HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 01, 2020

ELIMU YA SHERIA ZA UMILIKI WA ARDHI ZAWAAMSHA WANAWAKE MOROGORO

Baadhi ya Wanawake na Vijana zaidi ya 60 kutoka kata za Lundi, Bwakila Chini, Mngazi na Kisaki Kituoni katika halmashauri ya Wilaya ya Morogoro wakiwa katika mafunzo ya Sheria za Ardhi, utambuzi wa fursa na kuzitumia katika jamii zao. Mafunzo hayo yameandaliwa na Kituo cha Wasaidizi wa Sheria Morogoro.  (Picha na MPLC).

 

NA MWANDISHI WETU


WATU wengi wanamiliki ardhi kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo, lakini sio wengi wanaozifahamu sheria zinazofungamana na umiliki huo wa ardhi. 

Hali hii imesababisha migogoro mingi ambayo ina changamoto zake katika kuitatua.

Mkazi wa Kata ya Bwakila Chini, Tarafa ya Bwakila, Wilaya ya Morogoro Kusini, Mkoani Morogoro Rehema Hongo, anasema kuwa hakutarajia kumiliki ardhi na kupata hati za kimila, kutokana na mfumo dume uliokithiri katika eneo hilo.

Anasema kuwa, awali kabla ya kupata elimu ya sheria ya umiliki wa ardhi, mwanamke alikuwa hathaminiwi katika jamii hiyo kwa kuwa alionekana hana mchango katika kaya.

“Kipindi hicho ukiachika katika ndoa yako hupewi chochote, kwani mali zote ulizochuma na mumeo zinachukuliwa na huyo mwanaume, unaondoka na nguo zako tu,” anasema.

Hongo anasema kuwa, baada ya wasaidizi wa kisheria kutoka mkoani Morogoro kufika katika eneo hilo na kutoa elimu kuhusiana na sheria ya umiliki wa ardhi, kwa sasa hali imebadilika.

Anasema kuwa, elimu hiyo imewasaidia wanawake kusimama imara kutetea haki zao na hadi sasa wapo wanaomiliki ardhi na kupewa hati za kimila.

“Kwa kweli hadi hivi sasa wanawake wameamka, kila mmoja anamiliki ardhi na hata wale wanaume waliokuwa wanawakandamiza wanawake nao wamebadilika kifikra, baada ya kupata elimu,” anasema.

Mama huyo anaongeza kuwa, mbali ya kupata elimu hiyo, pia alichaguliwa na asasi hiyo kusambaza elimu kwa jamii inayomzunguka kuhusiana umuhimu wa wanawake kumiliki ardhi.

Anabainisha kuwa, hadi sasa ametoa elimu kwa wanawake zaidi ya 160, huku wanawake 50 walipata haki zao kwa kurejeshewa ardhi walizoporwa, ambapo wengine kwa sasa wanasubiri kupatiwa hati za kimila.

Hongo anawashukuru wasaidizi wa kisheria waliowawezesha kuamka na kusimama imara na kupigania haki zao.

Naye Fatuma Salehe, ambaye ni mkazi wa Bwakila Chini, mkoani humo, ni miongoni mwa wanawake ambao wamehamasika kumiliki ardhi ili kuepuka migogoro ambayo inaweza kutokea.

Fatuma mwenye umri wa miaka 57, ambaye ameolewa miaka 30 iliyopita na Kassim Khasira (65), katika maisha yao wamebahatika kupata watoto sita (6), wa kike watano na wa kiume mmoja. 

Shughuli kubwa wanayofanya ili kujiingizia kipato ni kilimo, mbako mama huyo anasema kuwa, alipata elimu kuhusiana na umiliki wa ardhi ambapo yeye na mumewe walihudhuria moja ya semina iliyofanyika katika kijiji chao kupitia mkutano wa kijiji.

Anasema kuwa, elimu ya umiliki wa ardhi waliopewa na wasaidizi wa kisheria ilieleweka vema, hivyo yeye pamoja na mkewe waliamua kufanya maamuzi.

Mama huyo anasema kuwa, mumewe alichukua hatua ya kumuongoza kwa wahamasishaji kujua utaratibu wa kupata fomu ili waombe hati miliki ya eneo lao ambalo lina ukubwa wa hekari 4, lakini aliomba usiwe umiliki wa pamoja, badala yake akaomba eneo lote amiliki mkewe.

Sababu ya kummilikisha eneo mkewe ni kuwa miaka saba iliyopita Kassim alifiwa na kaka yake, ndugu zake walimnyang’anya mke wa marehemu mali zote ambazo walizitafuta kwa pamoja, ikiwemo shamba lenye ukubwa wa hekari 1 na nyumba.

