, alizeti vilisombwa na maji na baadhi kufukiwa na udongo hatua iliyowaathiri kiuchumi.

“Hatuna mazao, hatuna vyakula maana mahindi, mpunga na hata mbaazi tulizozitegemea zilisombwa na maji na sasa hata ardhi ambayo tulikuwa tunaitegemea kwa makazi nayo imethirika kutokana na mafuriko hayo hivyo hatuwezi hata kuiendeleza.” Anasema.

MWENYEKITI WA KIJIJI CHA KISALA

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Ramadhan Kilangilo anaeleza kuwa uharibifu wa mazingira na shughuli mbalimbali za kibinadamu kimekuwa chanzo cha kingo za mto huo kuvunjika na mafuriko kukikumba kijiji hicho mwishoni mwa mwaka 2019 na mwanzoni mwa Januari mwaka huu.

Anasema kuwa akiwa kiongozi wa kijiji aliweza kuwasilisha taarifa zote kwa uongozi wa kata pamoja na wilaya ili kuhakikisha wanakijiji walioathiriwa na mafuriko hayo wanapatiwa msaada na kuweza kurudi katika maisha ya kawaida.

“Taarifa za hasara, upotevu wa mali na nyumba zilizobomoka kwa nyumba tuliziwasilisha kwa uongozi wa wilaya lakini bado hatujapata muafaka wa suala hili kwa kuwa kaya zilizopata tatizo hilo zinaishi katika mazingira magumu.

Anasema kuwa kuna umuhimu wa wawekezaji waliopo katika eneo hilo kushirikiana na uongozi wa wilaya ili kuzuia tatizo kama hilo kujitokeza tena.

“Wilaya na wawekezaji waangalie namna ya kutoa elimu na kuhamasisha upandaji wa miti pamoja na kuzuia shughuli mbalimbali za kibinadamu zisifanyike jirani na kingo za mito,

…Hii itasaidia kuondokana na athari za mafuriko ambayo yamesababisha hasara kubwa kwa wanakijiji ambao wengine hadi sasa bado hawajaweza kurudi katika hali ya kawaida kwani wengi wao wamepewa hifadhi kwa ndugu zao.” Anasema.

KAULI YA KAMANDA

Kwa mujibu wa taarifa iliyoandikwa katika tovuti ya mkoa wa Morogoro Februari 3, mwaka huu ikimnukuu Kamanda wa Polisi Mkoani humo Wilbroad Mutafungwa ilieleza kuwa mtu mmoja mwenye umri wa miaka 12 ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja amepoteza maisha na wengine wawili hawajulikani walipo baada ya nyumba zao kusombwa na maji  kutokana na mvua zilizonyesha katika Mji mdogo wa Turiani wilayani Mvomero Mkoani Morogoro.

RC SANARE

Pia katika tovuti hiyo ilimnukuu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ambaye alilitaka jeshi la  Polisi Mkoani humo kuhakikisha linawaondoa wakazi wote ambao nyumba zao zipo katika maeneo ya bondeni ambayo ni hatarishi ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mvua.

Sanare anawataka wananchi kuwa na tabia ya kuheshimu maelekezo na miongozo inayotolewa na viongozi ikiwemo kuwataka kuhama mara moja katika maeneo ya mabondeni ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Mkoani humo.

KAULI YA ALIYEKUWA DC MVOMERO

Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro juu ya madhara yaliyosababishwa na mafuriko hayo kupitia tovuti hiyo ya mkoa, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mwl. Mohammed Utali anasema nyumba kadhaa zimeathirika katika maeneo mbalimbali Wilayani humo kutokana na mafuriko hayo huku jitihada zikiendelea kuwahamisha wananchi ambao nyumba zao zipo hatarini.

Akifafanua zaidi, juu ya athari za Mvua hizo, Utali anasema Kijiji cha Kisala nyumba 185 zilizungukwa na maji huku nyumba 32 zikibomoka, Kijiji cha Manyinga nyumba 95 zilizungukwa na maji na 19 zimebomoka, Kijiji cha Lusanga nyumba 83 zilibomoka na Madizini nyumba 3 zimebomoka kutokana na mafuriko hayo.

MRADI WA TURP

Aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) George Simbachawene aliwahi kukutana na kikao na ujumbe kutoka Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) kujadili kuhusu Mradi wa Tanzania Urban Resilience Programme (TURP) unaotekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) ambao umelenga kuzisaidia Halmashauri na Serikali Kuu katika kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.  

Mradi huu ukitekelezwa utaleta manufaa makubwa katika Jiji la Dar es Salaam ambapo utaokoa maeneo yaliyo hatari kwa mafuriko na kuyafanya salama kwa maendeleo ya jiji.

Hata hivyo madhara ya mabadiliko ya tabia nchi ni dhahiri katika jamii zetu. Miundombinu zikiwemo barabara zinaharibika na hivyo serikali inaingia gharama kubwa kutengeneza.

Mazao mashambani yanaharibika, magonjwa ya mlipuko yanaweka afya zetu hatarini huku wanawake na watoto wakiwa waathirika wakubwa.

HAKIARDHI

Taasisi ya Utafiti na Utetezi wa Masuala ya Ardhi (HakiArdhi) imekuwa mdau mkuu wa kutoa elimu kuhusiana na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

HakiArdhi katika baadhi ya Wilaya ilizopata kufikia imekuwa ikiwataka wananchi kuhakikisha wanapanda miti kwa wingi, kuepuka kukata miti hovyo na kuharibu vyanzo vya maji. Vilevile shughuli za viwandani na miradi mikubwa ya uzalishaji kwa ujumla izingatie utunzaji wa mazingira.

No comments:

Post a Comment

Pages