Viongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT wakipata maelezo mafupi kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa Shirika la Reli la Tazara.
Na Janeth Jovin
CHUO Cha Taifa cha Usafirishaji nchini (NIT), kimeliomba Shirika la reli la TAZARA kutoa nafasi kwa vijana wenye taaluma mbalimbali kufanya kazi katika Shirika hilo kwa kujitolea ili kuweza kutatua changamoto zilizopo.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo cha NIT Profesa Zacharia Mganilwa wakati wa ziara ya viongozi wa chuo hicho katika shirika hilo la Tazara kwa lengo la kuona na kujifunza jinsi linavyofanya kazi.
Amesema NIT pamoja na vyuo vingine utoa vijana wengi wataalamu ambao wengi wao ukosa ajira mara wanapohitimu hivyo anaiomba Tazara kutoa nafasi kwa vijana hao kufanya kazi kwa kujitolea na hatimaye watatue changamoto zinazolikabili Shirika hilo.
"Tunao vijana wataalum wa mainjini mbalimbali wanaomaliza chuoni pale, wanaosoma masuala ya Usafirishaji ikiwamo wa reli pamoja wataalamu wa masuala ya fedha katika mashirika ya Usafirishaji, vijana hawa wakipewa fursa ya kujitolea ndani ya miezi sita au mwaka wanaweza kuwa na mawazo mapya yatakayolisaidia Shirika hili la Tazara
"Shirika hili ni kampuni ya kibiashara lakini sasa hivi limeshindwa kufanya biashara na hawawezi tena kulipana mishahara sasa hapa panatakiwa kuwepo kwa mawazo mapya ili hali hiyo iweze kukomaa," amesema Profesa Mganilwa
Hata hivyo Profesa Mganilwa ameitaka Tazara kupeleka changamoto zao katika chuo hicho ili ziweze kufanyiwa utafiti na kupatikana kwa ufumbuzi na hatimaye shirika hilo kufikia malengo yanayotarajiwa na Serikali.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa chuo hicho, Bavo Nichomba amesema kuwa lengo kubwa la kutembelea shirika hilo ni kuangalia ni maeneo gani wanaweza kushirikiana na Tazara ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali zilizopo.
Amesema wamekuja kutembelea shirika hilo pia kuangalia ninkea jinsi gani wanaweza kushiriki katika kupata mainjinia watakaoweza kutatua matatizo yaliyopo Tazara.
"Katika maongezi ya awali tumeona kwamba Tazara wanauhitaji wa wataalamu kama Mainjinia na matekinishani lakini kikubwa tulikuwa hatuongei hivyo ujio huu leo unakwenda kufungua mashirikiano na wataalamu watapatikana," amesema.
Amesema NIT watachangamkia fursa ya kupeleka wataalamu TAZARA kwani kwa mwaka zaidi ya wanafunzi 1500 wanahitimu masomo yao huku wengine wakikosa kazi.
Kaimu Mkurugenzi wa TAZARA, Geoffrey Sengo amesema kuwa ujio wa bodi ya NIT itakuwa sehemu moja wapo ya kuiboresha Tazara kwani kumekuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazoikumba ikiwemo upungufu wa wataalumu kama inavyotakiwa
TAZARA (Tanzania Zambia Railway) ni shirika ya reli ya pamoja ya nchi za Zambia na Tanzania Inaunganisha bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania na kituo cha New Kapiri Mposhi iliyopo kwenye njia ya reli kati ya Lusaka na Kitwe kwenye ukanda wa shaba wa Zambia
No comments:
Post a Comment