MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewaomba Watanzania wamchague mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu ni kiongozi ambaye anaimudu nafasi hiyo na ni kiongozi mwenye msimamo thabiti wa kuleta usawa kwa wananchi wote.
“Urais si kazi ya mchezo ya kumpa kila mtu, ni lazima tumtafute mtu aliyetulia. Hata kama kuna ndugu yako anaogombea kama hana uwezo usimchague achana naye. Tunataka rais mwenye sera za kuleta maendeleo kwa wote bila ya kujali itikadi za vyama vyao. Ikifika Oktoba 28 twendeni tukamchague Rais Dkt. Magufuli urais anaumudu.”
Ameyasema hayo leo (Jumapili, Oktoba 11, 2020) alipozungumza na wananchi katika mikutano ya kampeni wa kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM Rais Dkt. Magufuli, mgombea ubunge jimbo la Muheza, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM. Mkutano huo ulifanyika kata ya Misalai, Muheza.
“Tunataka kiongozi atayeweza kupambana na wala rushwa na mafisadi, usimchague kiongozi ambaye yeye mwenyewe ni mla rushwa na waliomzunguka wote ni wala rushwa huyo hatufai. Tumchague Dkt. Magufuli ambaye anatoka kwenye chama chenye mipango inayotekelezeka na ana dhamira ya kuwatumikia watu wote hadi wa vijijini.”
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imedhamilia kuboresha maendeleo ya wananchi wake na kwamba itaimarisha kilimo cha chai na viungo wilayani Muheza pamoja na kutafuta wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha viungo ili kuviongezea thamani na kuongeza ajira hususani kwa vijana.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya CCM imedhamiria kujenga na kukuza uchumi shindani hususan kupitia sekta za viwanda na huduma za kiuchumi utakaowezesha ustawi wa wananchi wote hivyo itajenga kituo cha utafiti wa mazao ya chai na viungo wilayani Muheza ili kutoa fursa kwa wananchi walime kwa tija.
Akizungumzia kuhusu changamoto ya barabara, Mheshimiwa Majaliwa amesema tayari Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Amani – Muheza yenye urefu wa kilomita 34 ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM. “Kipindi cha 2020/25, Serikali itafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mombo – Mzeri – Muheza yenye urefu wa kilomita 42.”
Kuhusu nishati ya umeme, Mheshimiwa Majaliwa amesema zaidi ya vijiji 9,300 nchini vimefikishiwa umeme kutoka vijiji 2,018 mwaka 2015, hivyo hali ya upatikanaji wa umeme imeimarika, watumiaji wa umeme wameongezeka kutoka asilimia 35 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 85 hivi sasa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema gharama ya kuunganishiwa umeme vijijini imepungua kutoka shilingi 177,000 hadi kufikia shilingi 27,000 tu na kati ya vijiji 91 vya wilaya ya Muheza mkoani Tanga, vijiji 50 vimepelekewa huduma ya umeme na vijiji visivyokuwa na umeme ni 41 tu, ambavyo navyo vitafikishiwa huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment