HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 27, 2020

TCRA yaifungia Clouds Televisheni na Redio kwa siku Saba

Na Janeth Jovin

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesitisha leseni ya utoaji huduma za utangazaji wa kituo cha Clouds Televisheni na Redio kwa siku saba kuanzia Agosti 28 hadi Septemba 3, mwaka huu.

Aidha TCRA imekitaka kituo hicho kuanzia muda wa agizo hilo mpaka mwisho wa siku la leo kuahirisha matangazo yote na kutumia muda wote uliobakia wa siku ya leo kuomba radhi kwa umma wa Tanzania kwa kukiuka Kanuni za Utangazaji kupitia kipindi cha Clouds 360 na Clouds Entertainment.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba amesema iwapo Clouds Televisheni na Redio watashindwa, itakataa au kukaidi uamuzi uamuzi huo, hatua zaidi za kisheria na kiudhibiti zitachukuliwa dhidi yao.

Akizungumzia sababu za kukifungia kituo hicho, Kilaba amesema vituo hivyo vimekiuka kanuni za utangazaji na kanuni ndogo za utangazaji wa masuala ya Uchaguzi za mwaka 2015 kupitia vipindi hivyo viwili vinavyorushwa katika kituo hicho.

Kilaba amesema Agosti 26, mwaka huu kati ya saa moja hadi saa nne asubuhi kupitia vipindi  vya Clouds 360 na cha Power Breakfast cha Televisheni na Redio, vilirusha takwimu za wagombea wa Ubunge waliopota bila kupingwa na kudai kuwa taarifa hiyo haikudhibitishwa na Tume ya Uchaguzi hivyo kukosa mizania.

"Katika vipindi hivyo mtoa huduma alikiuka kanuni mbalimbali zikiwemo kanuni za utangazaji na za mwenendo wa utangazaji wakati wa uchaguzi za mwaka 2015," amesema Kilaba

Hata hivyo, Kilaba ametoa wito kwa vyombo vya utangazaji vyote kuzingatia kanuni ndogo za utangazaji wa masuala ya uchaguzi na zile za NEC ili ziwawezeshe kutangaza masuala ya uchaguzi kwa weledi mkubwa na hivyo kudumisha amani ya nchi.

"Natoa wito kwa watumiaji wote wa mitandao ikiwamo ile ya kijamii hususani wasimamizi wa makundi mbalimbali ya mtandao hiyo na wanachama wa vyama vyote kuzingatia matakwa ya kisheria kuhusu masuala ya uchaguzi tunapohusisha mitandao ya Mawasiliano," amesema

Aidha Kilaba aliongeza kuwa Julai mwaka huu ilikutana na vituo vya utangazaji kwa ajili ya kutoa elimu na kukumbushana umuhimu wa kuzifahamu kanuni ndogo za utangazaji wa masuala ya Uchaguzi.

"Elimu hii ililenga kuhakikisha kuwa watangazaji na waandishi wote wana elimu sahihi ya kanuni hizi na kwamba watatangaza habari zote za uchaguzi kwa weledi mkubwa," amesema

Amesema wamesikitishwa kuona kuwa tayari ukiukwaji wa kanuni hizo umeanza kujitokeza katika vyombo vya habari.

No comments:

Post a Comment

Pages