HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 10, 2020

ICVA yazitaka NGOs za msaada wakibinamu kushirikiana


Katibu Mkuu wa Tanzania Refugee and Migration Network (TAREMINET), ABEID Kasaizi akielezea warsha ya siku moja ya wadau wa msaada wa kibinadamu iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
 
Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Khoti Kamanga akifafanua jambo kuhusu dhana ya ushirikiano katika mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs).
 
 
 
NA SULEIMAN MSUYA

MASHIRIKA yasiyo ya Kiserikali nchini Tanzania (NGOs) yanayojihusisha na kutoa msaada wa kibinadamu yameshauriwa kushirikiana ili yaweze kufikia malengo waliyojiwekea.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Program wa  International Councils of Volunteers Agency (ICVA), Michael Hyden wakati akitoa mada kwenye warsha ya siku moja kuhusu dhana nzima ya ushirikiano kwa wadau wa masuala ya msaada wa kibinadamu jijini Dar es Salaam.

Warsha hiyo iliandaliwa na Mtandao wa Mashirika yanayoshughulika na kutoa msaada wa kibinadamu la Tanzania Refugee and Migration Network (TAREMINET).

Hyden alisema popote kwenye mafanikio msingi mkubwa ni ushirikiano wa wadau husika na kwamba dhana ya kila mtu kujipendelea itakuwa changamoto.

Mkurugenzi huyo alisema umoja na ushirikiano utaweza kuishawishi Serikali, Mashirika yaliyopo chini ya Umoja wa Mataifa (UN) na mengine mengi kuwasaidia kutimiza malengo ya msaada wa kibinadamu.

"Niwe muwazi kuwa iwapo mnataka kufanikisha malengo yenu mnatakiwa kuwa pamoja ili muimbe pamoja jambo ambalo litawarahisishia kufikia wadau wote katika muhimu na sisi tutasaidia ambapo mnakwama kama ni masuala ya kisheria iwapo kuna changamoto hiyo," alisema.

Alisema nchi ambazo NGOs zinafanya kazi pamoja mafanikio ni mengi tofauti na zile ambazo zinafanya kila mtu mwenyewe.

Alisema ICVA wanapromoti kanuni za msaada wa kibinadamu ziweze kutekelezwa katika nchi husika kwa kuwa wamesaini mikataba mbalimbali ya Kimataifa.

Mkurugenzi huyo alisema ushirikiano huo utafanikishwa na uongozi bora, usimamizi, uratubu, ushirikishwaji, uwazi na mengine muhimu kwenye taasisi.

Mwenyekiti wa TAREMINET, Janemary Ruhundwa warsha hiyo imejikita kujadili dhana nzima ya ushirikiano katika ngazi ya NGOs za ndani ya nchi katika utoaji wa msaada wa kibinadamu nchini.

Alisema kumekuwepo na mjadala mpana duniani tangu mwaka 1990 ila dhana hiyo haijatekelezwa kisawasawa na kuonekana kwa jamii husika.

"Warsha hii itatupa muongozo wa nini kifanyike hapa nchini kutekeleza dhana ya ushirikiano katika eneo la msadaa wa kibinadamu kwani makubaliano yalifikiwa bado tupo nyuma kiutekelezaji," alisema.

Ruhundwa alisema bado NGOs nyingi zinaamini katika kusubiri mashirika ya kimataifa kusambaza dhana hiyo jambo ambalo linawachelewesha.

Katibu Mkuu wa TAREMINET, Abeid Kasaizi alisema mtandao huo ni muunganiko wa mashirika 12 ya msaada wa kibinadamu Tanzania.

Alisema warsha ya leo imelenga kuona ni namna gani wanaweza kutumia nguvu ya pamoja katika kutatua majanga yanayopata nchi kwa pamija.

"Kuna majanga kama mafuriko, tetemeko na mengine ambayo yanahitaji NGOs zinazojihusisha na msaada wa kibinadamu kutoa msaada bila kubaguana.

" Sisi tumeamua kupigania msaada wa kibinadamu kwa miaka mingi hivyo tunapswa kuwa pamoja kupitia jukwaa la TAREMINET ili tusisambaze rasilimali zinazopatikana na wahanga watapata kilichobora zaidi,"alisema.

Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Sheria na Kituo cha Wakimbizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Khoti Kamanga alisema tatizo la wakimbizi ni kubwa duniani na njia sahihi ya kukabiliana nayo ni wadau wote kushirikishwa.

Prof.Kamanga alisema dhana ya ushirikiano inataka kuwe na lugha moja shirikishi na sio watu fulani kufanya maamuzi kwa niaba ya kundi fulani.

Alitolea mfano janga la wakimbizi pamoja na kwamba asilimia 83 wanatoka nchi maskini lakini sera kuhusu kundi hilo zinatungwa na nchi tajiri jambo ambalo sio sahihi.

"Pia mgawanyo wa fedha unafanyika huko katika nchi tajiri jambo ambalo halileti dhana ya ushirikiano inakosekana kwa nchi maskini ambazo ndizo zenye tatizo," alisema.

Mhadhiri huyo alisema changamoto nyingine ambayo inaonekana kutokana na kukosekana kwa ushirikiano ni nchi maskini kushindwa kufanya utafiti wa kina wa hali halisi ya tatizo.

Alisema ni wakati muafaka kwa mashirika ya kimataifa na wadau wa maendeleo kuwezesha wataalam ili wafanye utafiti wa hali halisi ya wakimbizi nchini na wahitaji wa msaada wa kibinadamu.


No comments:

Post a Comment

Pages