Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) Godfrey Mngereza (katika) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Na Janeth Jovin
SHIRIKISHO la Wanamuziki Tanzania limetoa onyo na kuwapiga marufuku wasanii ambao sio walezi wala marais wa Chama cha Wanamuziki wa Injili nchini (Chamwita) kujiita vyeo hivyo.
Aidha Shirikisho hilo limewataka wasanii wote waliochaguliwa na vyama mbalimbali vya siasa kushiriki katika kampeni za uchaguzi mkuu, kuhakikisha wanafanya kazi zao za sanaa kwa kufuata maadili, sheria na kanuni za nchi na za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Rai hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Rais wa Shirikisho hilo, Addo November wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).
November amesema Shirikisho hilo linatoa onyo na kupiga marufuku kwa watu hao kujiita vyeo hivyo kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria na taratibu za chama hicho na watakaoendelea watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
"Kabla hatujaanza kuwachukulia hatua hizo za kinidhamu kwa wale wanaofanya hayo mambo, tumeanza kwa upendo kuwaonya na kuwaeleza kuwa mtu kujipa jina ambalo sio lako ni kosa la jinai na kitaaluma mimi ni wakili tutawashughulikia wanaokiuka utaratibu," amesema November
Hata November amesema anavipongeza vyama mbalimbali vya siasa ambavyo vimewaamini wasanii na kuwapa nafasi za kugombea Ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
"Tunaviomba vyama vya siasa kuendelea kuwaamini wasanii na hawa waliopata nafasi wakkpita basi wateuliwe kuwa mawaziri ili waweze kushughulikia kwa ukamilifu matatizo ya wasanii wenzao," amesema
Naye Katibu Mtendaji wa Basata Godfrey Mngereza amewaonya na kuwahasa wasanii wa muziki na filamu kuhakikisha kipindi chote cha uchaguzi kuacha malumbano bali washiriki katika kampeni kwa amani na kuzingatia weledi wakati wote wanapofanya shughuli zao za kisanaa.
"Tunakwenda kwenye kampeni wasanii wakumbuke wao ni watanzania hivyo wanajukumu kubwa la kulinda na kuitunza amani ya nchi yetu," amesema.
No comments:
Post a Comment