Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Shinyanga
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga jana tarehe 10 Agosti 2020 amefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora na Wilaya ya Iramba Mkoani Singida ambapo amekagua na kuridhishwa na hali ya ununuzi wa msimu wa Pamba kwa mwaka 2020/2021.
Waziri Hasunga amesema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kuhakikisha kuwa wakulima wanaondoka katika dhana ya kilimo cha kujikimu badala yake kuwa kilimo cha kibiashara.
Amesema kuwa ili kusimamia jambo hilo kwa vitendo tayari serikali imeanza kutoa elimu kwa wakulima kupitia Maafisa ugani na wataalamu mbalimbali wa kilimo kuhusu namna bora ya kuzingatia mbinu bora za kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji.
Katika ziara hiyo akiwa katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora Waziri Hasunga amewahakikishia wakulima kuwa serikali inasimamia kwa weledi mkubwa sekta ya kilimo ambacho ndicho muhimili mkubwa wa maendeleo ya wananchi na ikichangia kwa asilimia kubwa uchumi wa nchi.
Hasunga amesema kuwa ili kuboresha kilimo na maisha ya wakulima ni dhahiri kuwa serikali lazima ifanye mazungumzo na Benki mbalimba ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Mfuko wa Pembejeo za Kilimo AGITF kwa ajili ya kupunguza riba na masharti magumu kwa wakulima ili waweze kukopa kwa ajili ya kuboresha kilimo chao.
Akiwa katika ziara ya Kikazi Wilaya ya Iramba mkoani Singida Waziri Hasunga ameipongeza kampuni ya ununuzi wa Pamba ya Biosustain kwa kuhakikisha kuwa imemaliza madeni yote ya wakulima wa Pamba kwa msimu wa mwaka 2018/2019 mkoa wa Singida.
Amesema kuwa pamoja na changamoto iliyojitokeza ya Ugonjwa wa Mapafu-COVID 19 lakini kampuni hiyo imehakikisha kuwa wakulima wote wanalipwa fedha zao kwa wakati.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga jana tarehe 10 Agosti 2020 amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku mbili katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Tabora na Singida.
No comments:
Post a Comment