Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (Organ Troika) ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imekutana na kujadili namna ya kurejesha hali ya amani, ulinzi na usalama nchini DRC ili nchi hiyo iweze kupiga hatua katika maendeleo.
Akiongea katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao (Video Conferencing) na kujadili masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama nchini Kongo DRC, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amesema kuwa mkutano huo ulizihusisha nchi za utatu wa siasa ulinzi na usalama pamoja na nchi tatu ambazo zinazotoa askari wa kikosi maalumu kinachoshughulikia masuala ya ulinzi na usalama katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (Force Intervention Brigade).
“Tangu mwaka jana SADC na Umoja wa Mataifa tumekuwa katika mazungumzo ya jinsi ya kuimarisha kikosi hicho pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama nchini DRC hasa upande wa Mashariki mbapo umekuwa ukipambana na vikundi vyenye misimamo mikali na kuifanya DRC kukosa utulivu na amani,” Amesema Prof. Kabudi
Waziri ameongeza kuwa Tanzania kwa muda mrefu ikiwa ni sehemu ya SADC imepeleka askari wake upande wa mashariki mwa DRC, ambapo pamoja na mambo mengine mkutano wa leo ulikuwa ni nwebdelezo wa mazungumzo kati ya Tanzania na nchi nyingine za SADC ili kuwa na msimamo wa pamoja katika mazungumzo yake yanayoendelea na Umoja wa Mataifa (UN) kwa lengo moja la kusisitiza suala la kurejesha hali ya amani nchini Kongo hasa Mashariki mwa Kongo.
“Tunashukuru kusema kwamba DRC ambayo ni sehemu ya SADC msimamo wake umekuwa ni ule ule unaofanana na wa nchi za SADC, pili Nchi za SADC na umoja wa Mataifa tumeazimia jambo linalofanana kuhakikisha kwamba Kongo inamaliza migogoro yake, Kongo inarejea kuwa na Amani na utulivu na Kongo inakuwa na mshikamano ili wananchi wa Kongo waweze kupiga hatua kubwa katika maendeleo,” Amesema Waziri Kabudi.
Kongo imekuwa ni muhanga wa machafuko na vita kwa muda mrefu ni imani ya Tanzania na nchi za SADC kwamba wakati umefika sasa kwa Kongo na hasa kwa Mashariki ya Kongo kupewa nafasi yake ya utulivu na mshikamano ili iweze kupiga hatua kubwa ya maendeleo.
Mkutano umehudhuriwa na Jamhuri ya Afrika Kusini, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Malawi, Zimbabwe, Botswana, Zambia, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof.
Palamagamba John Kabudi (katikati) akiwa na Waziri wa Ulinzi Mhe.Dkt.
Husseni Mwinyi (kushoto) pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Brigadia Generali, Balozi Wilbert
Ibuge (kulia kwa Prof. Kabudi). Wengine ni Katibu Mkuu
Wizara ya Ulinzi Dkt. Faraji Mnyepe (wa kwanza kushoto) pamoja na
Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Mkutano wa Asasi ya
Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (Organ Troika) ya Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa
njia ya mtandao (Video Conference).
Mkutano ukiendelea.
No comments:
Post a Comment