HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 04, 2020

MAHAKAMA KONDOA YAMALIZA MASHAURI 184 KATI YA JANUARI NA JULAI


Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya Kondoa akitoa ufafanuzi juu ya maboresho ya miundombinu ya Mahakama yalivyorahisisha utoaji haki kwa wakati. Picha na MAHAKAMA na Idara ya Habari-MAELEZO
Jengo Jipya la Mahakama ya Wilaya ya Kondoa
linalotumika kutoa huduma za kimahakama.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kondoa akitoa rai kwa wananchi wa Kondoa kuitumia Mahakama ili kusuluhisha migogoro yao.

Na Innocent Kansha – Mahakama Kondoa

Mahakama ya wilaya ya Kondoa imesikiliza na kumaliza mashauri ya jinai na madai 184 kati ya mashauri 262 yaliyokuwepo katika Mahakama za wilaya za
Kondoa na Chemba.

Akizungumza na Maafisa Habari wa Mahakama ya Tanzania, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Kondoa Mhe. Francis Robert Mhina alisema mashauri hayo yamesikilizwa na kumalizika kati ya mwezi Januari na Julai, mwaka huu.

“Mashauri yaliyobaki mwezi Desemba 2019 yalikuwa ni 152, yaliyosajiliwa kati ya Januari na Julai mwaka huu ni mashauri 110, tumesikiliza na kumaliza jumla ya mashauri 184 na kubakiwa na mashauri 78”, alifafanua Mhe. Mhina.

Kwa mujibu wa Hakimu Mfawidhi huyo, asilimia kubwa ya mashauri yanayofunguliwa kwenye Mahakama hizo ni yale yanayohusu ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji, pamoja na mauaji, kujeruhi na mashauri ya kukutwa na nyara za wanyama pori.

Alisema mashauri yanayohusu nyara za taifa hasa wanyama pori yanatokana na uwepo wa mapori tengefu ya hifadhi za Swaga swaga na Mkungunero.

“Wananchi wengi wanaoishi kando kando ya hifadhi hizi wamekuwa wakiendesha shughuli zao mbalimbali za kiuchumi bila kuzingatia mipaka na kujikuta wanakinzana na sheria za hifadhi kama kulima ndani ya hifadhi, kuvua samaki, kuchoma mkaa, kukutwa na nyara za Taifa na kuwinda wanyama pasipo kuwa na vibali halali”, alisema Mhe. Mhina. Mhe. Mhina alisema asilimia kubwa ya mashauri ya mauaji yanatokea Wilaya ya Chemba.

Mahakama ya Wilaya ya Kondoa pia inahudumia Wilaya Chemba kwa sasa.

Kuhusu matumizi ya Tehama katika Mahakama ya wilaya ya Kondoa, Mhe. Mhina amesema yamesaidia kwa kikubwa kurahisisha suala la upatikanaji wa haki kwa wakati.

Aliongeza kuwa mfumo wa kusajili mashauri (JSDS II) unatumiwa vizuri na watumishi katika kutunza kumbukumbu za kila siku za mashauri baada ya kufungiwa mkongo wa Taifa wa mawasiliano.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Kondoa Bw. Andrea Ng’hwani alisema Serikali Wilayani humo imeyapokea maboresho ya miundombinu ya Mahakama kwa furaha kwani yametatua changamoto na kero za wananchi wa Kondoa kwa kiasi kikubwa.

“Nawakumbusha wananchi kuwa nchi hii inaongozwa kwa misingi ya kisheria na hakuna mazingira yoyote yanayoruhusu mtu kujichukulia sheria mikononi ndiyo maana kuna Jeshi la Polisi na Mahakama ili kutatua kero zao” alisisitiza Katibu
Tawala.

“Kero za wananchi zimepungua sana na sasa hatupokei malalamiko yanayohusu Mahakama kiutendanji na mambo mengine yanayohusu uelewa wa taratibu za kimahakama tumekuwa mstari wa mbele kuyatolea ufafanuzi wa kuwaelekeza sehemu sahihi ya kutatua na kupata ufafanuzi”, alisema Katibu Tawala.

Bw. Ng’hwani alisema wananchi wanapaswa kupeleka migogoro yao mahakamani ili iweze kutatuliwa kisheria na pale wanapoona hawajaridhika na maamuzi, wakate rufaa Mahakama ya juu zaidi kupata haki ili Amani na utulivu vizidi
kuimarika.

No comments:

Post a Comment

Pages