Kassimu anasema hakufurahishwa na kitendo hicho, alikiita kuwa ni cha kikatili na cha kumnyanyasa mwanamke, hivyo elimu aliyoipata ya mirathi na masuala ya umiliki mali, kutoka kwa wahamasishaji wa masuala ya ardhi, ndiyo iliyosababisha kuona umuhimu zaidi wa kummilikisha mkewe eneo hilo.

Anasema kuwa kwa sasa mkewe amepata hatimiliki kwa msaada wa wasaidizi wa kisheria ambayo itamsaidia asiingie kwenye mgogoro wa ardhi na familia au watu waliopakana naye.

Naye Asha Duichile, ambaye ni mkulima anayefanya shughuli za kilimo eneo la Kisaki, anamiliki eneo la ukubwa wa hekari 10 bila kubugudhiwa na mtu yeyote kwa muda mrefu.

Anasema Mwaka 2016 eneo lake lilivamiwa na mfugaji ambapo alipigania haki yake kwa kupeleka suala hilo katika Baraza la Kijiji la usuluhishi wa migogoro ya ardhi ambalo lipo katika kijiji cha Kisaki Kituoni.

Baraza hilo lilimpa haki Asha baada ya kutembelea eneo lenye mgogoro na kuona vielelezo zikiwemo risiti za umiliki inayolipiwa katika Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Kisaki na mmiliki huyo.

Anasema kuwa mfugaji huyo hakuridhika na maamuzi hayo ndipo alipoamua kupeleka kesi hiyo Baraza la Usuluhishi Kata ambapo alipata haki.

Hata hivyo, jambo hilo lilimsababisha Asha kukata rufaa na kwenda Baraza la Ardhi na Nyumba wilaya Morogoro, ambapo baada ya kusikiliza mgogoro huo walimpatia haki yake.

Baraza hilo lilimtambua mwanamke huyo kuwa mmiliki halali wa eneo lenye mgogoro, hivyo mfugaji hakutakiwa kujihusisha na kitu chochote katika shamba hilo.

“Haki yangu imepatikana kwa kutumia sheria bila kupigana, hivyo nawashukuru viongozi na mahakama kwa kusimamia na kunisaidia kupata nilichokuwa napigania, haki imetendeka namshukuru Mungu,” anasema.

Hali hiyo inaonesha mwamko wa wanawake katika kupigania haki yao ya kumiliki ardhi na kuilinda ardhi, umeongezeka ndani ya jamii hivyo wanawake wana nafasi ya kumiliki mali kama wanaume.

Anasema hivi sasa ameongeza ujasiri wa kusimamia ardhi yake baada ya kuhudhuria mikutano ya kijiji na kupata elimu kutoka kwa wahamasishaji wa masuala ya ardhi waliokuwa wakihamasisha umuhimu wa kuwa na hati miliki ya kimila.

Asha anasema akipatiwa hati miliki kutamuepusha na migogoro ambayo inaweza kuja kujitokeza hapo baadae.

KAULI YA OFISA UFUATILIAJI

Ofisa Ufuatiliaji na Tathimini wa Morogoro Paralegal Center, Sakina Nyumayo, anasema kuwa kituo hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mkoa huo ambao walikuwa wakikabiliwa na ukosefu wa uelewa wa masuala ya ardhi.

Nyumayo anasema kuwa, hadi sasa kituo hicho kimeweza kuwafikia wananchi zaidi ya 1,500 wa Wilaya ya Morogoro Vijijini.

“Kati ya hao, wanawake waliopata elimu ya masuala ya ardhi ni 893 na wanaume 654 na hadi sasa walioandikishwa kwa ajili ya kupata hati za kimila ni wananchi 283,” anaeleza

Ofisa huyo anasema kuwa takwimu hizo ni za kuanzia Januari mwaka huu hadi Agosti.

MIRADI YA KULINDA ARDHI

Uwepo wa Mradi wa Kulinda Haki za Ardhi kwa Wanawake na Wajasiariamali Wadogo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, umeweza kupunguza migogoro mbalimbali ikiwemo Ardhi  iliyokuwa inachangia wananchi kushindwa kufanya shughuli za maendeleo na kutumia muda mwingi kutatua migogoro.

KAULI YA OFISA ARDHI

Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Herman Ambala, anasema kuwa Serikali hivi sasa imejipanga kuhakikisha inamfikia kila mwananchi mwenye kuhitaji kumiliki ardhi kisheria na kuondokana na umiliki wa kiholela.

“Lengo la Serikali ni kuona migogoro ya ardhi inakwisha kabisa, wananchi wanaishi kwa usalama na kuelewana, hivyo yeyote mwenye kumiliki kipande cha ardhi awatumie maofisa ardhi kupima na kupatiwa hati miliki ya kimila ili kuondoa migogoro ya ardhi,” anasema.

No comments:

Post a Comment

Pages