MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea kusikiliza utetezi katika kesi ya kutoa maneno ya kuudhi dhidi ya Rais John Magufuli inayomkabili Mgombea wa Ubunge Jimbo la Kawe kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema), Halima Mdee, kwa sababu wakili wa mshtakiwa huyo hakuwepo mahakamani.
Kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuanza utetezi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba lakini imeshindwa kuendelea baada ya wakili wa Mdee, Peter Kibatala kutokuwepo Mahakamani.
Kutokana na sababu hiyo Hakimu Simba amehalisha kesi hiyo hadi Novemba 11 mwaka huu itapokuja tena kwa ajili ya kuanza utetezi.
Baada ya kauli hiyo, upande wa mashtaka uliowakilishwa na wakili wa serikali Grace Mwanga haukuwa na pingamizi lolote.
Katika kesi ya msingi Mdee anadaiwa kutoa maneno ya kuudhi dhidi ya Rais Magufuli.
Inadaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema, zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Mdee alitamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa, ‘anaongea hovyo, anatakiwa afungwe breki,’ kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kusababisha uvunjifu wa amani.
Mdee alifikishwa mahakamani hapo Julai 10,2017 na kushtakiwa kwa mashtaka ya uchochezi.
No comments:
Post a Comment