Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo, akifungua maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam Dar
NA JANETH JOVIN
SERIKALI imevitaka vyuo vyote vikuu nchini kuhakikisha vinatafuta namna ya kupanua udahili wa wanafunzi ili kuweza kumudu idadi ya wahitimu watakaomaliza elimu ya bila malipo ngazi ya msingi na Sekondari kwa siku zijazo.
Imesema mpaka sasa kiasi cha Sh. Trilioni 1.03 kimekwishatolewa kugharamia elimu bila malipo ngazi ya elimu msingi na kuongeza kuwa hali hiyo imeleta ongozeko kubwa la wanafunzi ngazi ya msingi kutoka Milioni 8.3 mwaka 2015 hadi kufikia Milioni 10.9 mwaka huu.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 2,2020 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo wakati akifungua maonesho ya 15 ya vyuo vikuu nchini yanayoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU)
Amesema idadi pia ya wanafunzi wa kitado cha kwanza hadi cha nne imeongezeka kutoka Milioni 1.6, 2015 hadi kufikia Milioni 2.2 mwaka 2019, huku kidato cha sita wakiwa 153,000.
Akiwilapo amesema kutokana na idadi hiyo wanatambua kuwa kutakuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi watakaomaliza elimu ya Sekondari na kuingia vyuo vikuu hivyo vyuo vinapaswa kuangalia namna ambavyo vitapanua udahili ili kuweza kumudu idadi hiyo.
"Ni wazi kwamba katika miaka michache ijayo utoaji wa elimu bila ada utaathiri vyuo vikuu kwa sababu kutakuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliomaliza elimu ya Sekondari na wanahitaji kujiunga na vyuo, hivyo tunaviomba vyuo kupanua udahili wao ili wakati ukifika wa wanafunzi hao kujiunga kusitokee taharuki," amesema Akwilapo
Aidha imetoa wito kwa vyuo hivyo vikuu na taasisi za utafiti kujielekeza zaidi katika kufanya tafiti zenye lengo la kujenga msingi wa uchumi wa viwanda hususani ni utafiti wa teknolojia, bidhaa za viwandani, kilimo, mifugo, uvuvi, utalii, maliasili za misutu na madini.
Naye Mwenyekiti wa TCU, Profesa Mayunga Nkunya amesema tume hiyo imeendelea kuvishauri vyuo vikuu kutoa elimu na kuandaa mitaala inayoendana na vipaumbele vya maendeleo ya kitaifa, mahitaji ya wataalamu katika soko la kitaifa pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia ikiwamo mapinduzi wa viwanda.
Amesema tume hiyo imeimarisha pia mifumo yake ya utoaji elimu kwa umma na hivyo kuweza kuwafikia wadau wengi zaidi.
"Kutokana na kuimarisha mifumo hiyo kumekuwa na mwamko wa wadau wa elimu ya juu katika maeneo mbalimbali, pia kwa mara ya kwanza tume imeweza kusajili jumla ya kampuni 14 zinazohusika na udahili wa wanafunzi katika vyuo vikuu vya nje ambao wote hawa wamekidhi vigezo na taratibu zilizowekwa na tume
"Lengo la usajili huu ni kuwalinda watanzania wanaokwenda kusoma nje ya nchi dhidi ya mawakala wasio waaminifu wanaowapeleka kusoma katika vyuo vilivyo na programu za masomo zisizo kubalika," amesema
Hata hivyo amesema TCU itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia watanzania katika sekta hiyo ya elimu ya juu ili kuhakikisha wanapata elimu yenye kukidhi viwango vya ubora vya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TCU, Profsa Charles Kihampa amesema katika maonesho hayo jumla ya taasisi 67 zimeshiriki na kuongeza kuwa kati ya hizo 58 ni zile zinazotoa elimu ya juu.
No comments:
Post a Comment